23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

TASAF YASAIDIA WAKAZI MERU  KUUPA UMASKINI KISOGO

Na Mary Mwita, Arumeru


“TASAF imekomboa familia yangu, maisha yalikuwa magumu mno, sikuwa na fedha za kuwanunulia watoto wangu madaftari wala chakula. Maisha yangu yalikuwa magumu sijui hata nieleze vipi ili uweze kunielewa, kwa sasa naishukuru Serikali kupitia TASAF kutusaidia.”

Hiyo ni kauli ya Neema John mkazi wa Akheri Wilaya ya Arumeru, ambaye ananufaika na mpango wa kunusuru kaya masikini wa TASAF.

Neema anasema ameweza kuanzisha mradi wa kuku kupitia fedha anazopewa kila baada ya miezi miwili na TASAF.

“Fedha hizi ni nyingi kwangu kwa kuwa kabla ya kuzipata maisha yangu yalikuwa magumu na hakuna mtu aliyenisaidia. Kwa hiyo najiona kama nimekombolewa kutoka katika shimo kubwa,” anasema.

Kwa upande wake Elinuru Bahati, mkazi wa Kingori  Halmashauri ya Meru, anasema  TASAF imemsaidia kutunza famiilia na kupata uhakika wa  kipato baada ya kumpatia kuku wa kufuga na fedha taslimu.

“Wanawake katika jamii yetu hii wanabebeshwa mzigo mkubwa wa kulea familia, hivyo tulikuwa tumeelemewa, lakini tangu tulipoanza kupokea fedha kutoka TASAF, maisha yamebadilika,” anasema.

Hata hivyo, baadhi yao wanasema kuwa fedha zinazotolewa hazitoshelezi mahitaji hivyo wanaomba waendelee kusaidiwa ili waweze  kuboresha maisha yao zaidi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, Christopher Kazeri anasema mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III katika Halmashauri ya Meru unatekelezwa katika vijiji 47.

Anasema mpango huo unawasilisha fedha kwa kaya maskini 5,570 katika vijiji 47.

Anasema utekelezaji umefanyika katika vijiji 9 ambavyo pia wahusika wamehamasishwa na kuwezeshwa kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopa.

Mkurugenzi huyo anasema walengwa wamewezeshwa kuibua miradi mipya ambayo inasaidiwa na mfuko wa Opec III  katika vijiji 12 vya halmashauri hiyo.

“Fedha hizi zimesaidia sana wahusika ambapo pamoja na mambo mengine wameweza kubadili maisha yao na kupeleka watoto shule, pia wameweza kulipia gharama za matibabu na kujiunga na bima ya afya,” anasema Kazeri.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF, Proches Bureta anasema malipo yametolewa kwa vipindi 12 kuanzia  Julai/Agosti 2015  hadi Mei/Juni 2017.

Anataja jumla ya fedha iliyotolewa ni Sh 2,341,085 ,174. Bureta anasema walengwa wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara ya jinsi ya kutumia fedha hizo na kutunza miradi waliyoanzisha kwa faida yao.

Anasema vijiji tisa vilivyobahatika kupata fedha za TASAF inayotekelezwa na Opec III wananchi wake wanajihusisha na ufugaji wa kuku, ujenzi wa miundombinu ya elimu katika vijiji vya Maruvango na Ngejusosia.

Miradi mingine ni ukarabati wa mfereji na umwagiliaji Kipande Nkoavele, utengenezaji wa makinga maji, sakila na urejeshaji wa vyanzo vya maji Nkoanekoli.

Bureta anafafanua kuwa miradi  hiyo itatumia Sh 382,652,417.45  na kwamba fedha hizo pia zimetumika kujenga bweni katika Shule ya Sekondari Kingori iliyopo Kijiji cha Ngejusosia, kujenga nyumba ya mwalimu katika Shule ya Sekondari Maruvango na ufugaji wa kuku  katika kijiji cha Songoro.

Bureta anasema miradi ya kuku imepewa kwa vikundi 27 vya ujasiriamali na inatekelezwa katika vijiji vinne vyenye jumla ya watu 450 watakaonufaika. Anasema kila mlengwa anapatiwa kuku wanne ambao ni mtetea na jogoo.

“Kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini, walengwa wameweza kuhamasishwa na kuanzisha vikundi vya kuweka akiba na kuwekeza, lengo likiwa ni kuboresha hali zao kiuchumi.

Vikundi 44 vilianzishwa katika vijiji hivyo na halmashauri ilipokea nyaraka kutoka TASAF na masanduku 44 kwa ajili ya kuzitunza,” anasema Bureta.

Anasema kuna idadi kubwa ya watu ambao hawako kwenye mpango huo, hali inayozua malalamiko pindi wanapotoa mgawo kwa watu waliobahatika.

“Kwa kweli kuna changamoto ya idadi kubwa ya watu wenye maisha duni ambao hawajaingia katika mpango huu, tumetuma orodha yao TASAF makao makuu ili waweze kuona uwezekano wa kuwasaidia,” anasema Bureta.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Mkoa wa Arusha  Mathias Methew anasema TASAF Mkoa wa Arusha imeweza kuwafikia walengwa  45,752 na kuwawezesha kuanzisha shughuli ndogo ndogo.

Seif anasema wananchi  kutoka kaya maskini wanaopata fedha kila baada ya miezi miwili kwa kiasi kikubwa wameweza kukombolewa na wengine wameanzisha miradi midogo midogo ya kuwaongezea kipato  na hivyo kuwawezesha kutunza familia zao.

Anasema iwapo kila mhusika atatumia fedha hizo kwa malengo maalumu ni wazi kuwa  wataondokana na umasikini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles