Tatizo la macho laongezeka kwa jamii

0
668

AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

RAIS wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Macho Tanzania (TOS), Dk. Frank Sandi amesema tatizo la afya ya macho linaendelea kuongezeka, huku jamii ikiwa haina uelewa wa kutosha kutokana na kuchukulia ugonjwa huo kama tatizo dogo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Dk. Sandi alisema kila ifikapo Oktoba 10, dunia huadhimisha Siku ya Afya ya Macho ambayo kwa mwaka huu kaulimbiu ni “Afya ya macho kwa wote”.

Dk. Sandi alisema kuwa takwimu za dunia zinaonyesha kuwa takribani watu bilioni 1.3  wanasumbuliwa na matatizo ya macho na hapa nchini makadirio ni milioni 1 na laki 8, sababu kubwa ni afya ya macho kuwa na mgogoro.

“Changamoto nyingine ni watu wengi wanakuja wakiwa wamechelewa, hali hiyo hufanya madhara kuwa makubwa zaidi.

“Hata hivyo, sababu inayoongoza ni mtoto wa jicho kwa asilimia 39, sababu nyingine ni upungufu wa macho kuona kwa asilimia 24.

“Mengine ni kama shinikizo la jicho asilimia 18, magonjwa ya muda mrefu kama kisukari, presha, mafuta mengi, haya yanasababisha madhara kwa asilimia 10. Pia kuna umri kwenda, hasa uzee, hii inachukua asilimia 18,” alisema Dk. Sandi.

Makamu wa Rais wa chama hicho ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka Hospitali ya CCBRT, Dk. Cyprian Ntowoka aliiomba Serikali kuupa kipaumbele ugonjwa huo kwa kutoa elimu kwa jamii.

“Mwaka huu tunawakumbusha Watanzania kuwa tatizo la macho linatibika, kwahiyo kila mtu ajali afya ya macho kwa kupima macho angalau mara moja kwa mwaka.

“Pia naiomba Serikali sasa kulipa kipaumbele suala la afya ya macho kwani takwimu zinaendelea kuongezeka na tunapata wagonjwa wengi, hivyo kampeni ya elimu inahitajika kwa jamii,” alisema Dk. Ntowoka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here