Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori Tanzania(TAWA) wameitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro, Fatma Mwasa kwa lengo la kumsalimia, kujitambulisha na kumpa taarifa zinazohusu Uhifadhi mkoani humo.
Ziara hiyo imefanyika Septemba mosi, 2022 ikiongozwa na Kaimu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mabula Nyanda.
Katika salamu hizo, Kamishna wa Uhifadhi alimpatia taarifa ya shughuli mbalimbali ambazo TAWA inayashughulikia hasa katika Pori Tengefu la Kilombero, fursa na changamoto pamoja na hatua mbalimbali ambazo TAWA imeshachukua katika kukabiliana nazo.
Naye Mkuu wa Mkoa kwa upande wake ameishukuru TAWA kwa kufika ofisini kwake, kumkaribisha Morogoro na kuonyesha ushirikiano katika masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo katika mkoa huo.
Ameelezea kuwa kuna umuhimu mkubwa wa TAWA kwa mkoa wa Morogoro katika masuala ya Uhifadhi wa vyanzo vya maji ambavyo vimekua vikiharibiwa kutokana na uvamizi wa mifugo, ukataji miti na uchomaji wa misitu.
“Uwepo wenu hapa mkoani kwetu ni muhimu sana hasa ikizingatia watu zaidi ya milioni 11 wa mkoa wa Morogoro na maeneo jirani wanategemea maji ambayo vyanzo vyake ni kutoka katika mkoa wa Morogoro na nitashangaa sana kama mtaharakisha kuhamia Dodoma wakati bado unawahitaji sana katika masuala ya uhifadhi ili kulinda vyanzo vya maji ambavyo bila jitihada kubwa kuchukuliwa vyanzo hivyo vitakauka,” amesema Fatma Mwasa.
Kaimu Kamishna wa TAWA, Mabula Nyanda alimkabidhi Mkuu wa Mkoa Nembo ya TAWA na Jarida ambalo linazungumzia mipango na mikakati ya TAWA.