23.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 28, 2023

Contact us: [email protected]

Tanzania yaamka kuunganisha intaneti shule za sekondari

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Ujenzi na Miundombinu Profesa Faustine Kamuzora akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Jangwani, wakati wa kusaini makubaliano kati ya serikali na kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Kampuni hiyo itaunganisha shule za sekondari na intaneti kupitia mradi wa E-Schools.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Ujenzi na Miundombinu Profesa Faustine Kamuzora akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Jangwani, wakati wa kusaini makubaliano kati ya serikali na kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Kampuni hiyo itaunganisha shule za sekondari na intaneti kupitia mradi wa E-Schools.

Na Hamisa Maganga,

NCHI jirani zimepiga katika suala la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) shuleni. Moja ya nchi ambazo zinatajwa kuwa mbali zaidi katika suala hilo ni Rwanda, ambayo inasemekana kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi nchini humo wanatumia kompyuta mpakato darasani.

Inasemekana kuwa shule za msingi 1200 nchini humo wanafunzi wake wanatumia kompyuta mpakato.

Kwa upande wa Tanzania, kinachofurahisha ni kwamba shule nyingi za binafsi zimekuwa zikifundisha pia somo la Tehama na serikali haiko nyuma katika kuunganisha shule za serikali za msingi na sekondari kwenye Tehama.

Sasa hivi Tehama haionekani tu kama kitu cha kuongeza ubora wa huduma bali ni eneo la kimkakati katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Katika kuonesha umuhimu wa intaneti shuleni, Kampuni inayoongoza kwa mtindo wa maisha ya kidijitali Tigo Tanzania, imeingia ubia na Wizara ya Mawasiliano, Ujenzi na Miundombinu, katika kuwezesha kufikiwa kwa intaneti katika shule za sekondari nchini, lengo likiwa ni kuwezesha elimu kielektroniki shuleni katika zoezi ambalo litachukua miaka miwili.

Kama sehemu ya makubaliano hayo, wizara itabainisha na kutoa orodha ya  shule zisizo na maabara za kompyuta ili ziunganishwe na hali kadhalika  kuongoza utekelezaji wa mradi  wakati Tigo itadhamini maendeleo ya miundombinu shuleni, ikiwa ni pamoja na kuunganisha nyaya ndani ya madarasa na kufunga visivyotumia nyaya (LAN) na vituo vinavyofikia  mtandao wa intaneti.

Akisaini makubaliano hayo katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Tigo, Shavkat Berdiev, alisema: “Kupitia idara yetu ya huduma kwa jamii hivi sasa tunatekeleza  dira ya serikali ya kuibadilisha nchi kuingia katika uchumi uliojikita katika uelewa ifikapo mwaka 2025 na kampuni yetu  imejipanga kuhakikisha  shule nyingi za sekondari Tanzania  zinafikiwa na mtandao wa intaneti.

“Tunajivunia  kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano, Ujenzi na Miundombinu  katika kuwezesha vijana na jamii kwa ujumla  kuingia katika  mkondo wa kidunia wa habari  na uelewa, ambako watajifunza, kupanua uelewa wao na kushirikiana na wenzao katika sehemu mbalimbali duniani.”

Berdiev aliongeza kusema, “Tigo itaendelea  kufanya kazi na serikali  katika miradi  mingine ya ubunifu na inayovutia ili kunyanyua maisha ya Watanzania walio wengi.”

Akiishukuru Tigo wakati wa kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Ujenzi na Miundombinu Profesa Faustine Kamuzora alisema; “ni kupitia ushirikiano kama huu ndipo tutaweza kusambaza stadi za kisasa za Tehama pamoja na uelewa kwa vijana ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto zinazotokana na mtiririko wa mabadiliko ya habari ya kila siku ndani ya jamii na katika uchumi wa dunia.”

Profesa Kamuzora aliongeza; “Naipongeza Tigo kwa utayari wake wa kujiingiza katika makubaliano baina ya sekta binafasi na sekta za umma ili kuwasaidia wanafunzi wa shule za sekondari nchini, vile vile tunakaribisha wadau wengine  kushiriki kuunganishwa kwa teknolojia hii.

Mradi wa kielektroniki shuleni (eSchools) ni moja ya miradi mkakati ya uwekezaji kijamii ya Tigo na hadi sasa tumeweza kuunganisha shule 31 za sekondari za serikali  na  mtandao wa intaneti ikiwa na mpango wa baadaye wa kuziunganisha  shule 50 kwa mwaka huu.

Ufungaji wa intaneti shuleni kwa namna moja au nyingine unaweza kuleta mabadiliko makubwa kiasi cha kupunguza hata utoro kwa wanafunzi. Akizungumza kuhusu umuhimu wa intaneti shuleni, Mwalimu wa shule moja ya sekondari iliyopo jijini Dar es Salaam,(hakupenda jina la shule litajwe) Shabani Ayoub, alisema vijana waliokimbia shule watatamani kurudi darasani kwa kuwa ni hatua itakayohamasisha wengi kujifunza kompyuta na intaneti.

“Kuna mambo ambayo yanaweza kuhamasisha wanafunzi kupenda shule, kama hili la mtumizi ya kompyuta na kuwapo kwa huduma ya intaneti shuleni,” anasema Mwalimu Shabani.

Kimsingi, hatua ya kupeleka intaneti shuleni ni muhimu na inapaswa kuwa moja ya vipaumbele vya nchi, kwa kufanya hivi tutaweza kuifikisha nchi yetu kwenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Ni vyema mpango wa kuziwezesha shule zote za umma Tanzania kuwa na intaneti ukaharakishwa kwa maana ya serikali na wadau kuongeza juhudi za kusambaza elimu ya Tehama shuleni.

Shule zinapounganishwa kwenye mfumo wa intaneti, licha ya kusaidia katika kutoa maarifa, vijana wetu pia watapata ujuzi wa Tehama ambao una nafasi kubwa katika uchumi wa kisasa.

Hivyo, juhudi za kusambaza umeme vijijini ziende sambamba na kupeleka elimu ya Tehama shuleni kwa kuwa ndiko tutakakoweza kupata maendeleo ya uchumi na rasilimali watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,745FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles