NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limeelezea kupokea kwa masikitiko taarifa za mchezaji wa Simba, Mwinyi Kazimoto, kumpiga na kumshambulia mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Mwanahiba Richard na kulaani vikali kitendo hicho.
TEF imeutaka uongozi wa klabu ya soka ya Simba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuchukua hatua stahiki za kinidhamu dhidi ya mchezaji huyo kutokana na kitendo alichomfanyia mwandishi huyo akiwa kazini kwani huo ni ukiukwaji wa haki ya kufanya kazi kwa uhuru bila kubughudhiwa na kupigwa.
Inadaiwa kuwa Februari 10, mwaka huu Kazimoto alimpiga na kumuumiza mwandishi huyo katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati akitimiza wajibu wake wa kukusanya habari.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa TEF, Theophil Makunga, imeeleza kuwa mchezaji huyo alitumia ngumi na makofi kutimiza uovu wake dhidi ya Mwanaiba huku akimtuhumu kwamba aliwahi kumuandika vibaya gazetini.
Taarifa hiyo ilieleza kwa kuwa tukio hilo limeshafunguliwa jalada polisi mjini Shinyanga, TEF inatarajia kwamba Jeshi la Polisi nchini litalichukulia kwa uzito ili mtuhumiwa afikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu mashtaka ya kumshambulia mwandishi huyo na kumjeruhi.
“Tunaliomba Jeshi la Polisi litekeleze wajibu wake katika suala hili kwa ukamilifu na kwa hali, tunatoa rai kwa wanamichezo na umma kwa ujumla kwamba kama kuna malalamiko yoyote ya kutokutendewa haki na vyombo vya habari au mwandishi mmoja mmoja ni vyema hatua stahiki zikachukuliwa kama jamii iliyostarabika inavyofanya
“TEF kama mdau muhimu kwenye tasnia ya habari haiwezi kufumba macho na kubariki udhalilishaji kama huu, hivyo tunalaani kitendo cha Kazimoto kumpiga na kumjeruhi Mwanaiba,” ilieleza taarifa hiyo.