Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kwa kuonyesha ushirikiano kusikiliza na kutatua baadhi ya changamoto zilizokuwa zinavikabili vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa baadhi vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungiwa.
Hayo yamebainishwa Februari 10, 2023 jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile wakati akizungumza na Waandishi wa Habari.
Amesema jambo jingine wanalomshukuru Rais Samia ni pamoja kupunguza gharama za leseni za Luninga kutoka Sh milioni 73 kwa mwaka hadi 32.
“Tuliwasilisha Agenda 14 Ikulu kwa Mheshimiwa Rais na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dk. Samia kwani kati ya hizo agenda nyingi za kikanuni zimesharekebishwa lakini pia Februari 10,mwaka huu bunge lilipoisha tumeona mswada umesomwa na bunge limerejeshwa na litaonenywa mubashara kupitia vyombo vya habari,” amesema Balile.
Aidha, Balile amemshukuru Waziri wa Habari Mawasiliano na Tenolojia ya Habari, Nnape Nnauye kwa kuonyesha ushirikiano mkubwa kwa Jukwaa hilo kwani kuna baadhi ya changamoto nyingi walizokuwa wakikutana nazo katika zoezi zima kutafuta haki na uhuru wa vyombo vya habari ikiwa ni kuhakikisha kwamba yale yaliyokuwa magumu yaliweza kuwekwa katika usawa.
Ameongeza kwamba anamshukuru pia mwanasheria Mkuu wa Serikali kwani ameonyesha ushirikiano mkubwa na kuonyesha kwamba anapenda nchi hii iwe na sheria ambazo zina uhuru wa habari.
“Baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza mswada wa marekebisho ya sheria ndogo ndogo tunaamini wataweka kwenye website ya Bunge tutaisoma na pamoja tutaanza kuijadili tutaona kama yaliyomwo yatatusaidia kujenga Taifa lililo moja na kwamba kila mwanachi maoni yake yataheshimika na kusikilizwa.
“Sisi Jukwaa la wahariri tunapigania uhuru wa vyombo vya habari lakini sio kwa ajili ya waandishi wa habari tu ni kwa ajili ya wananchi wote kwani kila mwanachi ana haki ya kupata habari pamoja na haki ya kujieleza, na huu ndio utakuwa mwanzo wa demokrasia nchini, ukuaji wa utoaji mawazo, ukuaji wa nchi yetu, ustaarabu katika nchi yetu na tutakuwa na utawala bora na utawala wa sheria,” amesema Balile.
Kwa upande wake Mjumbe wa Jukwaa hilo, Said Salim amesema kwamba wanachokifanya TEF ni kile wanachokidai haki ya kujieleza Watanzania wawe watu wenye uhuru wa kujieleza, kusikia sauti za wananchi tofauti wakitoa maoni yao ndio utawala bora.
Naye, Angella Akilimani akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TEF amesema anaungana na Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri na waandishi wote kuishukuru Serikali kwa Mswada huo kusomwa bungeni kwa mara ya kwanza na ana Imani kwamba anategemea kuona sheria kandamizi sasa zitaondolewa na utakuwepo uhuru wa vyombo vya habari na maisha bora kwa waandishi habari.