Na Sheila Katikula, Mwanza
UONGOZI mpya wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) mkoani Mwanza umeahidi kuhakikisha unawaunganisha wafanyabishara wote mkoani hapa kulenga kujiimarisha kiuchumi na kisera ili kuendana na kasi ya maendeleo ya serikali ya awamu ya sita chini ya utawala wa Rais Samia Suluhu.
Akizungumzia malengo hayo, Mwenyekiti mpya wa TCCIA mkoani Mwanza, Gebriel Kenene alisema ili kufikia adhima hiyo ataanza kwa kujenga chemba imara za wafanyabishara kwenye wilaya zote zitakazoshiriki kikamitifu kutatua changamoto zinazowakabili sanjari na kuwatetea wafanyabiashara.
Alisema kwa kipindi cha uongozi wake TCCIA itatoa elimu ya mara kwa mara kwa wanachama wake na kuhakikisha wanashirikiana na kila sekta ya serikali kwenye shughuli za kisera na kimiradi ili kusaidia kukuza mawasiliano na mahusiano mazuri baina ya taasisi za serikali na binafsi.
Makamu Mwenyekiti wa TCCIA Mwanza upande wa Viwanda Mwanabure Ihuya alisema kusudio la uongozi huo mpya ni kufanya kazi kwa ukaribu na wafanyabishara wa makundi yote ikiwemo wanawake kulenga kuwawezesha waweze kupiga hatua kiuchumi.
Alisema akiwa miongoni mwa viongozi wapya atasimama imara na kuhakikisha anawashika mkono na kuwainua zaidi wanawake waweze kuchangamkia fursa zitakazojitokeza katika sekta za viwanda na kufikia hatua ya ushindani wa kibiashara.
Naye Makamu wa Rais wa TCCIA Mwanza aliyemaliza muda wake baada ya kuongiza kwa awamu mbili, Joseph Kahungwa amesema chemba hiyo ni taasisi muhimu kwa wafanyabishara kwani wanachama na wasio wanachama wananufaika kwa kutatuliwa changamoto zao kwa urahisi zaidi na kuepusha migongano na serikali.
Kahungwa amesema miongoni mwa mafanikio yakiyotokana na uwepo wa TCCIA ni wafanyabiashara kushirikishwa katika maboresha ya sera mbalimbali za serikali na kuweza kuondoa tozo nyingi ambazo siyo rafiki kwa wafanyabishara hivyo ni vyema kila mfanyabiashara ajiunge kwenye chama hicho.Â
Miongoni mwa nafasi ambazo zimepata viongozi wapya wa Chama hicho ni Mwenyekiti,Makamu Mwenyekiti biashara,Makamu Mwenyekiti viwanda,Makamu Mwenyekiti Kilimo na Wajumbe wa halmashauri Kuu Mwanza.