31.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

TATIZO SI HAPI, TATIZO NI BUNGE

KAULI ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Salum Hapi, kuwa amewatimua wabunge watatu katika ofisi kwenye majengo ya makao  makuu ya wilaya hiyo,  imezua mjadala mkubwa. Hapi ametangaza kuwatimua Halima Mdee ambaye ni Mbunge wa Kawe, Saed Kubenea anayeliwakilisha Jimbo la Ubungo na John Mnyika wa Kibamba. Wabunge wote hawa ni wa Chadema.

Pande mbili zimeibuka, moja ikimlaumu Mkuu huyo wa Wilaya kwa kitendo cha kuwafukuza wabunge hao huku kundi jingine likimsifia kwa kile alichokifanya.

Kwa bahati mbaya sana, jambo hilo limeupa mjadala huo sura ya kisiasa. Kwa kuwa waliofukuzwa kwenye ofisi wote ni wabunge wa chama cha upinzani, Chadema huku wengi wanaomlaumu Hapi wanatokea upande huo wakati wengi wa wale wanaotetea uamuzi wake, wanatoka upande wa pili kisiasa.

Matokeo yake, tatizo kubwa linalohusiana na jambo hilo, limeachwa pembeni katika mjadala. Wakati tatizo la msingi ni ukosefu wa ofisi za wabunge, wengi wamejikita kujadili uamuzi wa Hapi. Ukosefu wa ofisi ni tatizo linalowakabili wabunge wengi nchi nzima.

Ingawa wengi wakimlaumu Hapi kwa hatua yake hiyo, wabunge wanaohusika na sakata hilo wanakiri kuwa haikuwa sahihi kwao kuendelea kuwa na ofisi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Kinondoni baada ya kufanyika kwa mabadiliko ya maeneo ya utawala yaliyozaa Wilaya mpya ya Ubungo. Ndio maana, baadhi yao walishaamua kuondoka katika ofisi hizo ili kusogea karibu zaidi na wapiga kura wao. Saed Kubenea alishaachia ofisi hiyo na kujitafutia nyingine binafsi wakati John Mnyika hata hakuwahi kuitumia ofisi hiyo. Mnyika ana ofisi yake binafsi Kibamba na anasema haiyumkini kwa mpiga kura wake anayetokea karibu na Kibaha asafiri mwendo wote hadi Kinondoni kufuata huduma kwa mbunge wake.

Aidha, wakati watu wengi wakishupalia mjadala wa Hapi na wabunge wa Chadema, ukitembelea maeneo mengi utawakuta wabunge wana ofisi zao katika majengo ya Serikali, hasa hasa kwenye makao makuu ya wilaya. Hali haikupaswa kuwa hivyo kwa sababu ofisi nyingi za wilaya ni finyu sana kiasi kuwa majengo yaliyopo hayatoshelezi kwa mahitaji ya ofisi za idara na maofisa. Hivyo, kuwaleta wabunge katika ofisi hizo ni kuongeza mzigo ambao tayari ulishakuwa mkubwa.

Ndio maana miaka kadhaa iliyopita likatolewa agizo kuwa ofisi ya mbunge inayojitegemea ijengwe katika kila jimbo na kuwekewa samani zote zinazohitajika. Hii itawapatia wabunge mazingira mazuri zaidi ya kuwatumikia wananchi wao. Lakini pia itapunguza mbinyo kwenye ofisi za wilaya ambako hivi sasa wabunge wanalazimika kujibana.

Mwenye jukumu la kusimamia agizo hilo ni Ofisi ya Bunge. Kazi hii ya ujenzi wa ofisi za wabunge inapaswa kutengewa Bajeti kupitia Mfuko wa Bunge.

Agizo hili limetekelezwa kwa kiasi kidogo sana na inavyoelekea wahusika walishasahau kuwa wanapaswa kulitekeleza kwa sababu kwa kipindi kirefu sasa hakuna ofisi za wabunge zinazojengwa.

Kujenga kwa ofisi hizi za wabunge si tu kutasaidia kuondoa migongano kama hii ya Kinondoni ambayo sasa inaelekea kuchukua sura ya kisiasa, bali pia kutawapatia wabunge mazingira mazuri zaidi ya kuwatumikia wananchi wao.

Kwa upande mwingine, wananchi watakuwa na uhakika wa mahali ambapo wakimhitaji mbunge wao watampata kwa urahisi. Hivi sasa, watu wengi hawazifahamu ofisi binafsi zinazotumiwa na wabunge wengi. Lakini pia ujenzi wa ofisi za wabunge kutasaidia kupunguza shida za ofisi katika wilaya nyingi ambazo sasa zinalazimika kuwapatia wabunge ofisi.

Alichofanya Hapi ni kulikumbusha Bunge kuwa lina wajibu wa kuwajengea wabunge ofisi nzuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles