GLORY MLAY-DAR ES SALAAM
TIMU ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake walio na umri chini ya miaka 20 (Tanzanite), imeibuka mabingwa wa michuano ya Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Kusini mwa Afrika( Cosafa), baada jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zambia, katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Wolfson Port Elizabeth, Afrika Kusini.
Mabao ya Tanzanite yalifungwa na Opa Clement dakika ya 24 na Protosha Mbunda dakika ya 87, huku bao pekee la Zambia likipachiwa wavuni na Loveness Nalunga dakika ya 58.
Tanzanite ilikuwa timu mwalikwa katika michuano hiyo ilianza kutimua vumbi Agosti 1 na kufika tamati jana.
Hadi inatwaa ubingwa, Tanzanite inayofundishwa na Kocha Mkuu, Bakari Shime na msaidizi wake, Edna Lema ilipoteza mchezo mmoja pekee dhidi ya Zambia, katika hatua ya makundi, ambapo ilichapwa mabao 2-1.
Hiyo ina maana kwamba, mbali ya kubeba taji hiyo, ushindi wa jana kwa kikosi hicho ulikuwa wa kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa awali dhidi ya Zambia.
Safari ya Tanzaniate ilianza kwa kuumana na Botswana, ambapo Tanzanite ilishinda mabao 2-0, ikaifumua Eswatini mabao 8-0, kabla ya kupoteza kwa mabao kwa Zambia.
Matokeo hayo yaliiwezesha kutinga nusu fainali , baada ya kukusanya pointi sita na mabao 10.
Nusu fainali ilikutana na wenyeji Afrika Kusini na kuitungua mabao 2-0, ushindi ulioipeleka fainali.
Kwa upande mwingine, Zambia ilitinga fainali, baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Zimbabwe.
Katika michezo hiyo, mchezaji wa Tanzanite Aisha Kasim alifanikiwa kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja ‘Hat-trick’, huku beki wa timu hiyo, Enekia Kasonga akitwaa tuzo ya mchezaji bora.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Shime alisema alikiamini kikosi hicho tangu mwanzo walipocheza mechi ya kwanza, ndio maana hakuwa na wasiwasi wowote.
Alisema baada ya kufungwa na Zambia katika mchezo wa hatua ya makundi, aliyafanyia kazi mapungufu yao ikiwemo kutumia nafasi wanazopata kama walivyofanya katika mchezo wa jana.
“Tumepambana na tumefanikiwa kutwaa ubingwa, nawapongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kuhakikisha malengo yetu yanatimiza.
“Nina imani siku zinavyokwenda timu hii itakuja kupata mafanikio makubwa, endapo itapata sapoti ya kutosha,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mgambo Shooting.