27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

TDB yaipongeza Tanzania ujenzi wa reli

Mwandishi wetu -Dar es salaam

RAIS na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), Dk. Admassu Tadesse ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) kwa kutumia fedha zake za ndani na kuahidi kuwa benki yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inatafuta fedha za kujenga reli hiyo.

Dk. Tadesse ametoa kauli hiyo juzi, alipotembelea sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo, kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na kujionea kazi kubwa iliyofanyika.

Alisema mradi huo hautainufaisha Tanzania peke yake, bali pia nchi za ukanda wa Afrika, hususan ambazo hazipakani na bahari.

Kiongozi huyo wa juu wa TDB, alisema kuwa mwaka huu benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani bilioni moja sawa na takribani Sh trilioni 2.3 kwa utekelezaji wa miradi yake mikubwa ya maendeleo.

Dk. Tadesse alisema Tanzania imenufaika pia na kiasi kingine cha zaidi ya dola bilioni moja zilizotolewa na benki yake miaka ya nyuma na ameelezea kufurahishwa na namna nchi inavyokua kwa kasi kiuchumi na kwamba inakopesheka.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, ameishukuru benki hiyo kwa kuonyesha nia ya kusaidia ujenzi wa reli hiyo katika awamu zinazofuata.

Kadogosa alisema kuwa hadi sasa ujenzi wa reli ya kisasa ambao umetumia fedha za ndani kati ya Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 72, huku kipande cha Morogoro hadi Makutupora mkoani Singida kikiwa kimekamilika kwa asilimia 22.

Alisema kuwa Serikali inatafuta fedha nyingine kujenga reli hiyo kuanzia Makutupora, Tabora, Isaka hadi Mwanza na kwamba watafanya mazungumzo na benki hiyo kuona namna watakavyofadhili ujenzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles