24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yapata ‘dili’ usajili vizazi

Na ASHA BANI-DAR ES  SALAAM

TANZANIA  imechaguliwa na Umoja wa Afrika (AU) kuwa kati ya nchi tano za Bara la Afrika zitakazoongoza kampeni ya kuongeza kasi ya Usajili wa Vizazi kwa watoto Barani Afrika inayojulikana kama “Bila kuwa na Jina; Utambulisho wa Kisheria kwa kila mtoto; Upatikanaji wa haki kwa kila mtoto”

Kampeni hiyo inaendeshwa kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Umoja wa Afrika (AU).

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika  Novemba 3, mwaka huu inaeleza kuwa Tanzania itatekeleza jukumu hilo katika nchi za ukanda wa Mashariki wa Bara la Afrika na kwamba imechaguliwa kutokana na mafanikio iliyoyapata miaka ya hivi karibuni katika kuongeza kasi ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu hasa usajili wa vizazi kwa watoto.

Sababu nyingine zilizoainishwa ni pamoja na nchi kuwa na utashi wa kisiasa katika masuala ya usajili wa vizazi na kutekeleza kikamilifu kanuni muhimu zinazounga mkono kampeni hiyo.

 Kwa mujibu wa Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu/ Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA ,Emmy Hudson kama nchi kiongozi Tanzania inatakiwa kufanya kazi na Umoja wa Afrika Mashariki ili kufanikisha mambo mbalimbali yakiwemo kuitangaza kampeni ndani ya nchi na katika Ukanda wa Mashariki ya Afrika.

“Kuchukua taarifa za mafanikio  na kuzitangaza katika hafla mbalimbali za kanda na Bara la Afrika na kuwezesha nchi kubadilishana taarifa za mafanikio.

“Pia kusaidia masuala ya Usajili wa matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu  hasa Usajili wa Vizazi kuwa ajenda  ya Umoja wa Afrika na kushiriki katika kutafuta rasilimali fedha kutoka kwa Wadau wa Maendeleo kwa ajili kuendesha masuala ya Usajili wa vizazi katika ngazi ya Kanda na Bara la Afrika.

“Kampeni hii ilizinduliwa mwezi Juni 2020 kwa lengo la kuhakikisha kila mtoto anatambuliwa katika mifumo rasmi ya serikali kwa ajili ya kumwezesha kupata haki mbalimbali  na usajili wa kizazi ni jambo la msingi katika kufikia hatua hiyo,”Alisema Emmy

“Uzinduzi wa kampeni hiyo umekuja katika  wakati sahihi huku wasiwasi ukiongezeka juu ya kushuka kwa  viwango vya usajili wa Vizazi kutokana na  uwepo wa Janga la Homa Kali ya Mapafu (COVID-19).

 Vilevile, kama nchi kiongozi, Tanzania ilipewa nafasi ya kuwasilisha mada katika kikao cha mawaziri na viongozi wa ngazi za juu wa nchi za Afrika kuhusu masuala ya Usajili wa Vizazi ambapo kauli mbiu ya kikao ilikuwa “Kuelekea usajili wa vizazi vyote Barani Afrika; Changamoto na fursa katika kipindi cha ugonjwa wa COVID-19.

 Alisema maamuzi mazuri ya Rais wa Tanzania,Dk. John Magufuli katika kupambana na Covid-19 yaliwezesha huduma za usajili wa vizazi kuendelea kama kawaida kwa kuzingatia  ushauri wa wataalamu wa afya hivyo kuifanya Tanzania kuwa taifa la mfano katika Bara la Afrika.

Kwa mujibu wa Mtendaji huyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania ilifanya maboresho  katika mfumo wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu hasa usajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto.

Maboresho hayo yalifanywa kupitia Mpango wa Usajili wa Watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

“Katika kutekeleza miongozo mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa kama  Malengo Endelevu  ambapo Lengo la 16.9 linataka nchi wanachama kutoa utambulisho kisheria kwa watu wote ikiwemo usajili wa vizazi ifikapo Mwaka 2030, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na Ilani ya Chama Tawala – Chama cha Mapinduzi (CCM) ,”

“Mpango wa usajili wa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano mpaka sasa unatekelezwa katika mikoa umewezesha kugatua majukumu ya usajili na kusogeza huduma hiyo karibu na makazi ya wananchi ambapo zaidi ya watoto Milioni 5.2 wameweza kusajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa,” alisema Emmy.

Idadi hiyo imefanya  kuongeza kiwango cha usajili ya watoto wa kundi hilo kutoka asilimia 13 mwaka 2012 mpaka kufikia asilimia 49.4 Mwaka 2020 huku utekelezaji katika mikoa 8 iliyobaki unatarajiwa kukamilika Mwaka 2022.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles