Na Mwandishi Maalum, Madrid, Hispania
UJUMBE wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro upo Jiji la Madrid nchini Hispania, kushiriki mkutano mkuu wa 24 wa Kimataifa wa Utalii Duniani ulioandaliwa na Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Utalii Duniani ( UNWTO), huku ukitumia fursa hiyo kunadi vivutio vya Tanzania.
Katika mkutano huo wa siku nne ulioanza jana Novemba 30,unaotarajiwa kufunguliwa rasmi leo Desemba Mosi, ambapo Waziri Ndumbaro ameweka bayana mambo mbalimbali ambayo Tanzania itanufaika na mkutano huo.
Akizungumzia mambo hayo, Dk. Ndumbaro amesema katika kuhakikisha idadi ya watalii inaongozeka pamoja na mapato yatokanayo na Utalii, suala la kutangaza utalii wa Tanzania katika nyanja za kidunia ni suala ambalo haliepukiki.
Ametaja moja ya kati ya maeneo ya kutangaza utalii huo, ni kuhudhuria mikutano mikubwa duniani ikiwamo kwenda Hispania ambako ndiko makao makuu ya utalii duniani katika jiji la Madrid kwa ajili ya kuhudhuria mkutano.
Ikiwa ni siku ya kwanza ya mkutano huo, Tanzania ilipata fursa ya kutangaza vivutio vilivyopo nchini.
”Waje Tanzania wauone Mlima Kilimanjaro, waje Tanzania waione Serengeti, waje Tanzania waione Ngorongoro, waje Tanzania waone fukwe nzuri zenye mchanga mweupe zilizopo Zanzibar, waje Tanzania waone vivutio mbalimbali ambavyo tupo navyo.’’ Amesema Dk. Ndumbaro.
Dk. Ndumbaro amesema jambo la pili katika mkutano huo, Tanzania itasaini mkataba na UNWTO wa kuweza kuwa mwenyeji wa mkutano wa 65 wa Utalii Barani Afrika ambao utafanyika kati ya tarehe 6-8 Oktoba 2022 katika jiji la Arusha.
‘’Mkutano huu tunauleta kwa sababu ni fursa nyingine kwa Tanzania, Tulishapewa kuwa mwenyeji wa mkutano wa utalii wa kanda ya Afrika kule nchini Cape Verde, lakini sasa tumekuja kusaini makubaliano ya kuwa wenyeji wa mkutano huo, baada ya kusaini sasa tutakuwa na uhakika asilimia 100 na tumetengeneza ‘Post card’ ambapo kila mshiriki aliyekuja hapa tunampa post kadi hizi ambayo inasaidia sana kutangaza utalii wa Tanzania.
‘’Jambo lingine ambalo tunalifanya katika mkutano huu, ni kupitisha sheria ya kutetea haki za watalii duniani pale inapotokea matatizo. Tumejifunza kutokana na kadhia ya Uviko- 19 kwamba nchi zilifunga mipaka na baada ya nchi kufunga mipaka, watalii walikuwa wapo kwenye nchi zingine na hawaweza kurudi.
‘’Sasa haki zao zilikuwa haziwezi kutetewa na sheria za kimataifa. Kwa hiyo sasa tunapitisha sheria ya kimataifa ya kutetea watalii katika mazingira ya dharura kama hayo. Ni sheria ambayo itaongeza heshima ya baishara ya utalii duniani kwa sababu unapolinda haki ya mtalii, mtalii anajiona yupo salama zaidi kuja na kushiriki katika nchi yako, Tanzania tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sheria hiyo inapita.’’ Amesema Dk. Ndumbaro.
Amefafanua kuwa mkutano huo una faida nyingi kwa nchi katika kutimiza idadi ya watalii milioni tano na mapato zaidi ya bilioni sita.