Na ATHUMANI MOHAMED
MAISHA ya binadamu yanatofautiana sana. Wapo matajiri na masikini, lakini kuna wale wanaoishi maisha ya kati. Wakati familia fulani katika moja ya vijiji kule Liwale mkoani Lindi ikipata muhogo wa kuchemsha na samaki wabichi kama chakula cha mchana, wapo wanaokosa kabisa mlo wa mchana.
Zipo familia zinapata mlo mmoja tu, lakini wengine wakila milo mitatu iliyokamilika. Nimekupa mfano wa familia inayokula muhogo na samaki kama mlo wa mchana, yawezekana familia fulani katika Kitongoji cha Masaki, Kinondoni jijini Dar es Salaam wanapiga mapochopocho.
Nataka kufufundisha nini hapo? Tofauti za maisha kati yetu. Ndiyo maana si ajabu kabisa labda wewe upo katika hali ya chini au kati na hujawahi kuota kumiliki gari, lakini familia fulani yenye watoto sita, wote wana magari yao.
Ni suala la nafasi tu. Lakini je, ni kweli kwamba ukizaliwa kwenye familia masikini, unapaswa kuendelea kuwa masikini siku zote? Je, ni kweli kwa sababu hujasoma, basi maisha yako ni ufukara tu? Ni sahihi kwamba, kwa sababu wazazi wako hawajawahi kumiliki hata baiskeli basi na wewe utakufa ukiwa unanuka ufuraka?
Jibu ni moja tu, siyo kweli. Unaweza kabisa kubadilisha maisha yako. Fahamu kwamba, hao matajiri unaonawaona leo hii, hawakuzaliwa ghafla na kukutana na maisha mazuri, walihangaikia.
Wapo ambao wamezaliwa na kukuta neema ya utajiri kwenye familia zao, lakini siyo wote. Kuna vijana wengi walizaliwa kwenye familia masikini, lakini wakaongeza juhudi na sasa ni matajiri wakubwa.
Wamebadilisha maisha ya wazazi wao na yao pia. Wameweza kuwatoa wazazi wao kwenye aibu na kudharauliwa. Hayo yanawezekana ikiwa utakuwa tayari kufuata kanuni za kifedha na utafanikiwa.
Unaweza kuwa mfanyabiashara mzuri, mfanyakazi unayelipwa mshahara mkubwa na unaishi maisha yasiyo na wasiwasi, lakini jiulize, unayo nidhamu ya fedha? Mirija yako ya fedha ikoje? Ukiweza kudhibiti mirija yako ya fedha sawasawa, basi ni rahisi kabisa kufikia mafanikio.
UNATUMIAJE FEDHA ZAKO?
Ili ufanikiwe inategemea sana na namna unavyotumia fedha zako. Maisha ya kifedha yanafananishwa na kifaa kinachopitimia mafuta ya rejareja madukani.
Chombo kile mara nyingi hupitimia mafuta ya kula au taa, ambacho kwa juu kuwa kibana zaidi na cha duara, wakati pale pa kuingilia mafuta huwa kidogo sana.
Maana yake ni kwamba, kwanza unatakiwa kuhakikisha una vyanzo vingi vya mapato lakini matumizi yako yawe madogo kadiri inavyowezekana. Namna matumuzi yako yanavyozidi kuwa chini, ndivyo akiba yako inavyozidi kuwa kubwa na kukusogeza kwenye mafanikio.
WEWE UNAISHIJE?
Je, utaratibu wako wa maisha ukoje? Unafuata kanuni za mafanikio au unaangalia fulani atakuonaje au atakufikiriaje? Ndugu yangu, usiishi watu wanavyotaka, angalia namna ya kujikomboa kwenye umasikini.
Hili si kwa watu wa chini pekee, hata kama una fedha nyingi kiasi gani, ikiwa matumizi yako yatakuwa hayana tija, basi utakuwa unajisogeza kwenye kuporomoka kimafanikio.
Kata mirija ya matumizi yasiyo na maana. Jifunze kuweka akiba na mara zote shughulisha ubongo wako juu ya namna gani utakuwa bora zaidi kwenye maisha yako.
MCHAWI NI WEWE
Acha kulalamika, mchawi wa mafanikio yako ni wewe mwenyewe. Ukiweza kudhibiti matumizi yako, ukakata mirija yako isiyo na tija, basi utajiri utakuwa rafiki yako.
Badili mtazamo kuhusu maisha, angalia maisha katika jicho pana, huku kiu yako ya kuwa mwenye mafanikio zaidi na zaidi ikiishinda hata ile ya maji ya kunywa!
Kufanikiwa ni haki yako. Kwa leo naishia hapa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine ya kufungua bongo zetu kuhusu mafanikio.