Na Ramadhan Hassan, Dodoma
KATIKA mwaka wa fedha 2023-2024 Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imepanga kutumia Sh bilioni 8 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Hayo yameelezwa leo Agosti 10,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Bahati Geuzye wakati akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha mwaka 2023-2024 kwa Waandishi wa Habari.
Mkurugenzi huyo amesema kiasi hicho kitatumika kufadhili miradi 82 katika shule 81 zikiwemo shule 48 za msingi na 33 za sekondari katika maeneo mbalimbali Tanzania Bara.
Amesema miradi hiyo itakapokamilika itanufaisha wanafunzi 39,484 na walimu 169 katika shule za msingi na sekondari.
Amesema miradi itakayofadhiliwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 82, matundu ya vyoo 336, mabweni 10, ujenzi wa maabara 18 za masomo ya sayansi na nyumba za walimu 32.
Mkurugenzi huyo amesema katika mwaka huo wa fedha TEA itatoa ufadhili kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu na kuwezesha ununuzi wa vifaa vya kujifunzia na kufundisha katika Taasisi Moja ya Tanzania ambapo mradi huo umepanga kutumia Sh milioni 300 katika utekelezaji wake.