Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeteua timu ya wataalamu wabobezi wa habari, ili kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari zinazohusu mchakato wa mabadiliko ya sheria za habari nchini.
Jukwaa hilo limefanya kikao na wanataaluma washauri (mentors) wa waandishi hao Ijumaa Julai 15, 2022 kwa lengo la kuweka mikakati ili kufikia malengo.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, kimefanyika Julai 15, 2022 katika Ofisi ya TEF, jijini Dar es Salaam.
Akizunguza kwenye kikao hicho, Balile amesema lengo la uteuzi wa timu hiyo unalenga kuongeza chachu ya harakati kuelekea mabadiliko Sheria za Habari nchini.
“Tunapaswa kuwa na waandishi wabobezi katika harakati hizi, ndio maana tumeunda timu ya wanataaluma ambao watawasimamia waandishi ili waweze kupita njia itakayoleta mafanikio.
“Mimi kama mwenyekiti naamini, timu hii ya wataalamu wabobezi, itasaidia kwa kiwango kikubwa kunyoosha mwelekeo na hatimaye kupata matokeo chanya,” amesema Balile.
Wanataaluma walioteuliwa kusimamia waandishi hao ni Joseph Kulangwa, Mhariri wa Raia Mwema; Stella Aron, Mhariri wa Majira; Rashidi Kejo, Mhariri wa Mwananchi; Angela Akilimali, Mhariri wa TBC na Joseph Nakajumo na Midladjy Maez ambao ni Wahariri Wastaafu.
Angela Mang’enya amepangwa kuwakufunzi Fatma Hassan Ali (Channel Ten), Kissa Daniel (East Africa Tv), Faridy Mohammed (Mlimani Tv), Godfrey Monyo (ITV).
Joseph Nakajumo atawasimamia Christopher James (Radio One), Salma Juma (Classic Fm), Philip Nyiti (Clouds Media) na Brumo Bomola (Radio Tumaini).
Rashid Kejo atakuwa na waandishi Regina Mkonde (Mwanahalisi Online), Faraja Masinde (Mtanzania Digital), Brighter Davidi (Daily News Digital) na Iddy Lugendo wa Majira.
Joseph Kulangwa amepangiwa Alex Kazenga (Jamhuri Media), Peter Elias (Mwananchi), Mery Geofrey (Nipashe) na Goodluck Hongo wa Tanzania Daima.
Srella Aron atasimamia Anneth Nyoni (Tumaini TV), Humphrey Msechu (Spatklight TV), Jackline Martin (Times Majira) na Yusuph Digossi (IBN TV).
Kwenye timu hiyo, Maez atakuwa na kazi ya kupitia kazi na kuandika ripoti.