28.6 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

TBL Group yashinda tuzo ya Usalama, Afya 

22Na Mwandishi Wetu, Mbeya

KIWANDA  cha kutengeneza vinywaji vya TBL Dar es Salaam na TBL Mbeya, vimepata tuzo ya utekelezaji kanuni za Usalama na Afya  mahali pa kazi.

Tuzo hiyo hutolewa na Shirikisho la kimataifa la kusimamia masuala ya usalama mahali pa kazi lenye makao makuu nchini Afrika ya Kusini  lijulikanalo kama National Occupational Safety Association (Nosa).

Tuzo hii ambayo viwanda vya TBL Group vya Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam vimeipata mfululizo, imekuwa ikitolewa kutokana na kukidhi viwango vya kimataifa vya utekelezaji kanuni za afya,usafi na usalama mahali pa kazi ambapo wataalamu kutoka taasisi ya Nosa wamekuwa wakija nchini kufanya ukaguzi kwenye viwanda vyake ambapo  vimekuwa vikipata alama ya  kufanya vizuri kwenye kiwango cha nyota nne na nyota tano.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusherehekea tuzo  hiyo mwishoni mwa wiki katika kiwanda cha Ilala, Meneja TBL Dar es Salaam, Calvin Martin, alisema kampuni inajivunia kuendelea kufanya vizuri katika suala la usalama na afya mahali pa kazi ambapo mwaka huu imeshinda kwa kiwango cha nyota tano ambacho ni kiwango cha ufanisi cha hali ya juu.

“Tunayo sababu ya kusherehekea kupata tuzo hii tena katika kipindi cha mwaka huu kwa kuwa  inadhihirisha kuwa kampuni inajali suala la usalama na afya kwa wafanyakazi, na hili ni jambo la msingi kwa kuwa usalama na Afya ukikosekana mazingira yetu ya kufanyia kazi yatakuwa hatarini na  ufanisi hautakuwepo,” alisema Martin.

Aliwapongeza wafanyakazi wote kwa jinsi wanavyoshiriki kuzingatia kanuni na miongozo inayowekwa na kampuni, hali  ambayo inachangia kuleta mafanikio na kuvifanya viwanda vilivyopo chini ya TBL Group kuongoza kufanya vizuri na kuwa mfano wa kuigwa na viwanda vingine nchini.

Meneja wa Usalama na Afya kwa TBL, Renatus Nyanda, alisema kuwa kampuni imeweka mikakati kuhakikisha viwanda vyake vyote vinatekeleza kanuni za Afya na usalama kwa viwango vya kimataifa na ndio maana inaendelea kupata tuzo hizi za usalama zinazotolewa na taasisi za hapa nchini na nje ya nchi.

Aidha, meneja alitoa wito kwa wafanyakazi wote wa viwanda vya TBL Group kuendelea kutekeleza miongozo mbalimbali ya utendaji wenye kuleta ufanisi ili waendelee kuwa kioo hususani katika suala hili la usalama na afya kwa kuwa linawagusa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles