Na Mwandishi wetu – Dar es Salaam
WAKATI wanafunzi waliohitimu kidato cha sita mwaka huu wakijiandaa kujiunga elimu ya juu, Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), imetoa ada elekezi ya udahili kwa vyuo vyote vya elimu ya juu kuanzia mwaka wa masomo 2017/18 ambayo itakuwa Sh 10,000.
Kabla ya kutolewa ada elekezi hiyo, wanafunzi walikuwa wanaomba kujiunga na vyuo kupitia mfumo wa TCU walikuwa wanalipa ada ya Sh 50,000 kila mmoja kuomba nafasi katika vyuo vitano.
Pia kabla ya TCU kuanza kutumia mfumo huo, kila chuo kilikuwa na ada yake ya udahili ambayo ilikuwa ni kati ya Sh 30,000 mpaka Sh 50,000, hivyo mwanafunzi aliyekuwa akiomba nafasi kwenye vyuo vitano ilibidi alipe hadi Sh 250,000.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya 12 ya vyuo vikuu, Mkuu wa Idara ya Ithibati TCU, Valerie Damian, alisema hakuna chuo kitakachotoza ada ya udahili zaidi ya kiwango kilichowekwa sasa.
“Tumeamua vyuo kudahili wanafunzi baada ya hapo majina yaliyodahiliwa yatapelekwa TCU, hivyo hapatakuwa na wanafunzi wasio na sifa na ukaguzi utakuwa mara kwa mara,” alisema Valerie.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa Jacob Mtabaji, alisema vyuo vinapaswa kudahili wanafunzi kwa kuzingatia ada iliyotangazwa na tume hiyo.
“Naomba niwasihi viongozi wa taasisi mbalimbali za elimu zilizopo kwenye maonyesho haya, wazingatie maagizo ya tume na ada ya udahili isizidi Sh 10,000 … chuo kitakachokaidi maagizo sheria itachukua mkondo wake,” alisema.
Alisema TCU imeandaa mwongozo utakaowasaidia wanafunzi kujua ni programu zipi zimepewa uhalali wa kufundishwa kwenye kila chuo.
Profesa Mtabaji alisema mwongozo huo utawasaidia wanafunzi kujua kikomo cha kuomba udahili na kujiridhisha kama ataweza kumudu gharama za chuo alichoomba.
Alisema kila chuo kitengeneze mfumo ambao utakuwa rahisi kwa mwombaji kupata taarifa ya chuo husika ikiwa ni pamoja na kutumia mfumo wa mtandao.
MAJALIWA APIGILIA MSUMARI VYUO VILIVYOFUNGIWA
Wakati huohuo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Simon Masanjila, wamevitaka vyuo vikuu vilivyozuiwa kudahili wanafunzi kwa mwaka mpya wa masomo 2017/18, viache kutafuta njia za mkato na badala yake virekebishe kasoro zilizojitokeza.
Wametoa kauli hiyo ikiwa ni siku tatu tangu TCU ivifungie vyuo 19 kudahili wanafunzi wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/18, huku ikifungia fani 75 kutoka vyuo 22 vikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu Mzumbe.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Majaliwa alivitaka vyuo hivyo kuhakikisha vinamaliza kasoro hizo na kuomba kuhakikiwa badala ya kulalamika katika vyombo vya habari.
“Mabadiliko haya yanalenga kuhakikisha tunaendana na matakwa ya dhati ya taaluma ili kujiingiza katika ushindani.
“Hivyo kila mmoja apokee na ajikite katika marekebisho ya mabadiliko hayo na kuacha kulumbana katika vyombo vya habari na makongamano,” alisema Majaliwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Simon Masanjila, alivitaka vyuo vyote vilivyozuiwa kufanya udahili kuondoa kasoro zilizopo na kuomba kukaguliwa tena ili viruhusiwe kuendelea na udahili.
“Vyuo hivyo ni bora vikaondoa kasoro zilizobainika, maana vingine vimeanza kutafuta njia za mkato.
“Hata mimi nimepokea simu, ni vema vikamilishe taratibu vipeleke majibu TCU viombe kukaguliwa,” alisema.
Elimu ya kujiajiri
Katika hatua nyingine, Majaliwa aliagiza TCU na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha vyuo vinatoa wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kumudu ushindani katika soko la ajira.
Alisema kwa sababu hiyo vinapaswa kuangalia mitaala ya vyuo inayotumika kama inaendana na mabadiliko yanayotakiwa.
Alivitaka vyuo kuongeza mikakati ya udahili na a kozi zinazohusu masuala ya gesi na mafuta ili kupata wataalamu watakaotumika katika sekta hiyo ambayo awali haikuwa na wataalamu.
“Wanafunzi watumie maonyesho haya kujifunza sifa na ubora wa vyuo mbalimbali kujua kozi wanazopenda,” alisema Majaliwa.
Alisema vijana wapya wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka ni kati ya 650, 000 hadi 750,000 hivyo lazima elimu inayotolewa iwawezeshe kujiajiri.
Waziri Mkuu alisema bado kuna matatizo katika mfumo wa elimu nchini yanayotakiwa kurekebishwa kutokana na upungufu uliopo katika mfumo wa elimu.
Naye Mkuu wa Chuo cha Aga Khan cha Dar es Salaam, Profesa Joe Lugalla, aliiomba Serikali kuondoa baadhi ya vikwazo vinavyovikabili vyuo binafsi ikiwa ni pamoja na ucheleweshwaji wa vibali vya kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi.
Prosefa Lugolla alisema katika wakati huu wa kuelekea uchumi wa viwanda ni lazima vyuo vyote viwe na uwezo wa kutoa wataalamu wenye ujuzi wenye kuendana na matakwa ya maendeleo.
“Ndiyo maana sisi tumeamua kuwekeza katika masuala ya afya na elimu kwa sababu hakuna nchi inaweza kuendelea kama watu wake hawana afya njema ,wala kwa kuwa na watu wajinga.
“Lazima iwe elimu yenye kuleta mabadiliko na inayowezesha wananchi kutatua changamoto na matatizo yao,” alisema Profesa Lugalla.
*Habari hii imeandaliwa na LEONARD MANG’OHA, MWANAIDI MZIRAY(TSJ) na ABDALLAH NG’ANZI (Tudarco)
PONGEZI KWA HATUA KUPUNGUA KWA GHARAMA ZA UDAILI VYUONI
MAONI SHULE ZA SEKONDARI ADA YA UDAHILI IPUNGUE IWE CHINI KWA ASILIMIA KUMI YA ADA YA UDAHILI YA VYUO VIKUU.
IMEKUWA BIASHARA YA KUJIPATIA FEDHA KIRAHISI KWA WAMILIKI WA SHULE HIZO.