Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imewataka Watanzania kuacha kununua maziwa kiholela badala yake wanunue yaliyothibishwa ubora kuepuka maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama.
Kulingana na bodi hiyo magonjwa yanayoweza kusababishwa kwa kunywa maziwa yasiyo salama ni pamoja na Kifua Kikuu, magonjwa ya kuharisha na Brucella ambao unafanana kwa karibu na malaria.
Akizungumza Mei 21,2024 wakati wa semina kwa Waandishi wa habari kuhusu Wiki ya Maziwa kuelekea Siku ya Unywaji Maziwa inayoadhimishwa Juni Mosi kila mwaka, Msajili wa TDB, Profesa George Msalya, amesema upo uwezekano mkubwa wa maziwa kusababisha changamoto ya afya kwa walaji endapo hayatafahamika ubora wake.
Ametoa mfano wa magonjwa yanayoweza kusababishwa kwa kunywa maziwa yasiyo salama kuwa ni pamoja na Kifua Kikuu, magonjwa ya kuharisha na Brucella ambao unafanana kwa karibu na malaria.
“Bakteria wako kila mahali na watu wengi wamepata magonjwa kwa sababu ya kunywa maziwa yasiyofahamika ubora wake, Brucella unaambukizwa kwa kunywa maziwa au kula nyama ya ng’ombe na unasababisha kutoka kwa mimba ya mnyama, ng’ombe 30 kati ya 100 wana Brucella…tatizo analopata ng’ombe mwenye Brucella hata mama mjamzito anaweza kupata,” amesema Profesa Msalya.
Profesa Msalya amesema mpaka sasa wamesajili wadau wa maziwa 7,000 tangu mwaka 2004 na kusisitiza kuwa yeyote anayetaka kufanya biashara ya maziwa ni lazima asajiliwe na bodi hiyo.
Amesema pia viwanda vya uzalishaji maziwa vipo 152 wakati vituo vya kukusanyia maziwa ni 252 huku bodi ikitarajia kujenga vituo vingine 100.
Meneja Ufundi Maziwa kutoka TDB, Deorinidei Mng’ong’o, amesema zaidi ya virutubisho 100 vinapatikana kwenye maziwa na kuhimiza jamii kunywa maziwa ambapo kila mtu anatakiwa kunywa lita 200 kwa mwaka.
“Kuna upotoshwaji unaendelea kuhusu maziwa ya viwandani, maziwa ya viwandani ni salama kwa sababu yamepita katika mlolongo sahihi ikiwemo kuangaliwa ubora na kupimwa na wataalam,” amesema Mng’ong’o.
Kulingana na bodi hiyo mahitaji ya maziwa nchini ni lita bilioni 12 lakini zinazozalishwa kwa mwaka ni lita bilioni 3.9 hatua inayosababisha kuingizwa maziwa mengi kutoka nje.
Takwimu za bodi hiyo zinaonyesha kwa mwaka 2023 maziwa yaliyoingizwa kutoka nje ni lita milioni 11 zenye thamani ya Sh bilioni 23.
Mwaka huu TDB itaadhimisha Wiki ya 27 tangu ilipoanza maadhimisho hayo mwaka 1997 ambapo shughuli mbalimbali zinafanyika ikiwemo kutoa elimu kwa waandishi wa habari, shule, magereza na maeneo mengine kuhusu umuhimu wa kunywa maziwa.