TEKNOLOJIA YA KUHIFADHI MIILI YA BINADAMU NCHINI MISRI

0
746

Na JUSTIN DAMIAN


KWA wale ambao wamesoma historia au wanapenda kujua mambo ya kihistoria bila shaka ukiwauliza kuhusiana na nchi ya Misri watakuwa na mengi ya kuelezea. Hii ni kwa sababu kuna mambo mengi makubwa katika historia ya dunia yalifanyika katika nchi hiyo iliyopo jangwani.

Baadhi ya mambo ni pamoja na mapiramidi marefu yaliyojengwa mamilio ya miaka kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo kwa teknalojia ya ajabu ambayo wanasayansi wanapata kigugumizi kuielezea. Mapiramidi haya ni moja ya maajabu saba ya dunia na mpaka leo yapo. Binafsi nilipata kuyatembelea mapiramid hayo mwaka 2010, kwa hakika teknalojia iliyotumika ni ya kushangaza.

Jambo lingine muhimu lilotokea Misri ni ugunduzi wa kalenda. Wakulima waliokuwa wanalima kwa kutumia umwagiliaji, walioishi Misri mamilioni ya miaka wanaaminika ni watu wa kwanza kugundua na kutumia kalenda duniani. Haya ni baadhi tu ya matukio makubwa ya kihistoria yaliyogundulika nchini Misri.

Leo tutaangalia teknolojia nyingine muhimu ya kuhifadhi miili ya watu waliopoteza maisha (Mummification). Teknalojia hii ya kushangaza ambayo iliweza kuifanya miili ya wafu kutoharibika kwa mamilioni ya miaka, ilitumiwa na Wamisri kuhifadhi hasa miili ya watu mashuhuri kama wafalme wao miaka mingi kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo.

Wamisri wa zamani waliamini kuwa mfalme wao anapofariki, mwili wake ni lazima uhifadhiwe vizuri usiharibike ili kuwezesha roho yake kusafiri mpaka dunia nyingine ambako humfanya mfalme kuwa mmoja kati ya wafalme wanaoabudiwa na watu. Ili kuwezesha hili, miili yao ilihifadhiwa kwa ustadi mkubwa na kuwekwa kwenye mapiramidi.

Kimsingi waliamini kuwapo na maisha baada ya kifo na kwa hiyo walilazimika kuhifadhi miili ya wafalme ili roho zao zitakaporudi duniani tena zikute miili yao ikiwa katika hali nzuri.

Zoezi la kuhifadhi miili isiharibike lilikuwa likitumia teknalojia ngumu na likiuwa likifanyika kwa gharama kubwa. Watu wenye utajiri mkubwa pamoja na wafalme ndiyo waliweza kumudu gharama zake.

Kiongozi wa zoezi hili alikuwa ni Kuhani aliyevalia sura (mask) ya Anubis ambayo ilikuwa kama kichwa cha mnyama fisi. Anubis ni mungu wa wafu na ndiye ambaye alikuwa  akitoa baraka kabla ya zoezi hilo kufanyika ili liweze kufanikiwa.

Namna lilivyokuwa linafanyika

Kuhani huyo ambaye aliongoza timu ya watu wasiopungua watatu aliaanza zoezi hilo kwa sala maalumu mbele ya mwili kumuomba Anubis afanikishe zoezi hilo.

Baada ya hapo, aliingiza kitu kama ndoano ya kuvulia samaki kupitia kwenye shimo dogo karibu na pua na kisha kutoa sehemu ya ubongo.

Baada ya hapo alikata upande wa kushoto wa mwili karibu na tumboni kisha kutoa vitu nyote vilivyopo tumboni kama utumbo, maini, figo na vinginevyo.

Baada ya hapo viongo hivyo vya ndani hupakwa dawa maalum na kuachwa vikauke kabisa na baadaye mapafu, utumbo na maini huwekwa kwenye jagi maalumu ambalo huwekwa pamoja na mwili sehemu utakapohifadhiwa baada ya zoezi kumalizika na moyo hurudishwa kwenye mwili.

Mwili huoshwa kwa nje na ndani kwa kutumia mvinyo maalumu na viungo (spices) na baada ya hapo mwili hufunikwa na chumvi iliyo kama magadi kwa siku 70. Muda huo ukiisha mwili huoshwa na dawa maalumu kisha kufungwa bandeji kuanzia kishwani hadi miguuni na kuwekwa kwenye box linalofanana na jeneza.

Kama mwili ni wa mfalme, huwekwa kwenye chemba maalum ya kuzikia ukiwa na vitu vya thamani kubwa kama dhahabu na vinginevyo.

Ushahidi wa miili iliyohifadhiwa kwa njia hii upo hadi leo nchini Misri. Binafsi nilifanikiwa kuona jiwe maalumu kama kitanda ambalo hutumika kufanyia kazi hiyo katika Makumbusho yaliyopo Mji mkuu wa nchi hiyo Cairo. Nilifanikiwa pia kuona mwili uliofungwa ambao unadaiwa kufanyiwa uhifadhi wa aina hiyo lakini kwa bahati mbaya walikuwa hawaruhusu kupiga picha.

Wanasayansi bado hawajaweza kung’amua baadhi ya kemikali ambazo zilitumika kuweza kufanya miili isiharibike kwa miaka mingi na hivyo kufanya teknolojia hii kuwa ya ajabu na aina yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here