Na Alhaj Abdallah Tambaza
ILIKUWA siku ya Jumanne, Mei 24, mwaka huu, baada ya Magharibi kupita, nikiwa ndani ya Pantoni ya MV Magogoni nikielekea nyumbani Tuwangoma, simu yangu ya kiganjani ikalia. Kutokana na kelele na muungurumo wa injini wa kivuko kile, sikupenda hata kidogo kuijibu nikichelea kwamba nisingesikilizana na mtu wa upande wa pili. Lakini kwa taabu niliipokea:
“…Mzee wetu Kitwana Kondo amefariki jioni ya leo hospitalini Hindu Mandal maziko kesho, tupashane habari,” alisema ndugu yangu Mwinyi Mussa kutoka upande wa pili.
Nilijizoazoa kuelekea nyumbani nikiwa nimehuzunika kupita kiasi, kwani vifo vya ukubwa huu vilikuwa vimeongozana hapa kwetu Dar es Salaam katika mwezi mmoja. Alianza Mzee Issa Ausi kama wiki tatu tu zilizopita, akafuata mzee mwengine, Ali Mbaraka ‘Bobo’ na sasa tena Mzee KK- Inna Lillahi Waina Ilayhi rajuun!
Marehemu mzee KK alizikwa katika makaburi ya Tambaza siku ya Jumatano, Mei 25, mwaka huu baada ya sala ya alasiri. Miongoni mwa watu mashuhuri waliokuwapo mazikoni pale ni ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambaye ni Rais (mstaafu )wa Serikali ya Awamu ya Pili; Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais (mstaafu), Edward Lowassa, mmoja wa viongozi katika Ukawa na Waziri Mkuu mstaafu; na Prof. lbrahim Lipumba wa CUF.
Wengine ni Mzee Ngombale Mwiru, Abdulrahman Kinana, Prof. Hamza Njozi, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) pamoja na masheikh mbalimbali wa hapa jijini akiwamo Mufti Zubeir.
Tanzia ndefu na timilivu, kumhusu mzee huyu, ambaye wengine ni baba yetu, tayari imeshaandikwa na ndugu yangu kutoka Kuala Lumpur Malaysia, Balozi Ramadhani Kitwana Dau. Ndani ya tanzia ile hakikubaki kisichoelezwa hadi kufanya mtu mwingine naye achukue kalamu na kuandika, bila shaka yeyote hiyo itakuwa ni fujo! Lakini hali halisi ni kwamba, kila watu wanapotokeza kwa wingi kumuenzi Marehemu Mzee huyu ndivyo ambavyo tutakuwa tumemuenzi na kumlipa fadhila alizotukirimu.
Jina lake kamili ni Kitwana Selemani Kondo au KK kama alivyofahamika zaidi kwa upendo kutoka kwa marafiki zake. Jina hili lilivuma sana nchini kwetu hata kwa watu ambao hawakupata kumwona wala kukutana naye. Jina la KK limekuwa mithili ya ngoma ya mbali ambayo huvuma kwa mdundo mzuri ikiwa haina uhalisia.
Kwa sababu hiyo basi, watu wengi hapa kwetu walimjengea taswira, kwa sababu ya kutomjua vzuri, kwamba ni mtu pengine anayebwabwaja maneno tu kama Mswahili mwingine na kibahati bahati akawa Mbunge, Meya na Diwani.
Ndugu msomaji, mimi najisikia fahari pamoja na majonzi niliyokuwa nayo ya kuondokewa na Mzee KK, kwa sababu mimi ni sehemu ya historia ya Dar es Salaam. Jina langu ni Abdallah Mohammed Saleh Tambaza. Familia yetu iko karibu kabisa na historia ya Jiji la Dar es Salaam. Ikutoshe kwamba, ukisoma historia ya TANU na Uhuru wa Tanganyika, unamuona Jumbe Tambaza pale Upanga, Msikiti wa Tambaza, Makaburi ya Tambaza, Shule ya Tambaza na Hospitali ya Muhimbili ambayo Mzee Tambaza alitoa uwanja wake bure ijengwe kusaidia jamii kabla ya Uhuru.
Kwenye maeneo mengine ya jiji hili, kama vile Magomeni, alikuwapo Diwani Mwinyimkuu Mshindo na Diwani Ndugumbi Kitembe. Wote hao ni kina Tambaza. Mzee KK alizaliwa kijijini kwao Mtoni Kijichi maeneo ya Mbagala. Huko nako ni sehemu ya Diwani Tambaza Mwenye—kuuchimba.
Hivyo Mzee KK, pamoja na kwamba ni Mzaramo wa kutoka Mtoni Kijichi, Mbagala, hakukosea kitu kuamua azikiwe katika makaburi ya Upanga kwa Tambaza kwa sababu ana asili nako kinasaba, aliishi wakati wote na kusomea jijini Dar es Salaam.
Kwa mnasaba huo basi, mambo matatu aliyapenda sana: moja ni Utaifa usiotenganishwa kwa maana ya Dar es Salaam na Tanzania ni kitu kimoja; aliipenda Dar es Salaam yake kama alivyoipenda Tanzania kutoka Lindi hadi Mara; Tanga hadi Rukwa; Dar es Salaam hadi Mwanza, Kigoma na Mbeya, kwa maana ya Tanzania nzima, akipendelea zaidi utani wa makabila mbalimbali hasa kwa Wanyamwezi, Wasukuma na Wadigo.
Nimemjua Almarhum Mzee KK katika sura kama tano hivi:
Kwanza, Mzee Kitwana alisoma pale Shule ya Kitchwele Dar es Salaam wakati wa ukoloni pamoja na baba yangu mkubwa Mzee Yahya Saleh Tambaza na nduguye (babangu mzazi) pamoja na marafiki wengine wa baba zangu, wakiwamo akina Sykes, akina Aziz, Iddi Simba, Said Kassim, Zuberi Mtemvu, Heri Kilanga na Harold Mgone—kwa kuwataja wachache— ambao pia alicheza nao mpira wa chandimu utotoni na katika timu za Yanga na Sunderland (Simba).
Kila mara nilipokuwa nikimwona Mzee KK akiwa na baba zangu hao ilikuwa ni masikhara, vicheko na mambo ya namna hiyo ikiwamo utani wa Simba na Yanga.
Baba yangu mimi Mzee Mohammed Saleh Tambaza, ni Mwasisi wa Sunderland na Mzee KK yeye ni mwasisi wa timu ya Yanga huko mwanzoni, akiwa na kina Mzee Mangara, Kondo Kipwata, Saidia Msafiri, Mtaruke Mangara, Juma Shamte na Juma Vijiga Mohammed Mabost na wengineo wengi.
Kila palipokuwa na shughuli ya aina yoyote nyumbani kwetu, iwe arusi au misiba, daima nikimwona Mzee KK yuko jamvini akiupiga mpunga sawasawa huku akiwarushia rafiki zake, kwa upendo, maneno ya utani na ngonjera.
Pili, historia inasema kwamba miaka mingi nyuma wakati wa utawala wa Kiingereza hapa kwetu, Mzee KK akiwa na kundi la vijana wengine wanane waliofaulu vizuri masomo ya sayansi, alichaguliwa kujiunga na Chuo cha Mpwapwa Livestock Research Center (LRC) ili waje kuwa Veterinary Assistants wa kwanza hapa Tanganyika.
Sijui ilikuwaje hadi baadaye akaja kuwa katika Jeshi la Polisi na kuwa mwenye cheo cha Inspekta wakati nchi ikiwa mikononi mwa wazungu. Pamoja na kwamba hawakuwapo Waafrika wengi kwenye ngazi hiyo ya upolisi, lakini wale walioupata Uinspekta hawakuwa watu wa kawaida hivi.
Katika miaka ya 1950 wakati wa harakati za kupigania uhuru wetu, habari zinasema KK aliitumia nafasi hiyo ya upolisi kuwapa akina Nyerere na wenzake habari nyeti za Serikali ambazo zilikuwa zikipangwa dhidi ya mapambano ya Uhuru. Mingi ya mikutano hiyo kati ya KK na viongozi wa TANU wakati huo ilikuwa ikifanyika katika majumba ya watu Kariakoo na wakati mwingine pale kwenye klabu ya Yanga Mtaa wa Mafia na Sukuma, huku Mwalimu Nyerere akiwa kajibadilisha kwa kujifunika baibui ili kupoteza maboya asitambulikane.
Msomaji, unaweza kuona namna gani Marehemu KK alivyohatarisha maisha yake kwa ajili ya Taifa hili, maana kama wakoloni wangejua, si kama angepoteza kazi peke yake, lakini pengine angeuawa! Yeye aliona potelea mbali na iwe hivyo, akaendelea kuifanyia TANU kazi, tena na tena na tena mpaka leo kimeeleweka tuko huru.
Mzee KK, kutokana na umaridadi na utanashati wa kipolisi, alikuwa akijua kuvaa vizuri sana. Katika maisha yangu ya utoto nilikuwa nikimwona akirandaranda kwenye mitaa ya kwetu Kariakoo kwa madaha sana na miondoko ya maringo ya kiaskari huku akiwa amepangilia kama ni suti, suti kweli; kama suruali na shati basi ni vya hatari tupu! Huku kiatu chake cha ‘bei mbaya’ kikiwa ng’aring’ari mguuni.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa vijana wa zamani.
Na hapa nawakumbuka wazee wengine wa namna hiyo akiwamo Mzee Senga Mlela wa pale Mtaa wa Chura, Kariakoo; Marehemu Mzee Jagna Shaha na Maalim Abubakar Mzinga wa Mzinga&Sons Muslim School. Hawa wote wakati wa enzi zao walikuwa wakivaa ‘pamba kali’ kutoka maduka ya B. Choitram, Jan Mohammed, J.R. Steven’s, Teekay na Afi yote yakiwa pale Accacia Avenue (sasa Samora).
Miaka kadhaa baadaye, sasa nikiwa mwanafunzi wa sekondari katika Shule ya Mtakatifu Joseph, pale Forodhani, nilishangazwa kila nikimwona kwenye mitaa yule mzee ambaye namjua kama ‘rafiki yake babangu aliyekuwa Inspekta wa Polisi na baadaye kwenda mpaka Scotland Yard, akiwa katika magari mazuri mazuri ya kifahari kule mjini Dar es Salaam, wakati huo kukiitwa Uzunguni.
Kumbe nilikuwa sikufahamu umuhimu wake. Yule mzee alikuwa ameshika wadhifa wa Serikali ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sikujua ana mchango mkubwa sana katika kufanikisha Muungano na harakati za vyama vya ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, yakiwamo Mapinduzi ya Zanzibar. KK alikuwa rafiki mkubwa wa Karume na Kassim Hanga.
Ah! Pia, sikuwa nimejua KK yule ‘rafiki yake baba’, ndiye kwa namna ya kipekee kabisa alifanikisha kuzibadili siku za Sikukuu ya Pasaka wakati huo zikijulikana kama, “Bank Holidays” na kupatikana msimu wa ‘Sports,’ baina ya vilabu vya Dar es Salaam na Zanzibar kutembeleana kimichezo.
KK, alikuwa kiongozi mwandamizi wa Yanga aliyeasisi udugu baina ya klabu yake na ile ya African Sports ya Karume kule Unguja. Simba wao walikuwa na uhusiano na klabu ya Kikwajuni pia ya huko huko Unguja. Udugu huu, ulioendelezwa miaka nenda, miaka rudi; haukuishia mpirani tu bali baadaye ukahamia kwenye siasa na hivyo kuja kuunganisha nchi na kuzaliwa nchi ya Tanzania baada ya Sultani kupinduliwa kule Zanzibar.
Habari zinasema, ilikuwa ni kutokana na urafiki mkubwa baina ya KK na Karume wa Unguja na kwa ushawishi mzito wa KK, Marehemu mzee Karume akaizawadia klabu ya Yanga jengo la makao makuu yaliyopo mitaa ya Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam.
Aidha, habari zinasema, ilikuwa ni KK pia aliyemuunganisha aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Sunderland (sasa Simba) Mzee Ramadhan Kirundu na Hayati Mzee Karume ambaye alikuja kuwamalizia Simba sehemu ya jengo lao iliyokuwa haijakamilika. Mambo kama hayo ndiyo yalikuwa yakifanyika katika vilabu vya Simba na Yanga kwa wakati wa zamani. Ni kusaidiana, kuhurumiana, kutembeleana na kuzikana wakati wa misiba.
Watu waliopo sasa katika vilabu hivi kamwe hawawezi kuyafanya haya waliyoyafanya watangulizi wao, ni chuki, hasama na uadui tu vilivyotamalaki.
Zaidi ya mpira, Marehemu Mzee KK alipenda burudani za aina mbalimbali ikiwamo muziki wa dansi na ule wa taarab asilia. Aliipenda bendi ya Dar es Salaam Jazz wakijulikana kwa jina la, ‘’Majini wa Bahari,’’ ya wakati huo ikiongozwa na Mzee Mubba wa Gerezani; Kilwa Jazz ya Ahmed Kipande; Ulanga Jazz na Western Jazz iliyoongozwa na Yanga mwenziwe Marehemu Daudi Makwaia.
Nyengine ni ile ya Merry Black Birds ikiongozwa na rafiki yake Ally Sykes, waliokuwa wakitumbuiza kwa nyimbo na mitindo ya kizungu ya Rumba, Chacha, Foxtrot na Bolero kila Jumamosi pale ukumbi wa Arnautoglo.
Kwa upande wa taarab asilia, mzee KK alikuwa mpenzi mkubwa wa bendi ya Egyptian Musical Club ya Kariakoo. Bendi hii ilikuwa na uhusiano wa karibu na klabu yake ya Yanga. Kwa mtu wa namna yake kwa wakati ule ni lazima angevutiwa na taarab tu; maana muziki ule, ulikuwa ni sehemu ya utamaduni wa watu wa Dar es Salaam na pwani yake kutokana na maudhui, mashairi na lugha ya Kiswahili.
Vitu ambavyo almarhum Mzee Kitwana alivipenda sana. Daima nikipenda kumsikiliza akizungumza Kiswahili chake fasaha kama ambavyo leo watu wa Amerika walivyokuwa wakipenda kumsikiliza Obama akizungumza Kingereza.
Kiswahili cha Mzee Kondo hukipati Unguja wala Tanga na hata Mombasa. Ni Kiswahili cha Mrima kile na wenyewe ni watu wa Mrima. Kwa sasa ukipata bahati msikilize Mzee Iddi Simba au Suleiman Hegga utaamini ninachokizungumza. Misaada na michango ya Marehemu Mzee wetu huyu kwa jamii katu haiwezi kupimika kwa mizani ya kilo, yadi, futi au mita kwa marefu na mapana; wala si kwa lita kwa ujazo wa ndoo za maji. Ni mkubwa sana. Haupimiki!
Jiji la Dar es Salaam lilipozidi kukua baada ya Uhuru kupatikana, KK alifanya bidii kwa kushirikiana na Marehemu rafiki yake mpenzi Mzee Kibiriti wakaanzisha kwa fedha za KK, klabu mpya ya taarab waliyoipa jina la New Extra Musical Band.
New Extra iliongozwa na magwiji wa taarab wakati huo kama Maalim Abubakar Mzinga na mwanawe Hamis Mzinga; Bi. Pili na dadake Kibibi binti Abdallah.
Nakumbuka kama vile ni jana, uzinduzi wa bendi hii ulifanywa na aliyekuwa rafiki mkubwa wa KK wakati huo, hayati Abdallah Kassim Hanga aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Masuala ya Muungano. Bendi hiyo iliyojizolea umaarufu wakati huo, ilivuma sana kwa nyimbo zake za, ‘’Shambani Mazao Bora Shambani,’’ na ule wa kuhamasisha kujiunga na TANU, ‘‘Kina mama TANU, kina baba TANU, Afro yajenga nchi.’’ New Extra haipo tena. Imekufa kama zile zilizoitangulia za Alwatan, Egyptian na Jamhuri.
Katika kipindi alichofanya siasa, Mzee Kitwana Seleman Kondo alikuwa Mbunge miongoni mwa wabunge wa mwanzo mwanzo baada ya nchi hii kujitawala akipata nafasi, kwa nyakati tofauti kuwakilisha sehemu mbalimbali za majimbo ya Dar es Salaam, ikiwamo Ilala, Kigamboni, Temeke na Dar es Salaam Magharibi. Kutokana na uwakilishi wake uliotukuka uliomfanya awe anarudi bungeni kila mara, wabunge wenzake wa Bunge la Tanzania chini ya Spika Chifu Adam Sapi Mkwawa, hawakusita, kwenye miaka ya 70, kumpa ridhaa ya kuiwakilisha nchi nzima kwenye Bunge la Afrika Mashariki (East African Legislative Assembly).
Wawakilishi wengine wa Tanzania aliokuwa nao siku zile kule EALA walikuwa ni akina Bhoke Munanka, Joseph Nyerere, Edwin Mtei akiwa Katibu Mkuu East African Community, na mawaziri wakiwa ni Alnoor Kassum, John Malecela, Salim Rashid kutoka Zanzibar na Spika alikuwa Chief Sarwart wa Mbulu.
Bunge lile lilikuwa motomoto sana likipendeza kweli kulifuatilia majadiliano yake. Katika kipindi hicho miaka ya 70, nilikuwa mfanyakazi pale Idara ya Usalama wa Anga Afrika Mashariki (Directorate of Civil Aviation E.A) nikiwa Aeronautical Communications Officer pale Nairobi. Pale habari za Bunge lile zilizomhusu Mzee KK zilipoandikwa na magazeti ya Nation na Standard ya Kenya, haraka haraka niliwageukia wenzangu ofisini kuwaonyesha kwamba yule mzee ni baba yangu kutoka kwetu TZ. Kwa kweli nilijivunia sana.
Nakumbuka sana wakati ule kila ajapo Nairobi kwa vikao vya EALA, nilikuwa nikimtembelea hotelini kila jioni na humkuta akiwa amevaa seruni yake na fulana nyepesi; basi tulikaa kwenye balcony na kupiga stori hasa akinipa salam hizi na zile kutoka kwa baba zangu, hasa Mzee Yahya aliyekuwa mbunge mwenziwe wa Dar es Salaam (mashariki wakati huo):
“…salam zako nyingi kutoka kwa babako wewe… ameniagiza umnunulie…(anakitaja alichoagizwa).” Alisema mzee KK kwa upole huku tukinywa chai yetu ya saa na keki. Kenya ni nchi ya ‘mabazungu’ ile hivyo saa hiyo lazima watu wastue kwa chai ama kahawa— tena ya maziwa na siyo ya mkandaa!
Sura ya mwisho ya Mzee Kitwana Kondo niliiona kwenye miaka ya 1990s wakati niliporejea kutoka masomoni Marekani baada ya muda mrefu.Nilimkuta Alhaj Mzee Kondo akihimiza elimu kwa Waislamu; utaifa na mshikamano wa watu wa Dar es Salaam pamoja na nchi yote hii aliyoipenda na kuitumikia sana.
Akiwa Meya wa jiji, si tu kwamba alirudisha heshima ya cheo na ofisi ya meya (anatajwa kwamba ndiye aliyerudisha tena meya kuitwa Mstahiki Meya, kama wanavyotambulika kimila na kidesturi mameya wote wa Nchi za Jumuiya ya Madola (Commonwealth) aliwakumbuka na kuwaenzi wapigania uhuru wenziwe wa Dar es Salaam kwa kuwapa majina ya mitaa. Uliokuwa ukiitwa Somali Street, ulikwenda kwa Mzee Omari Londo; Aggrey Street aliupa jina la Max Mbwana; Kipata Street aliuita Kliest Abdallah Sykes; Tandamti ukawa Mshume Kiyate na Kongo ukawa Iddi Tulio.
Alikuwa ni mzee KK aliyeurudishia jina tena Mtaa wa Bibi Titi Mohammed baada ya kufutwa alipokosana na Mwalimu Nyerere na mtaa huo ukawa Mtaa wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT). Kondo hakupenda hilo!
Mwisho…..
Moja ya kazi kubwa ya kupigiwa mfano ya mzee huyu ni pale alipohangaika huku na huku kuhakikisha kwamba Waislamu wanapunguza pengo la elimu miongoni mwao kwa kuhakikisha wanapata majengo yaliyokuwa ya TANESCO Morogoro kuanzisha Chuo Kikuu akiwa Mwenyekiti wa Bodi. Haikuwa kazi rahisi kwa maana viongozi wengi waandamizi serikalini wakati huo, akiwamo Waziri Mkuu Sumaye, walilipinga wazo hilo kwa nguvu kubwa.
Marehemu KK hakukata tama; alitumia turufu kubwa na hatimaye majengo yale yakapatikana na leo Alhamdullilah chuo kinatoa wasomi si haba. Kwa hili sina shaka yeyote inaweza kuwa ni sababu ya kuingia peponi kwa mzee huyu. Mungu ameshaahidi hilo kwa wale wanaofanya mambo ya namna hii duniani.
Mzee KK aliugua kwa muda mrefu akiwa anapumzika zaidi nyumbani kwake. Miaka michache nyuma kabla kifo chake, kama wadhamini wakuu wa Masjid Mwinyikheri Akida wa Kisutu, Dar es Salaam, tulipokea taarifa mimi na ndugu yangu Mzee Mwinyikhamis Mussa kwamba mzee Kitwana Kondo alikuwa anataka kutuona nyumbani kwake kwa jambo la haraka sana. Ndiyo ikawa mara yangu ya mwisho kumwona akitembea na kuzungumza kwa shida kwelikweli.
Alitukaribisha na kusema hivi, “…nimepata taarifa kwamba mmepokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa TAPA – Taifa, Abdallah Bulembo ya kusema kwamba haraka sana mvunje msikiti katika muda wa wiki 3 kabla hatua kali hazijachukuliwa kupisha ujenzi wa Makao Makuu ya Tapa na kwamba nyinyi ni wavamizi wa kiwanja kile,
Mzee aliendelea, “… sasa nyinyi mamwinyi msisumbuke na hilo …kiwanja nilikitoa mimi na mimi ndiyo nitakayejibu upuuzi huu. Nilipewa kibali na Nyerere kutoa eneo hilo kwa msikiti na hivyo wakati bado nikiwa hai niachieni mimi nijibu hili, nyinyi mamwinyi pumzikeni tu … nitawaletea nakala yenu…” alimaliza mzee kwa sauti ya chini kabisa.
Huyo ndiyo Mzee KK alivyolishughulikia suala hilo pale Abdallah Bulembo, ulevi wa cheo cha CCM ulivyomzidi akasahau kuwa msikiti ni nyumba ya Allah yeye anataka auvunje ajenge ofisi yake ya TAPA—Inna Lillah Waina Ilayhi Rajuun.
Sasa KK hatunaye najua TAPA watatafuta namna ya kuja tena kutusumbua. Msikiti ule unaojulikana kama Mwinyikheri Akida ndiyo wa kwanza kujengwa jijini zaidi ya miaka 150 imepita. Una umri mrefu kuliko hata nchi yenyewe ya Tanzania.
Kwa kumalizia, ni kwamba hadi anafikwa na umauti, umaarufu wa mzee KK kwa masheikh, viongozi wa Serikali ya Tanzania, na viongozi wa SMZ, wakazi wa jiji na hasa viongozi wa Simba na Yanga, ulikuwa mkubwa sana kama ilivyoonyesha kwenye maziko yake.
Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Alhaj Dk Ramadhani Dau, katika taazia yake ndefu kwa mzee wake huyu alipendekeza kwa uongozi wa MUM utafute jengo moja lipewe jina la KK ili kumuenzi marhum. Mimi niliwasikia waombolezaji pale makaburini wakiteta kwamba ni vyema basi moja ya barabara za jiji hili—hata ndogo — iitwe Kitwana Selemani Kondo. Nawaunga mkono sana!
Mwisho, tunamwomba Allah (sw) aipokee roho ya Mzee Kitwana Kondo kwa wema na aipumzishe bila shaka katika pepo ya Firdaus — In shaa Allah.
Amin.