24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TASAF INAVYOZIINUA KAYA MASIKINI ARUSHA

Na MARY MWITA


NI Majira ya saa tano asubuhi nikiwa katika Halmashauri ya Arusha, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, nikishuhudia kundi kubwa la akinamama na wazee wa Kijiji cha Imbibia na Ilkiushin wakiwa na shauku kubwa  ya  kupokea msaada wa mbuzi  kutoka Tasaf. 

Naramatisho Logoliye, ni mama mwenye watoto 9 kutoka Kijiji cha Imbibia, Kata ya Mwandet katika Halmashauri ya Arusha. Anaonyesha uso wa furaha na kueleza kuwa tabasamu lake linatokana na maisha yenye matumaini baada ya kutambuliwa na mradi wa Tasaf na kuanza kupewa fedha kila baada ya miezi miwili  na kudai kuwa Tasaf imeokoa maisha yake na watoto wake.

Logoile anasema kuwa alikuwa amekata tamaa ya maisha kutokana na maisha duni aliyokuwa nayo kabla ya kupata msaada huo, lakini sasa amekombolewa  na kuwa mbuzi aliopewa kupitia mradi wa OPEC ( The Organization of the Petroleum Exporting Countries ),  atawatunza  na kwamba ana imani kuwa ataboresha maisha yake zaidi.

“Kweli maisha yangu yalikuwa magumu sana, siwezi hata kusema kwa kuwa watoto wangu wakati mwingine walilala na njaa na walishindwa kwenda shule lakini hizi fedha tunazopewa  na Tasaf zimeniokoa na watoto wangu Mungu aubariki mradi huu,” anasema Logoile.

Nagala Mollel, Mwenyekiti wa Kikundi cha Galilaya Kijiji cha Imbia, anasema mradi huo umewaondolewa hali duni ya maisha na kuwezesha kulipia watoto wao ada za shule na kudai kuwa kabla ya kupata msaada huo, watoto walikosa ada za shule na kulazimika kukaa nyumbani hadi watafute fedha kwa zaidi ya miezi miwili ndiyo watoto warudi shule.

“Niseme kuwa Tasaf imekomboa kizazi chetu, hususani sisi tunaotokea katika jamii hii ya Wamasai, tunabebeshwa mzigo mkubwa wa kulea watoto na hivyo tulielemewa sana, hivyo tulikuwa tumelewa sana, lakini tangu kuanza kupokea fedha kutoka Tasaf, maisha yamebadilika natumia fedha hizo kufanya biashara ndogo ndogo na kuongeza kipato ambacho kinaniwezesha kupata mahitaji ya familia,” anasema.

Mwanakamati wa miradi ya Tasaf  katika Kijiji cha Ilkiuish, Jonath Solomon, anasema watahakikisha kuwa wanafuatilia miradi hiyo na kwamba wameshawasimamia na kuweza kujenga  mabanda mazuri kwa ajili wa mbuzi hao na kuongeza kuwa wanatarajia kuwa mradi huo utainua hali za maisha ya watu katika Kijiji cha Ilkwishin.

Pamoja na mambo mengine, anasema msaada unaotolewa kwa walengwa wa kaya masikini hautoshelezi na kuomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza fedha kila baada ya miezi miwili na kuongeza idadi ya mbuzi ili nia njema ya kuwapunguzia umasikini iweze kufikiwa.

“Tunashukuru kwa msaada huu, lakini tunaomba Serikali iongoze msaada maana ni watu wengi ambao hawajafikiwa na wengine wanaopata haitoshi, lakini angalau si kama hapo awali ambapo walikuwa hawana chochote,” anasema Solomon.

Baada ya kusikiliza simulizi hizo, nilikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha, Wilson Mahera, akikabidhi mbuzi kwa kaya masikini katika Kijiji cha Imbibia na kutoa ufafanuzi wa msaada huo. Alisema mbuzi hao ni mradi uliobuniwa na wananchi wa Kijiji cha Imbibia na unafadhiliwa na nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi na unajulikana kama OPEC.

Mahera anasema lengo kubwa la mradi huu ni kuinua hali ya kipato kwa walengwa na kuboresha huduma za elimu na afya pamoja na mazingira na kuongeza uzalishaji.

“Sisi tuna bahati sana, Mradi wa OPEC unatekelezwa katika mikoa miwili nchini ambayo ni Arusha na Njombe na wilaya yetu iko katika Mkoa wa Arusha, hii ni bahati nawasihi ndugu wananchi mkatunze miradi hiyo ili iweze kuwaondolea umasikini na kukamilisha malengo ya wafadhili wa mradi huu,” anasema.

Hata hivyo, anasema jumla ya vijiji 45 vya Halmashauri ya Arusha vinanufaika na mradi wa Tasaf na vijiji tisa  vimebahatika kuchaguliwa kutekeleza miradi inayotokana na fedha za ufadhili wa OPEC.

Jabir Ally ni Mratibu wa Tasaf katika Halmashauri ya Arusha na anasema miradi inayofadhiliwa na OPEC ni miradi ya elimu, afya, ujenzi wa miundombinu kama vile zahanati na umwagiliaji.

Miradi mingine ni ajira za muda mfano kuboresha mazingira, kupanda miti, kuboresha mazingira, kupanda miti, kuboresha na kulinda vyanzo vya maji, miradi ya ujasiriamali na maji  kuongeza kipato mfano ufugaji wa kuku, mbuzi na nyuki.

Ally anataja vijiji tisa vilivyonufaika kuwa ni Themi ya Simba ambayo ina mradi wa vyumba viwili vya madarasa na choo cha matundu 6 yenye thamani ya Sh  72,091,456.82, mradi wa ujenzi wa nyumba ya watumishi Laroi yenye thamani ya Sh 71,091,459.82,

mradi wa hifadhi ya mazingira Lemugur  wenye  thamani ya Sh 67,965,940.66, mradi wa hifadhi ya udongo na mazingira Kiseriani  wenye thamani ya Sh 74,708,500, mradi wa ufugaji wa kuku chotora  kijiji cha Engorora Sh 21,587,607.05, mradi wa mbuzi wa maziwa Kijji cha Imbibia wenye thamani ya Sh 20,409,470.89.

Mradi wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa  Kijiji cha  Losikito  wenye thamani ya Sh 20,409,470.89, mradi wa ufugaji wa mbuzi wa maziwa Kijiji cha  Ikiushi wenye thamani ya Sh million  20,409,470.89.

Kwa upande wake Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Arusha, Mathias Sief, anasema Tasaf Mkoa wa Arusha imeweza kuwafikia walengwa  45,752 na kuwawezesha kuanzisha shughuli ndogo ndogo na hivyo kupata kipato.

Seif anasema wananchi  kutoka kaya masikini wanaopata fedha kila baada ya miezi miwili, kwa kiasi kikubwa wameweza kukombolewa na wengine wameweza kuanzisha miradi midogo midogo ya kuwaongezea kipato  na hivyo kuwawezesha kutunza familia zao.

Pamoja na mambo mengine, anasema Mkoa wa Arusha umebahatika kuingia katika mradi wa OPEC na kuwa jumla ya miradi 63 inayotarajiwa kutekelezwa  kupitia fedha hizo  na kwamba kila halmashauri inatakiwa kuwa na miradi 9  kulingana na jinsi wananchi walivyoibua.

Seif anataja baadhi ya  miradi hiyo kuwa ni miradi ya elimu, afya, ujenzi wa miundombinu kama vile zahanati, ujenzi wa vyoo na ujenzi wa nyumba za walimu.

Hata hivyo, anasema pamoja na kutekeleza miradi hiyo, baadhi ya changamoto walizokutana nazo ni baadhi ya wasimamizi miradi kupoteza uaminifu na kushawishika kutumia fedha za walengwa kinyume na taratibu na kudai kuwa wahusika wamechukuliwa hatua za kisheria.

Seif aliwataka wanufaika wa miradi ya Tasaf kutoka kaya masikini kutumia msaada huo kwa kubadilisha hali za maisha yao ili utakapofikia ukomo, waweze kuwa wamejikomboa kutoka katika hali duni ya maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles