23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

TBS: TAULO ZA ELEA HAZIKIDHI VIWANGO

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TBS, Profesa Egid Mubofu
Kaimu Mkurugenzi Mkuu TBS, Profesa Egid Mubofu

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), limesema upimaji wa awali wa taulo za kike aina ya Elea, umeonesha bidhaa hiyo haijakidhi viwango na haipaswi kuingizwa sokoni.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu TBS, Profesa Egid Mubofu, alisema hayo kupitia taarifa yake aliyoituma kwa gazeti hili alipotakiwa kueleza endapo wanazitambua taulo hizo ambazo zimekwisha gawiwa katika shule mbalimbali nchini.

“Shirika lilipokea maombi ya kupima pedi zinazotumika zaidi ya mara moja (Re usable pads) kutoka Kampuni ya Malkia ambao ni wazalishaji wa bidhaa za Elea.

“Upimaji wa awali wa bidhaa hii, ulifanyika na matokeo yalionesha haikidhi kiwango cha bidhaa husika ambacho ni TZS 1659:2014, mzalishaji akatakiwa kufanyia marekebisho bidhaa hiyo,” alisema.

Mtengenezaji na mbunifu wa taulo hizo, Jenipher Shigoli alikiri kwamba bidhaa hizo hazijapewa alama ya ubora na TBS.

“Ni kweli nilipeleka bidhaa yangu TBS ikapimwa, lakini sikupewa ‘certificate’ ili nianze kuweka alama ya nembo ya ubora ya TBS, niweze kuzisambaza sokoni.

“Waliniambia kuna vitu natakiwa kuboresha kwa hiyo kama nilivyokueleza awali tunajenga kiwanda Kibaha mkoani Pwani, hivyo natarajia kitakamilika Machi, mwaka huu na nitakuwa tayari nimekamilisha vigezo walivyonitaka kuwa navyo,” alisema.

 

DAKTARI ANENA

Akizungumza na MTANZANIA jana, daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Belinda Balandya, alisema kipindi cha hedhi ni muhimu kwa afya ya mwanamke na anapaswa kuzingatia usafi wakati wote.

Alisema iwapo hatazingatia usafi wa mwili wake, anajiweka katika hatari ya kuziba kwa mirija ya uzazi hali ambayo inaweza kumsababishia tatizo la uzazi baadae.

“Mwanamke anapokuwa katika siku zake hulazimika kutumia taulo maalumu ambazo kazi yake kuu ni kupokea ile damu inayotoka, kama hatavaa maana yake ni kwamba itapitiliza kuchafua nguo zake.

“Kwa mfano, taulo za kutumia na kutupa jinsi zilivyotengenezwa zina ‘layer’ maalumu kwa ndani ambayo hufyonza damu ya hedhi, hulazimu kubadili mara nyingi (inashauriwa abadili kila baada ya saa nne),” alisema.

Alisema iwapo haitabadilishwa, maana yake inachochea bakteria kuzaliana kwa wingi ambao huwa wana uwezo wa kusafiri hadi kwenye mirija ya uzazi na kwenda kuziba.

“Damu ni sehemu ambayo bakteria huota kwa urahisi kwa sababu wanakuwa wanapata chakula wanachohitaji kwa urahisi, wengi hawajui hili na unaweza kukuta mtu amevaa kwa muda mrefu, kwa sababu hajui jambo hili, ni hatari,” alisema daktari huyo ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas).

Aliongeza: “Kwa kuwa bakteria hupata chakula chao na kuzaliana kwa wingi, baadaye husababisha pia muhusika kupata maambukizi katika sehemu zake za siri.

“Kwa kuwa taulo inakuwa imenyonya ile damu, ikikaa muda mrefu muhusika huhisi kabisa kama vile umevaa kitu kibichi na ngozi huanza kupata michubuko.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles