26.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tarura kuendelea kufungua nchi kuwawezesha wakulima kuyafikia masoko kirahisi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital Dodoma

Katika kuhakikisha wakulima wanayafikia masoko kwa haraka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) umesema unaendelea na ujenzi wa barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutumia teknolojia mbadala zenye gharama nafuu.

Wakala huo umekasimiwa kusimamia kilomita 144,429.77 ambapo kazi kubwa inayofanywa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo.

Akizungumza Agosti 4,2024 kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dodoma, Mratibu wa Madaraja na Barabara za Mawe kutoka Tarura, Mhandisi Mshauri, Phares Ngeleja, amesema wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali ambazo zimewezesha ujenzi wa madaraja na barabara.

Mratibu wa Madaraja na Barabara za Mawe kutoka Tarura, Mhandisi Mshauri, Phares Ngeleja, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma.

“Tunawawezesha wananchi vijijini kufika sehemu ambazo hazifikiki, tunawawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kutoka vijijini mpaka maeneo ya masoko na kwenye maghala, katika jitihada za kupunguza gharama tumekuwa tukijenga madaraja ya bei nafuu,” amesema Mhandisi Ngeleja.

Amesema tangu wakala huo ulipoanzishwa mwaka 2017 wamejenga madaraja 275 nchi nzima yaliyogharimu Sh bilioni 10 huku Mkoa wa Kigoma ukiwa unaongoza na kwamba kama wangejenga kwa kutumia zege na nondo wangetumia zaidi ya Sh bilioni 50.

Aidha amesema ili kuwafikia wananchi kwa haraka wanajenga barabara kwa kutumia mawe ambapo katika Mkoa wa Mwanza wamejenga kilomita 20 za mawe, Kigoma (kilomita 3.34), Rukwa (mita 350), Morogoro (mita 310).

“Licha ya kutumia mawe pia tunatumia teknolojia zingine, mfano katika Mkoa wa Dodoma tuna barabara ya daraja dogo kilomita moja, Chamwino tuna zaidi ya kilomita saba, Iringa tuna zaidi ya kilomita sita pamoja na Mkoa wa Simiyu. Tutatumia teknolojia hizi kufungua barabara nyingi zaidi tuwawezeshe wakulima wafike maeneo yasiyofikika na kuyafikia masoko kirahisi,” amesema.

Kaimu Meneja wa Tarura Jiji la Dodoma, Mhandisi Kasongo Morijo, amesema wanahudumia kilomita 1,189 za barabara na kati ya hizo 224 ni za changarawe, 715 za udongo na 248 za lami.

Amesema wana miradi ya matengenezo na miradi mikubwa ya lami ambayo inalenga kuhakikisha maeneo yanafikika kuwezesha upatikanaji huduma za kijamii na kutolea mfano ujenzi wa Barabara ya Kisima cha Nyoka – Nkuhungu kuhakikisha wananchi wanafika mjini bila kikwazo.

“Tunataka kuhakikisha mpaka mwaka 2025 maeneo mengi ya Jiji la Dodoma yawe na lami na yaweze kupitika kwa wakati,” amesema Mhandisi Morijo.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Tarura, Catherine Sungura, amesema wanatumia maonesho hayo kuelimisha umma namna wanavyojenga miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji.

“Kazi kubwa imefanyika nchini, vijijini tumefanya kazi kubwa ya kufungua barabara ambazo zimewasaidia wananchi kuinuka kiuchumi na kupata maendeleo. Barabara ambazo tunajenga zimewasaidia wananchi mfano wajawazito walikuwa wanapata shida kufika kwenye huduma za afya lakini hivi sasa wanapata huduma bila changamoto, watoto wanakwenda shule na wakulima wanasafirisha mazao yao,” amesema Sungura.

Aidha amesema wana miradi katika mashamba ya Chai Kilolo mkoani Iringa na Tukuyu mkoani Mbeya ambako kuna barabara za lami zinazowarahisishia wakulima kusafirisha chai na kwenda kiwandani.

“Kufunguliwa kwa barabara hizi kumewezesha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na wa eneo husika kubadilika na tunaingiza kipato kwa serikali, tunajivunia kazi kubwa ambayo tumeifanya. Bado tuna vipaumbele vya kuhakikisha tunafika kusikofikika…tunawakaribisha wananchi wafike katika banda letu waone kazi kubwa inayofanywa na Tarura,” amesema Sungura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles