33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yapata neema ya Trilioni 17 Dubai EXPO

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Ushiriki wa Tanzania katika maonesho ya Dubai EXPO 2020 umezaa matunda baada ya kushuhudiwa utiaji saini wa mikataba 36 ya makubaliano katika sekta mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 17.

Sekta zitakazonufaika ni pamoja na nishati, kilimo, utalii, miundombinu, usafiri na teknolojia.

Utiaji saini huo ambao umeshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan umefanyika wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji ambalo pia limeshirikisha viongozi wa taasisi za Serikali, binafsi na wafanyabiashara mbalimbali.

Sehemu ya washiriki wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kwenye maonesho ya Dubai EXPO 2020.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Godius Kahyarara, amesema mikataba hiyo 36 ina thamani ya Dola bilioni 7.43 ambazo ni sawa na Sh trilioni 17.35.

Miongoni mwa mikataba hiyo umo wa uwekezaji katika umeme, uwekezaji katika Mamlaka ya Bandari (TPA) unaolenga kuondoa msongamano bandarini, kulipa uwezo Shirika la Maendeleo ya Petrol (TPDC) katika biashara ya mafuta, kuliongezea uwezo TTCL katika sekta ya ICT ambao pia utahusisha ujenzi wa kiwanda cha simu za mkononi za kisasa.

Aidha katika eneo la kilimo imesainiwa mikataba minne ikiwemo inayolenga kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuongeza teknolojia na upatikanaji wa nyenzo za kilimo ambapo mradi wa chini una thamani ya Dola 500, kufungua soko la bidhaa za Tanzania katika nchi za mashariki ya kati na kufungua fursa za wakulima katika soko la dunia.

Mkataba mwingine ni ule uliosainiwa baina ya Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar ambao unalenga kukuza utalii wenye thamani ya Dola milioni 100.

Vilevile umo mkataba wa kukuza biashara kati ya Tanzania na Supermarkets za Emirates ambapo wameanza na kahawa na korosho pamoja na ujenzi wa eneo la viwanda Kwala mkoani Pwani.

Mikataba mingine ambayo Rais Samia ameshuhudia utiaji saini wake ni ile inayolenga kufungua masoko ya bidhaa za mboga, matunda na maua (horticulture) kati ya Tanzania na India, kuiongezea uwezo, mtaji na teknolojia Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na uzalishaji wa mbolea kwa kutumia manyoya ya kuku, ngombe na mabaki ya mifugo.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Ashatu Kijaji, akizungumza wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji kwenye maonesho ya Dubai EXPO 2020.

Akihutubia katika kongamano hilo Rais Samia amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuwakaribisha wawekezaji zaidi kuja kuwekeza nchini.

“Leo tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba 36 ni matumaini yetu itaenda kutekelezwa kwa vitendo, na kama kuna changamoto yoyote kutoka Serikali yangu tafadhali nijulisheni haraka,” amesema Rais Samia.

Tanzania ni kati ya nchi 192 zinazoshiriki maonesho hayo yaliyoanza Oktoba Mosi 2021 yakitarajiwa kumalizika Machi 31 ambapo ushiriki wa Tanzania unaratibiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TANTRADE).

Sehemu ya Watanzania waishio Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wakimsikiliza Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza nao.

EXPO ni maonesho ya dunia yanyofanyika kila baada ya miaka mitano yakisimamiwa na Shirika la Kimataifa lijulikanalo kama Bureau of International Exhabition (BIE) lenye nchi wanachama 195 huku Tanzania ikiwa mwanachama tangu mwaka 1973.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles