Ramadhan Hassan, Dodoma
Shirika la viwango Tanzania (TBS) linatarajia kutumia Sh bilioni 9.9 kwa ajili ujenzi wa maabara katika Kanda zote nchini.
Hayo yameelezwa leo Agosti 1, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dk. Athuman Ngenya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uelekeo na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Dk. Ngenya amesema kwasasa Shirika hilo lina maaabara moja jijini Dar es Salaam ambalo inalazimika kuhudumia nchi nzima hatua inayoleta usumbufu kwa watumiaji.
“Tukisogeza huduma karibu na wananchi muda wa kutoa majibu utapungua, sasahivi kwa mfano Bakery (duka la mikate) umetengenezwa Bukoba sasa ili kupata nembo ya ubora wa mkate ule unatakiwa utoke Bukoba kwenda Dar es Salaam.
“Kutokana na hali hiyo inaweza kusababisha mkate ule kuharibika au kukosa huduma,” amesema Dk. Ngenya.
Hata hivyo, amesema zoezi hilo tayari limeanza katika Kanda ya kati ambapo maabara imeanza kujengwa mkoani Dodoma na tayari imefikia asilimia 20 ya ujenzi huo eneo la Njedengwa.
Amesema baada ya ujenzi kukamilika Dodoma mkakati ni kujenga Maabara katika Mikoa kitovu ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma na Mtwara.
Aidha amesema Shirika litatumia Sh bilioni 1.2 kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya ukaguzi nje ya nchi kabla ya bidhaa kuingia nchini ili kupunguza kasi za kuingiza bidhaa nchini ambazo nyingine hukwepa njia za kukaguliwa.