Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Jumla ya waogeleaji saba wanaounda timu ya vijana ya Tanzania wanatarajiwa kuondoka kesho Agosti 31,2023 kuelekea nchini Israel kushiriki mashindano ya Dunia ya kuogelea yatakayoanza Septemba 4-9, 2023.
Waogeleaji hao wameagwa jana katika hafla fupi na kukabidhiwa bendera iliyofanyika kwenye shule ya Kimataifa ya Tanganyika iliyopo Masaki, Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi bendera kwa wanamichezo hao, Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Mazugu, amewataka vijana hao kwenda kufanya vizuri wakitambua kuwa wamepewa jukumu kubwa la kuliwakilisha Taifa.
“Ninawaomba mtakapokwenda kushindana katika mashindano ya dunia, mtakutana na wachezaji wenye uwezo mkubwa kama nyinyi, tumieni fursa hiyo kutangaza utalii wa Tanzania,” amesema Mazugu.
Aidha, amekipongeza Chama Cha Kuogelea Tanzania(TSA) kwa kazi wanayoifanya kutengeneza waogeleaji wazuri, kwani mchezo huo haujawahi kuiangusha nchi katika mashindano makubwa.
Naye Katibu Mkuu wa TSA, Inviolata Itatiro amesema kushiriki mashindano hayo ni fursa nzuri kwa waogeleaji kwa sababu yanasaidia kupandisha nchi daraja.
Kwa upande wake mwakilishi wa wadhamini wa timu hiyo kutoka maduka ya vifaa vya michezo ya ‘Just Fit’, Ahmed Muharami ameeleza kuwa wametoa udhamini huo ili kuhamasisha mchezo huo kwa vijana na kupata Tanzania imara michezoni.