24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TEC: Ukawa rudini bungeni

Askofu Severine Niwemugizi
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi

NA RAYMOND MINJA, IRINGA

KANISA Katoliki Tanzania limeutaka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kurudi ndani ya Bunge hilo bila masharti yoyote.

Pia baraza hilo limewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuikataa Katiba itakayochakachuliwa na kuwanyima kura wanasiasa watakaosababisha hali hiyo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi, wakati akizungumza katika kilele cha Jubilee ya miaka 25 ya uaskofu wa Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, ambaye ni Rais wa Baraza hilo na Askofu Mkuu wa Jimbo la Iringa iliyofanyika katika viwanja vya jimbo hilo, Kichangani mjini Iringa.

Askofu Niwemugizi ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo la Rulenge Ngara alisema nchi haiko salama na imeanza kupata mpasuko katika maeneo mbalimbali likiwemo eneo hilo la mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya.

“Ndani ya Bunge tunashuhudia watu tuliowaheshimu na kuwapa dhamana ya kufanya kazi hii muhimu wasivyojiheshimu na wala kuwaheshimu Watanzania waliotoa maoni yao,” alisema.

Alisema pamoja na Bunge hilo kutumia kodi za Watanzania, maoni yao yanaelekea kupigwa teke huku baadhi ya wanasiasa wakidharau kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Katiba iliyoundwa na Watanzania wasomi, wakiwemo baadhi ya wanasiasa waliopata kushika nafasi nyeti serikalini.

“Ukawa rudini bungeni mkashirikiane na wenzenu kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba, kama itachakachuliwa, Kanisa linatoa wito kwa Wakristo na Watanzania kwa ujumla wao kuikataa kupitia sanduku la kura ya maoni,” alisema.

Alisema nchi haiko salama na inazidi kupoteza dira tofauti na walivyoifahamu wakati wa utawala wa waasisi wa Taifa.

“Usalama wetu na mali zetu uko mashakani, nchi inanuka rushwa, ubinafsi umetawala, tuliowapa dhamana hawajali na wanajiingiza pia kwenye maovu na kufanya biashara haramu zikiwemo za dawa za kulevya, nchi imekuwa ya matajiri wachache dhidi ya maskini wanaozidi kuongezeka,” alisema.

Aliwataka Watanzania waweke uzalendo mbele kwa kukataa mizengwe itakayojitokeza wakati wa kutengeneza Katiba hiyo.

Alisema wakati nchi ikijiandaa kuboresha daftari la mpiga kura, Watanzania wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kurekebisha taarifa zao ili uchaguzi mkuu wa mwakani wautumie vizuri kuwanyima kura wanasiasa watakaochakachua maoni ya wananchi katika Katiba hiyo.

“Tusipuuze jambo hili, Katiba ni mlinzi wa maisha yetu, ni mlinzi wa imani zetu, tukifanya mzaha tutakwenda na maji. Mambo ya uchaguzi yanahusu maisha yetu, tusiwakubali wanasiasa wanaochezea maisha yetu,” alisema.

Akifafanua maoni ya kanisa hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo alisema: “Askofu Niwemugizi ni rafiki yangu na katika suala ambalo ananigusa siku zote ni tabia yake ya uwazi.”

Alisema Serikali na Watanzania wanatakiwa kuendelea kuwatia moyo viongozi wa dini na hakuna sababu ya kuzua vita nao pale wanapowakosoa viongozi na Serikali yao.

Alisema kinachoendelea katika mchakato huo ni kuboresha mapendekezo yaliyoletwa na tume hiyo ikiwa ni pamoja na kuangalia kama Watanzania wanataka Serikali tatu, mbili, moja au ya shirikisho kama walivyopendekeza.

“Naomba wote bila kujali tunatoka wapi ili mradi tumepewa dhamana turudi bungeni kama ilivyoshauliwa na Askofu, tukabishane pale ndani. Na ni lazima tujue kwamba kazi tutakayoifanya itakuwa sawa na bure kwasababu ili tuwe na Katiba Mpya ni lazima Watanzania waipigie kura,” alisema.

Kuhusu uchaguzi mkuu wa mwakani, Pinda alisema Watanzania wanatakiwa kuchagua kiongozi bora asiye na sifa za Goliati zilizotajwa katika Biblia.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Nashukuru kwa kuendelea kutuhabarisutuhaba.maoni yangu ni kuwepo kipengere kitakachokuwa kikijali muelekeo wa nchi yetu ili tujue ni wapi pa kusimamia mara baada ya kujua msimamo wa watawala wetu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles