26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

TCU yafuta usajili vyuo vikuu tisa

Mwandishi wetu-Dar es salaam

TUME ya Vyuo Vikuu (TCU) imefuta hati za usajili wa vyuo vikuu vishiriki vitano, vyuo vikuu vitatu na chuo kikuu kishiriki kimoja, kupitia kikao chake cha 97 kilichofanyika Januari 20.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaama jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, alisema vyuo hivyo vimeshindwa kujirekebisha na hata vingepewa muda zaidi visingeweza.

Alivitaja vyuo vishiriki vilivyofutiwa hati za usajili kuwa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Yakobo (Ajuco), Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa (CARUMUCo), Chuo Kikuu cha Theofilo Kisanji (Teku-Dar es Salaam), Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania kituo cha St Marks na Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo tawi la Arusha (JKUA).

“Kufuatia mashauriano na maombi yaliyofanywa na wamiliki wa vyuo na tume katika kikao chake cha 97 kilichofanyika Januari 20, 2020, imeridhia maombi ya wamiliki hao kusitisha utoaji wa mafunzo, hivyo tume imefuta hati za usajili wa vyuo hivyo vishiriki na kuvifutia vibali,” alisema Profesa Kihampa.

Alisema TCU pia imefuta hati za usajili wa vyuo vitatu ambavyo ni Chuo Kikuu cha Josiah Kibira (Kagera), Mount Meru (Arusha) na IMTU (Dar es Salaam).

Chuo kikuu kishiriki kilichofutiwa usajili ni Chuo Kikuu cha Bagamoyo (Pwani).

“Licha ya tume kutoa ushauri na mafunzo ya namna mbalimbali za kuboresha mazingira ya kufundisha na kufundishia pamoja na muda wa kufanya maboresho kwenye maeneo mbalimbali kwa zaidi ya miaka mitatu, baadhi ya vyuo havikufanikiwa,” alisema Profesa Kihampa.

Alisema katika ukaguzi wa mwaka jana, vyuo 19 vilikutwa na kasoro kubwa  na kupewa ushauri na muda wa marekebisho, lakini havikuweza kurekebisha katika kipindi kifupi na hivyo kuwazuia kudahili wanafunzi wapya kuanzia mwaka wa masomo 2017 na 2018.

Profesa Kihampa alisema kati ya vyuo 19 vilivyotakiwa kufanya marekebisho, vinane vilivyokuwa vimefungiwa mwaka 2017 vilifanikiwa na kuruhusiwa kuendelea na udahili.

Alivitaja vyuo hivyo vilivyoruhusiwa kuendelea kutoa mafunzo kwa baadhi ya programu za masomo kuwa ni Chuo Kikuu cha Umoja wa Afrika Tanzania (UAUT), Chuo Kikuu cha Teofil Kisanji (Teku), Chuo Kikuu kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo Tabora (Amucta) na Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala  nchini Tanzania  (KIUT).

Vyuo vingine vilivyoruhusiwa kutoa mafunzo ni Chuo Kikuu cha Marian (MARUCo), Chuo Kikuu kishiriki cha Uhandisi na Teknolojia cha Mtakatifu Yosefu (SJUCET), Chuo Kikuu kishiriki cha Kikristi cha Tiba Kilimanjaro (KCMCo) na cha kumbukumbu cha Stefano-Moshi (SMMCo).

Hata hivyo, alisema tume imeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu kuhusu hali ya ubora katika vyuo ambavyo bado vilikutwa na mapungufu ya ubora na taratibu za kisheria zitafanyika.

“Lakini tume imerejesha udahili wa wanafunzi wapya kwa chuo kimoja kuanzia mwaka wa masomo wa 2020/2021 ambacho ni Mtakatifu Fransisco (SFUCHAS) baada ya kurekebisha mapungufu waliyokuwa wamekutwa nayo awali na kuwafanya kukidhi vigezo vya ubora.

“Pia imeridhia maombi ya wamiliki kufuta vyuo vikuu vishiriki viwili na vituo vitatu vya vyuo vikuu baada ya mashauriano na maombi yaliyofanywa na wamiliki na kuruhusiwa kusitisha utoaji wa mafunzo,” alisema Profesa Kihampa.

UAMUZI WA MWAKA 2017

Julai 2017, TCU ilitangaza kuvifutia udahili vyuo vikuu 19 nchini.

TCU pia ilifuta kozi 75 katika vyuo 22 kwa sababu ya kukiuka sheria, taratibu na kanuni za utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.

Akitangaza uamuzi huo awali, Ofisa Habari wa Tume, Edward Mkaku alisema uamuzi wa kuvifutia udahili baadhi ya vyuo ni kutekeleza agizo la Serikali lililoitaka taasisi hiyo kuvisimamia kwa karibu vyuo ili viweze kutoa elimu bora.

Aliongeza kusema kuwa vyuo ambavyo wanafunzi wanaendelea na masomo, mabadiliko hayo hayatawahusu wanafunzi waliopo, isipokuwa vyuo hivyo havitaruhusiwa kudahili wanafunzi wapya kwa mwaka huo wa masomo.

Pia baadhi ya sababu za vyuo hivyo kufutiwa udahili wa Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu ilikuwa ni kukosa vitendea kazi na wataalamu katika kufundisha elimu ya juu.

Alivitaja baadhi ya vyuo vilivyokuwa vinatoa taaluma za afya kama Kilimanjaro Christian Medical College (KCMC) cha mkoani Kilimanjaro, Kampala International University (KIU) na Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) vya Dar es Salaam ambavyo vilikuwa vikitoa kozi za udaktari, ufamasia pamoja na shahada ya uzamili katika udaktari wa magonjwa ya wanawake imebainika kuwa hawakuwa na vifaa na wataalamu wa kutosha kufundisha kozi hizo.

Vyuo vingine ni St. Joseph, St. John, Tumaini University pamoja na vingine kadhaa ambavyo havina walimu pamoja na vifaa kwa mujibu wa maelekezo ya tume.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles