TBS walia nguo za ndani kuendelea kuingizwa nchini

0
579

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SHIRIKA la Viwango Nchini (TBS) limeomba msaada kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Maji na Mifugo wa jinsi ya kukabiliana na uingizwaji wa nguo za ndani za mitumba nchini.

Ombi hilo lilitolewa jijini hapa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk. Yusuph Ngenya alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli zinazofanywa na shirika hilo kwa Kamati ya Kilimo, Maji na Mifugo.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stela Manyanya.

Hoja ya nguo za ndani iliibuliwa na mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM) ambaye alitaka apewe majibu ni kwanini bado nguo za ndani zimeendelea kuingizwa nchini licha ya Serikali kukataza.

“Nguo za ndani zinatupa shida sana, tunaomba mtusaidie, zinaingizwa kwa kufichwa,” alisema Ndassa.

Akimjibu, Dk. Ngenya alisema wamekuwa wakifanya jitihada za kuhakikisha mitumba ya nguo za ndani kama chupi na zingine haziingii nchini.

Alisema wafanyabiashara wamekuwa wakiziingiza nchini kwa kuchanganya na nguo zingine hali ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu kubaini.

“Wanazificha kwa kuziweka ndani ya nguo za kawaida, naomba mtusaidie, naomba msaada wa kamati kuhusiana na nguo za ndani, hebu hili tusaidieni,” alisema Dk. Ngenya.

Alisema katika kipindi cha miaka minne, TBS imekusanya viwango 1,600 katika sekta mbalimbali sawa na asilimia 108.5 

“Mafanikio tumefanikiwa ujenzi wa jengo jipya la maabara ya kisasa ambalo litarahisisha utendaji kazi pamoja na urahisishaji wa vipimo,” alisema Dk. Ngenya.

Alisema mwaka 2016/17 hadi Desemba 2019  shirika limetoa gawio kwa Serikali Sh bilioni 36.4.

Dk. Ngenya alisema kwa sasa mambo yote yanaenda kwa mtandao na hakuna urasimu wala rushwa katika utendaji kazi wa shirika hilo.

Alisema kumekuwapo na ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani katika mambo mbalimbali.

Dk. Ngenya alisema wanakabiliwa na changamoto ya ongozeko la njia zisizo rasmi pamoja na uhaba wa vifaa vya kisasa kwa maabara.

“Tumekuwa tukifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya mipakani na tumeanzisha vituo vya ukaguzi na tumeongeza pale Tarakea na maeneo mengine.

“Tumeendelea kununua vifaa vya kisasa ili kuleta tija, lakini pia tumekuwa tukisaidiwa na wadau wa maendeleo,” alisema Dk. Ngenya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Mahmood Mgimwa, ambaye alikuwa mgeni mwalikwa kwenye kikao hicho, alisema TBS inatakiwa itoe elimu ya kutosha ili wananchi waweze kuijua.

“Mmesema changamoto mnayokabiliana nayo ni kuwepo kwa njia za panya, sasa mbona hamjasema kwamba mna uhaba wa watumishi ili wawasaidie kuzuia hizo njia za panya, lazima ‘one stop centre’ (kituo cha pamoja cha huduma) ijengwe,” alisema Mgimwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here