Na Ramadhan Hassan, Dodoma
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema itahakikisha inasimamia maudhui yanayorushwa na vituo vya utangazaji nchini yanazingatia weledi na maadili ya uandishi wa habari.
Hayo yameeelezwa Novemba 3,2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Jabir Bakari wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mkurugenzi huyo amesema pia watahakikisha sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya utangazaji zinafuatwa.
Aidha, amesema sekta ya mawasiliano ya simu nchini imeendelea kukua hadi kufikia Septemba 2022 kulikuwa na laini za simu milioni 58.1.
“Ambazo zinajumuisha laini zinazotumiwa na watu na mashine kwa mashine.
Amesema mikoa inayoongoza ni Dar es Salaam laini milioni 9.756 Mwanza milioni 3.700 Arusha milioni 3.448 Mbeya milioni 3.089 na Tabora milioni 3.060.
Pia imesema gharama za kupiga simu kwa sasa zimepungua ukilinganisha na kipindi cha nyuma.
“Pia muunganisho wa simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka 2015 zilikuwa Sh 30.58 na kwa sasa ni Sh 2.00,”amesema
Amezitaja changamoto inazokabiliana nazo ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya mawasiliano.
“Utoaji wa huduma za mawasiliano kwa wote maeneo ambayo hayajafikiwa mahitaji makubwa ya bendi za masafa.
“Usalama wa mtandao na uhalifu mtandao kudhibiti maudhui ya mtandao na ubora wa huduma za mawasiliano,”amesema.
Aidha TCRA imesema kuwa inahakikisha mifumo ya usimamizi wa mawasiliano ya simu intaneti kwa serikali kuanzisha mfumo uitwao TTMS.
Amesema mfumo huo husimamia na kuratibu mawasiliano ya simu yenye uwezo wa kubaini takwimu mbalimbali zinazopita katika mitandao ya mawasiliano kwa watoa huduma.
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema serikali imetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 600 kwaajili ya mkongo wa taifa na kwa uwekezaji uliofanywa na serikali kupitia TCRA na uimara wa vyombo vya dola hakuna mtu anaeweza kufanya uhalifu mtandaoni akabaki salama.