23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yazidi kupeta kriketi ‘Division II’Afrika

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya taifa ya kriketi ya wavulana walio chini ya umri wa miaka 19 ya Tanzania imeendeleza wimbi la ushindi katika michuano ya Daraja la Pili ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi, lihusishalo wachezaji wa umri huo, kwa kuichapa Ghana kwa mikimbio 162 jijini Dar es Salaam jana.

Katika mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania ilipata fursa ya kuanza kupiga mpira na kupata mikimbio 215 huku wapiga mpira wote wa timu hiyo wakitolewa katika ova 35.4.

Waliofanya vizuri katika zamu ya timu hiyo kupiga mpira wakikuwa ni Karim Kiseto aliyepata mikimbio 91 na kumaliza zamu akiwa ni mpigaji mpira mwenye mikimbio mingi zaidi.

Mchezaji huyo ameibuka kuwa tegemeo katika timu ya taifa ya Tanzania, kwani katika mechi ya kwanza dhidi ya Nigeria iliyochezwa jijini wikiendi iliyopita alipata mikimbio 57.

Kwa maana hiyo, mchezaji huyo kwa sasa ni mmoja wa wachezaji wanaoongoza kuwa na mikimbio mingi katika michuano hiyo.

Wengine waliong’ara katika zamu hiyo ya kupiga mpira katika mechi dhidi ya Ghana walikuwa ni Dylan Thakrar, ambaye alipata mikimbio 47, Augustine Mwamele aliyemaliza na mikimbio 19, na Omary Ramadhan aliyemaliza na mikimbio 10.

Kwa upande wa Ghana, waliopata wiketi wakati wa zamu ya timu hiyo kurusha mpira ni nahodha Lee Nyarko, aliyemaliza akiwa na wiketi nne, David Ateak aliyepata wiketi tatu, na Derrick Ateak aliyepata wiketi mbili.

Timu ya taifa ya Ghana, ambayo ilitakiwa kupata mikimbio 216 ili kuibuka na ushindi, haikufua dafu ilipofika zamu ya timu hiyo kupiga mpira baada ya kuishia kupata mikimbio 53 tu katika ova 16.3 huku wapigaji mpira wote wa timu hiyo wakitolewa.

Waliofanikiwa kujitutumua wakati wa zamu ya timu hiyo kupiga mpira ni wawili tu, Bernard Kotei aliyepata mikimbio 20 na Aariz Sood aliyemaliza akiwa na mikimbio 18, huku waliobaki wakishindwa kuhimili mikiki mikiki ya warushaji mpira wa Tanzania.

Warusha mpira wa timu ya taifa ya Tanzania walifanya kazi kubwa kuwadhibiti wapigaji mpira wa timu ya taifa ya Ghana, huku nahodha Laksh Bakrania na Khalid Juma wakiongoza jtihada hizo kwa kupata wiketi nne kila mmoja.

Huu ni ushindi wa pili mfululizo kwa timu ya taifa ya Tanzania, ambayo ilianza michuano vizuri kwa kuitandika Nigeria kwa wiketi sita.

Katika mechi nyingine iliyochezwa katika uwanja wa Gymkhana, Nigeria ilipata ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo kwa kuichapa Msumbiji kwa mikimbio 314.

Timu ya taifa ya Tanzania, katika mechi ya tatu, itakuwa ikiwania kujikita kileleni mwa kundi B la michuano hiyo kwa kucheza na timu ya taifa ya Msumbiji kesho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles