28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

TDI kupanda miti 1,500, kuchimba kisima shule ya Nyamilama

Na Mwandishi wetu, Mwanza

KATIKA kuhakikisha wanakabiliana athari za mabadiliko ya tabianchi, Shirika la Together Development Initiative (TDI) lililopo Nyakato jijini Mwanza limeamua kupanda miti 1,500 ya matunda, kivuli, mbao na dawa katika shule ya msingi Nyamilama wilayani Magu na kuchimba kisima cha maji.

Miti hiyo itapandwa katika shule hiyo iliyopo kijiji cha Lugeye kata ya Kitongosima, Magu kupitia mradi wa mabadiliko ya tabianchi unaofadhiliwa na Shirika la Global Fund la nchini Marekani, ambao umezinduliwa leo shuleni hapo huku walimu na baadhi ya watendaji wa Serikali katika kata hiyo wakipewa elimu ya uhifadhi mazingira.

Akizungumzia mradi huo, Afisa Programu wa shirika la TDI, Gozbert Mutta, amesema lengo la mradi wao ni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Kata ya Kitongosima na kuona hali ya hewa inakuwa ya kijani ikiwemo kupanda miti na kuitunza ambapo wanatarajia kuutekeleza ndani ya miezi mitano kuanzia sasa.

Amesema kupitia mradi huo watatoa elimu ya uoteshaji miti, kuipanda na kuitunza, ambapo wanafunzi wa klabu za mazingira watapata elimu hiyo kisha watawafundisha wengine shuleni hapo kutunza mazingira, huku jamii inayozunguka shule hiyo ikijifunza namna ya utunzaji mazingira na upandaji miti kupitia mfano wa shule hiyo.

“Tunategemea kupanda miti 1,500 ya matunda, mbao, dawa na kivuli itakayosaidia kutengeneza madawati ya shule ili Serikali isitumie fedha nyingi kila mwaka kutengeneza madawati, pia itaongeza oksijeni na ufaulu kwa wanafunzi, kupata dawa wanafunzi wanapougua ikiwa ni hatua ya kwanza kabla ya kwenda hospitalini, kuongeza lishe kwa wanafunzi na kutokomeza utapiamlo,” amesema Mutta

“Tunategemea wananchi wa kata hii watapata elimu ya uoteshaji miti na kuipanda kutoka hapa shuleni kwetu, kwakuwa tutakuwa tumepanda miti mingi hapa shuleni tunategemea pia kujenga kisima cha maji ambacho kitasaidia kupata maji ya kutosha yatakayotumika kumwagilia miti hiyo ikue,”

“Lakini pia maji hayo yatatumiwa na wanafunzi kupata maji safi na salama ya kunywa, wakati wote maji yatakuwepo miti yetu tutakayoipanda itaendelea kukua vizuri. Katika mradi huu tunategemea kata nzima ya Kitongosima itakuwa imepata elimu na itapanda miti ya kutosha ya kusaidia wananchi ili hali ya hewa ya hapa iwe ya kijani na iwe mfano kwa maeneo mengine,” amesema Afisa huyo

Afisa Kilimo Kata ya Kitongosima wilayani Magu, Theodora Sokone akitoa elimu ya umuhimu wa kilimo cha bustani, kupima ubora wa udongo na upandaji miti ikiwemo ya matunda kwa walimu wa shule ya msingi Nyamilama wakati wa uzinduzi wa mradi wa mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa na Shirika la Together Development Initiative (TDI) shuleni hapo.

Mwalimu Mkuu wa shule ya Nyamilama, Faith Katunzi amesema anaamini mradi huo utakuwa na faida kubwa katika shule yake huku akishauri utekelezwe kwa mafanikio ili kuboresha mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema shule yao yenye ukubwa wa ekari 33 imekuwa ikifanya jitihada za kupanda miti lakini inakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji kwani wanategemea kisima kimoja cha mtaa ambacho kinatumiwa na wananchi, hivyo, wanafunzi kujikuta wakipanga foleni na kupoteza muda mwingi nje ya madarasa.

“Tumeupokea mradi huu kwa furaha kubwa tunategemea ukianza utasaidia kuboresha mazingira ya shule yetu wametuahidi kutuletea maji, katika eneo hili maji ni changamoto kubwa kwahiyo tukipata hicho kisima tutaboresha mazingira, maua na eneo letu la shule na litakuwa la kijani,” amesema Katunzi na kuongeza;

“Kwahiyo kisima chetu pia kitaweza kuwahudumia wananchi na kutatua kero ya maji, tumejitahidi kupanda miti ya aina nyingi lakini changamoto ni ukame mingi haikui. Tunategemea tukipata maji tutaotesha miti miti na tutakuwa na mazingira mazuri zaidi,” amesema

Naye, Afisa Kilimo Kata ya Kitongosima, Theodora Sokone, ameiomba jamii ya eneo hilo kushirikiana kuhakikisha mradi unaanza na kwenda vizuri, huku akiwataka kulinda miti itakayopandwa na kuitunza wapate faida zilizokusudiwa kwenye mradi huo.

Mwanafunzi wa darasa la saba katika shule shule ya msingi Nyamilama, Amos Martin, amesema “Tutaitunza miti hiyo kwa kuiwekea mbolea na kuimwagilia mara kwa mara kwa sababu miti hutusaidia mambo mbalimbali na tutatoa elimu kwa wazazi wetu wasikate miti hovyo ili tuweze kulinda mazingira yetu kwa vizazi vijavyo,”

“Tunashukuru shirika la TDI kwa kutuletea miti tunaahidi tutaitunza vizuri na kuhakikisha inakua. Pia tunashukuru kwa kutuletea kisima cha maji ambapo tutapata maji ya kunywa na kumwagilia miti yetu,” amesema Martin.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles