26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TBL KUENZI WATEJA WAKE KUPITIA BIA CASTLE LITE

Na JUSTIN DAMIAN


MAENDELEO ya sayansi na teknolojia yamebadilisha kwa kiasi kikubwa namna ambavyo watu wanafanya biashara pamoja na wanavyotafuta huduma na bidhaa.

Maendeleo haya ambayo yanakwenda sambamba na utandawazi, yamesababisha kuongezeka kwa ushindani wa kibiashara. Dunia imekuwa kama kijiji na umbali si kikwazo kwa biashara. Watu wanaweza kununua bidhaa kutoka sehemu yoyote na kuzipata kwa urahisi.

Ushindani katika biashara siku zote huwa na faida kwa wateja kwa kuwa huwafanya kuwa na uchaguzi  mwingi wa aina ya bidhaa au huduma wanazozitaka. Uwepo wa bidhaa nyingi sokoni husaidia kushuka kwa bei kwa kuwa wauzaji hushusha bei  ili kuwavutia wateja wengi zaidi.

Katika mazingira ya kiushindani, makampuni pia hulazimika kutengeneza bidhaa nzuri na zenye ubora ili kuhakikisha wanawavutia wateja wengi kuliko washindani wenzao.

Moja kati ya biashara yenye ushindani mkubwa ni biashara ya bia  na vinywaji vyenye vileo. Pamoja na kwamba biashara hii imekuwa ikikua, ushindani uliopo ni mkubwa jambo ambalo hufanya makampuni yanayojihusisha na biashara hii kufanya kazi kubwa kuendelea kuwepo sokoni.

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ni moja kati ya kampuni kongwe za kutengeneza bia hapa nchini ambayo pamoja na kuwepo na mazingira ya ushindani mkubwa, imeendelea kuwa ni moja ya makampuni yenye wateja wengi zaidi.

TBL imekuwa ikipata ushindani kutoka kwa makampuni ambayo baadhi yao yamekuwa yakitengeneza  bia hapa nchini pamoja na mengine ambayo yamekuwa  yakiingiza bia kutoka nje ya nchi.

Ubunifu ni moja kati ya sababu ya kampuni hii kongwe kuendelea kuwa kinara sokoni, huku ikiwa ni mmoja kati ya walipa kodi wakubwa.

Ili kuendelea kuilinda nafasi yake katika soko, mwishoni mwa wiki iliyopita TBL kupitia moja ya bia yake inayopendwa ya Castle Lite, walizindua kampeni kubwa na ya aina yake ili kuwaleta wateja wake pamoja.

Kampeni hiyo itakayodumu kwa wiki 12, itawaleta karibu zaidi wateja wa kampuni hiyo ambao ni wanywaji wa bia ya Castle Lite, huku wakipata nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali.

Ikijulikana kama ‘Castle Lite Unlocks’, kampeni hiyo inafanyika katika nchi zote ambazo bia ya Castle Lite inauzwa na pia itatoa nafasi ya wateja wa bia hiyo kupata burudani kupitia tamasha kubwa la muziki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja masoko na huduma za wateja wa kampuni hiyo, George Kavishe, alisema kampeni hiyo itagharimu zaidi ya Sh milioni 700.

Kavishe aliwaambia waandishi wa habari kuwa, wateja wa bia ya Castle Lite watakapofungua chupa zao ndani ya kizibo, kutakuwa na zawadi kama muda wa maongezi wa Sh 10,000 ambazo wataweza kujishindia.

“Jumla ya muda wa maongezi wenye thamani ya shilingi milioni 30 utaweza kushindaniwa na wateja. Wateja wetu wa mikoani 1000 watalipiwa tiketi za ndege pamoja na malazi katika hoteli ya nyota tano wakati watakopokuja kwenye hitimisho la kampeni,” alieleza Kavishe.

Ikiwa ni moja ya kampuni ya bia yenye historia ya ubunifu, Kavishe alisema kampeni hiyo itaambatana na tamasha kubwa  la muziki linalotarajia kuvutia watu zaidi ya 15,000 watakaoshuhudia  wasanii mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi wakitumbuiza.

“Muziki ni sehemu muhimu ya maisha ya kila siku na ndiyo maana tumeona pamoja na zawadi, tuwape wateja wetu nafasi ya kupata burudani ya muziki kutoka kwa wanamuziki wanaowapenda huku wakifurahia bia yao ya Castle Lite,” aliongeza.

Meneja huyo alisema kampeni hiyo pamoja na mambo mengine, pia ina lengo la kuongeza wateja wa bia hiyo ambayo alieleza kuwa na mchango mkubwa katika mapato ya kampuni hiyo ya bia hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles