TANZANIA NDANI YA KINYANG’ANYIRO CHA MWANAFUNZI BORA, SHULE INAYOVUTIA AFRIKA

0
847

Na Aziza Masoud, Dar es Salaam

SUALA la utoaji wa elimu bora kwa wanafunzi hasa katika nchi za Afrika Mashariki limekuwa kikwazo kutokana na sababu mbalimbali.

Zipo sababu ambazo zinachangiwa na serikali ya nchi husika lakini pia zipo za kimazingira ambazo zinakuwa kikwazo kwa wanafunzi  kupata ama kushiriki kikamilifu katika elimu.

Hali ngumu ya maisha, umbali wa kutoka nyumbani hadi  shuleni navyo ni vikwazo vinavyochangia watoto wa nchi hizo kukosa elimu.

Kiwango cha elimu kinachotolewa katika nchi za jumuiya hiyo inategemea  na utaratibu uliowekwa kulingana na sera na taratibu za nchi husika.

Katika nchi ya Uganda ambayo inaonekana kukimbiliwa na wanafunzi pamoja na kutajwa kuwa  na gharama nafuu ya ada, utaratibu wa kufundisha kwa mchepuo wa Kiingereza ulikuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania baada ya kuwapo kwa shule chache zinazofudisha kwa lugha hiyo hapa nchini.

Nchi hiyo ambayo ina utaratibu wa elimu ya  msingi na sekondari mpaka kidato cha sita imekuwa kivutio kikubwa kwa Watanzania kwakuwa unafanana na uliopo nchini.

Mbali na Uganda nchi ya Kenya nayo inatajwa kutoa elimu bora. Utaratibu wanaoutumia ni ule wa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi hulazimika kusoma hadi kidato cha nne na baadae kujiunga na vyuo.

Hata hivyo, mfumo huu ulisumbua katika nchi hiyo, kwakuwa wanafunzi wanamaliza na kusoma vitu vikubwa bila kufanyiwa maandalizi ya kutosha.

Kuna wakati fulani mfumo huo ulisababisha kushuka kwa elimu katika nchi hiyo hali ambayo kwa sasa imeshatengamaa.

Nchi ya Rwanda nayo pamoja na kwamba haisifiki kielimu lakini imekuwa na mfumo mzuri.

Rwanda ni nchi ambayo imeweza kujiwekeza katika elimu kwa kuwawezesha wanafunzi wa ngazi kuanzia ya msingi kutumia kompyuta.

Kila nchi imekuwa ikijitahidi kwa uwezo wake ili kuweza  kufikia malengo ya elimu waliyojiwekea.

Tanzania nayo inajulikana kwa kutoa wahitimu wenye sifa na kufanya kazi katika mashirika na miradi mikubwa, licha ya kwamba inatajwa kutoa elimu duni.

Kutokana na sifa hizo, wazazi  wengi kutoka nchi za Afrika Mashariki ikiwamo Kenya hujiunga na masomo hasa ya kidato cha tano na sita kwa ajili ya kujiandaa na elimu ya juu.

Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali za nchi hizo kuhakikisha wanaongeza ubora wa elimu nchini bado kuna changamoto ambazo zinakwamisha sekta hiyo.

Uhaba wa walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia vinatajwa kama sababu ya kudorola kwa ubora wa elimu.

Mbali na hayo, motisha kwa walimu na wanafunzi pia vinachangia kuzorotesha sekta hiyo muhimu nchini.

Mchango wa mwalimu na mwanafunzi anayefanya vizuri katika mitihani hasa ya kitaifa unaonekana kwa kiasi kidogo katika jamii hivyo kushindwa kutoa motisha ambayo itachangia wengine kufanya vizuri.

Yapo baadhi ya mashirika na kampuni ambazo zinajitahidi kutambua michango ya  makundi hayo katika jamii  lakini inakua kwa kiasi kidogo  kutokana na kukosa ushirikiano kutoka sekta husika.

Kampuni ya All Stars Media ni waandaaji tuzo za wanafunzi wanaofanya vizuri zinazoitwa Allstars Students Awards(ASSA). Tuzo hizi hutolewa kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaaluma  katika nchi za Afrika Mashariki.

Kwa mwaka huu kampuni hiyo inatarajia kutoa tuzo nane kwa wanafunzi hao, kati ya tuzo hizo zitakazotolewa ni pamoja na tuzo kubwa itakayaowajumuisha wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa kwa kidato cha nne na sita katika nchi nne za Afrika Mashariki.

Akizungumzia tuzo hizo ambazo zinafanyika kwa mara ya pili sasa Mkurugenzi wa Allstars Media, Aron Mbwana anasema tuzo hizo ambazo zinafanyika kwa mara pili sasa zina lengo la kutambua mchango wa walimu na wanafunzi  ndani na nje ya nchi.

Anasema  tuzo inayohusisha wanafunzi wa kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda itawaangalia zaidi wanafunzi walioongoza katika mitihani ya Taifa ya kidato cha nne na sita kwenye masomo ya Hisabati, Biology, Physics na Chemistry.

“Utaratibu uliotumika kuwapata washindi waliofanya vizuri katika masomo haya ni kuwasiliana na mawaziri  wanaohusika na elimu na kutupatia orodha ya majina katika masomo tunayoyahitaji na baadae tunaangalia walioongoza,” anasema Mbwana.

Wanafunzi nchini Kenya

Anasema wanafunzi wengine watakaopatiwa zawadi kutoka katika nchi hizo ni waliokuwa vinara katika masomo ya Kiswahili na Kiingereza, lengo likiwa ni kuzitangaza lugha hizo.

“Wanafunzi wote wanaopaswa kuchukua tuzo kutoka nchi zote watahudhulia, tumeshawasiliana na mabalozi wao waliopo hapa nchini na wenyewe watakuwepo  kwa ajili ya kushuhudia ghafla hii,” anasema Mbwana.

Anasema  tuzo hizo kwa sasa zinaendelea kuvuka mipaka kwakuwa awali zilitolewa kwa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.

Anasema mbali na tuzo hiyo ambayo imejumlisha  nchi za Afrika Mashariki, ASSA pia itatoa tuzo nyingine saba ambazo zitawahusu wanafunzi  na shule zilizopo nchini.

Anasema tuzo ya kwanza itamuhusu msichana aliyeongoza nchi nzima katika mitihani ya kidato cha nne na sita.

Tuzo nyingine itakayotolewa ni kwa mwanafunzi mwenye kipaji maalumu.

“Hii itatolewa kwa mwanafunzi aliyefanya vitu maalum, mfano kuna mwanafunzi aliwaokoa wenzie na wakanusurika vifo walipokuwa wanavuka maji, tunaangalia vitu kama hivyo,” anasema Mbwana.

Anasema tuzo nyingine itakayotolewa na kampuni hiyo ni ya mwanamichezo bora ambao watapatikana  kupitia matokeo ya Umitashumta na Umisenta.

Anasisitiza washindi wa  kipengele cha michezo  kuanzia mpira wa miguu hadi netiboli watapatiwa fursa ya kuendeleza vipaji vyao kwa kuunganishwa  katika klabu kubwa za mpira.

“Tutawaunganisha na timu kubwa zenye timu za watoto lengo letu baadae waje watoe ushuhuda utakaoionyesha jamii kwamba mbali na tuzo pia yapo mafanikio mengine wameyapata kupitia vipaji vyao,” anasema Mbwana.

Anasema mbali na wanafunzi, tuzo hizo pia zimeangalia shule bora za mwaka ambapo zitaangaliwa zile zilizofanya vizuri kielimu na mazingira.

Anasisitiza kuwa tuzo hizi zitahusu shule za serikali pekee na si binafsi lengo likiwa ni kutoa motisha.

“Kwenye shule bora kielimu tutaangalia shule za serikali zilizoongoza katika mitihani ya kidato cha nne na sita kwa mwaka jana, hatujaziweka shule binafsi kwenye orodha kwakuwa wenyewe huwa wanapatiwa motisha ili kuweza kufikia malengo,” anasema Mbwana.

Anasema tuzo hiyo itaenda samabamba na ya shule yenye mazingira bora ambayo itapatikana kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira inayosimamiwa na Januari Makamba.

“Tuzo hii itatolewa kwa shule ya serikali hakuna shule binafsi ambayo itashindanishwa kwakuwa wao teyari tunajua wana mazingira mazuri,” anasema Mbwana.

Aidha, kampuni pia itatoa tuzo kwa mtu aliyefanya jambo kubwa lililochangia kuinua elimu nchini.

“Hii inaweza ikatolewa kwa viongozi au watu wa kawaida, hapa tumeangalia mtu aliyetoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu na tutampatia tuzo ya ukumbusho,” anasema Mbwana.

Kwa upande wa Meneja wa Matukio wa kampuni hiyo, John Maganga anasema kwa mwaka huu tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Julai 28.

“Watu wajitokeze waje waone jinsi tunavyotoa motisha kwa wanafunzi wanaofanya vizuri, tunategemea kuwa na mabalozi ambao watawasindikiza wanafunzi waliotoka katika nchi zao,” anasema Maganga.

Anasema zawadi zitakazotolewa ni pamoja na vyeti na vifaa vya kujifunzia, mbali na zawadi hizo kampuni hiyo pia ipo mbioni kuhakikisha wanafunzi hao wanapata usajili wa masomo katika baadhi ya shule.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here