NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limepinga uamuzi wa serikali wa kulifuta kwenye daftari la msajili gazeti la Mawio kwa madai ya kuandika habari za uchochezi.
Pia limeitaka Serikali kutafakari upya na kwa kina uamuzi wake huo ambao TEF inautafsiri kama mwendelezo wa ukandamizaji wa tasnia ya habari.
Tamko la TEF lilitolewa Dar es Saalam jana na Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda na Katibu wake, Neville Meena.
Walieleza kutoridhishwa na nia ya serikali ya kupatikana kwa sheria bora ambazo imeahidi kuzifanyia kazi kuhusu tasnia ya habari.
Akisoma tamko hilo Meena alisema:
“Hii ni aina mpya ya ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini kwani serikali zilizopita zilikuwa zikipambana na vitendo vya kufungiwa kwa magazeti kwa muda maalum lakini si kuyafuta”.
Meena alisema katika serikali zilizopita adhabu kubwa iliyowahi kutolewa ilikuwa ni kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kabla gazeti hilo kurejeshwa kwa umma na mahakama, kufungiwa siku 90 gazeti la Mtanzania na siku 14 gazeti la Mwananchi.
“Kwa kuwa hii inaonekana ni dhamira rasmi ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kutumia sheria kandamizi kudhibiti demokrasia na uhuru wa habari, tunatoa wito kwa watawala wetu kutafakari upya suala hili na kuachana kabisa na dhamira hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu.
“Uamuzi wa kufuta Mawio (hata kama lilifanya makosa) umetufikirisha sana, tumetafakari kwa kina na kujiuliza kwamba habari ambazo ziliandikwa na gazeti hili zilikuwa hatari kwa kiasi gani kwa nchi kiasi cha kufikiwa uamuzi huo? Ni magazeti mangapi yatafuata baada ya Mawio ikiwa serikali itaendelea na ubabe wa aina hii?” alihoji Meena.
Katika hoja zake TEF imesema mfumo wa sasa wa kushughulikia matatizo au kasoro za taaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi kwa vile unamfanya Waziri kuwa ‘Mhariri Mkuu’ na ana mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata kama utakuwa unakinzana na misingi ya taaluma.
“Tunajiuliza ikiwa kwa miezi takriban mitatu tu tangu kuanza kazi serikali mpya (Novemba 5 mwaka jana alipoapishwa kuwa rais), serikali ya Dk Magufuli tayari imefuta gazeti moja itakuwaje katika safari ya miaka mitano ambayo atakuwa madarakani?” alihoji Meena.
Katibu huyo alisema kwa taaluma ya habari, Serikali bado imeendelea kujipa mamlaka ya “kukamata, kushtaki, kusikiliza kesi, kuhukumu na kufunga” kwa sababu kama ilikuwa ni kesi iliyozaa hukumu ya kufutwa, basi uendeshaji wake ulifanyika katika “mahakama ya siri”.
Alisema usiri huo matokeo yake ni hukumu ya siri ambayo haikuwapa wahusika kutoa utetezi wa kile kilichokuwa kikilalamikiwa dhidi yao.