Na Brighiter Masaki, Mtanzania Digital
CHAMA Cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), kimewakutanisha wanahabari na kujadili nafasi zao katika kuonyesha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika ushiriki wa shughuli za kiuchumi.
Akizungumza katika mafunzo hayo jijini Dar es Salaam, Mwanahabari mkongwe, Edda Sanga amesema kuwa nafasi ya mwanamke na ushiriki wake katika shughuli za kiuchumi ni mkubwa na kuwataka wahabari kuwafikia na kuzionesha juhudi hizo zinazofanywa kwa jamii.
“Wanawake wanahitahi fursa, haki, usawa na ustawi na hili linajidhihirisha wazi wanawake wanajihusisha katika shughuli za uzalishaji mali kwa asilimia 90.4 kupitia kilimo hasa cha jembe la mkono na wanakidhi mahitaji ya chakula kwa nchi nzima kwa asilimia 70,” amesema.
Edda amewataka wanahabari kuwaibua wanawake waliopambana na kuleta matokeo chanya katika jamii, Taifa na familia zao kwa ujumla ili kuleta chachu kwa mabinti na kujenga taifa imara lenye haki na usawa hasa wa ushiriki wa shughuli za kiuchumi na biashara.
Katika semina hiyo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwamo ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za kiuchumi na biashara, vikwazo na namna ya kuwafikia wanawake wengi zaidi na kuvumbua jitihada zao zinazoleta matokeo chanya katika jamii.