26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

TCU IRUDIE UHAKIKI WA TAARIFA ZA WANAFUNZI

NI kawaida mjadala kuhusu elimu ya hapa nchini kuibuka na kupotea. Kiini hasa ni wasiwasi wa wadau wengi juu ya ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi Tanzania. Ingawa idadi ya vyuo inazidi kuongezeka ubora wa elimu inayotolewa hauwaridhishi wadau wengi. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ndicho chombo kilichopewa kazi ya kuhakikisha vyuo vikuu vinadahili wanafunzi wenye sifa tu za kujiunga na elimu ya juu na si vinginevyo. TCU imezua mjadala mpya ulioleta mkanganyiko hapa nchini baada ya kutoa orodha ya wanafunzi zaidi ya 8,000 ikisema taarifa zao za uhakiki zina kasoro na hivyo wako hatarini kupoteza sifa za kuendelea na masomo ya chuo kikuu.

Kwanini umeleta mkanganyiko? Ni baada ya kutangaza baadhi ya wanafunzi kuwa hawana sifa za kujiunga na vyuo vikuu ingawa walishadahiliwa hapo awali.

Sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunasema taarifa hizo zina mkanganyiko kwa sababu kuna vyuo vimedai baadhi ya waliotajwa katika orodha hiyo walishamaliza masomo yao miaka mitatu iliyopita.

Mfano wa vyuo vilivyoilalamikia orodha hiyo ni Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut). Chuo hicho kimetajwa kuwa na wanafunzi 1,046 wasiokidhi vigezo. Saut imedai ilifuata taratibu zote za uhakiki na wanaishangaa TCU kwa kuja na taarifa walizodai kuwa ni za mkanganyiko. Pia TCU ilitoa orodha ya vyuo 52 ambavyo wanafunzi wake walidahiliwa kwa masomo wasiyostahili na kwamba walitakiwa kufanya uhakiki upya hadi ifikapo Februari 28, mwaka huu vinginevyo wangepoteza sifa za kuwa wanafunzi kwa masomo husika.

Kimsingi, tuna wasiwasi na umakini wa utendaji kazi ndani ya TCU. Taasisi hiyo ndiyo inayoidhinisha kwa mfano wale wenye stashahada zinazotolewa na vyuo vingine nje ya nchi. Cha ajabu ni TCU hiyo ndiyo inayodai kuwa baadhi ya wanafunzi walioorodheshwa hawana vyeti hivyo wakati vyuo husika vilipokea vyeti hivyo kutoka kwao. Kama kuna wanafunzi ambao taarifa zao zina utata ni wazi wataondolewa lakini kama alivyosema Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Florens Luoga, lazima muda utengwe kujua usahihi wa orodha ile na kama wapo wasio na sifa basi waondolewe kwa kufuata utaratibu.

Pia tunaungana na wadau wa elimu wanaosema Serikali kupitia TCU ndio wanaopaswa kubeba lawana juu ya kadhia hiyo. Pia hatupendi vyuo vyetu vya elimu ya juu kudahili wanafunzi wasio na vigezo.

Lakini tusingependa pia kuwa na taasisi inayoleta usumbufu hata kwa wanafunzi wenye sifa kwa sababu tu ya uzembe wa kushindwa kuwabaini wanafunzi wasio na sifa kwa wakati. Tunaishauri TCU kuwa ni vyema busara ikatumika ili utolewe muda wa kutosha zaidi wa kushirikiana na vyuo husika kupitia orodha hiyo kwa umakini zaidi ili kadhia kama hiyo isijirudie.

Pia tunaishauri irudie upya mchakato wake wa kuhakiki taarifa za wanafunzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles