24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania na matarajio muflisi uchumi wa gesi

saba

Na Shermarx Ngahemera,

Waandishi wa habari wametakiwa kuwa makini katika kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka kwa wajuzi wa masuala husika, badala ya kutegemea wanasiasa  ambao si wataalamu wanaopenda kupotosha umma  ili waweze kupeleka mbele agenda zao za kisiasa.

Wataalamu wawili wa Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) wamesema hayo kwenye semina ya wahariri iliyofanyika Bagamoyo wiki iliyopita, wakitoa wasiwasi wao  juu ya  upotoshaji wa makusudi  au kwa kutokujua  masuala mahsusi  ya mafuta na gesi  na hivyo kuleta matarajio tarajali yasiyo kamilifu kwa wananchi kuwa neema  yaja na  nchi itakuwa ya asali na maziwa mapema iwezekanavyo.

Wakiwasilisha mada mbili ya ‘Mapitio ya Sekta Rasilimali Gesi Asilia Historia yake, Hali ya Sasa na Mipango ya Baadaye’  iliyotolewa na Mhandisi Shaidu Nuru Mwanajeolojia na Mratibu wa  Mchango wa Nchi (Local Content) wa TPDC na ya ‘Mapitio ya Matumizi, na Mkondo wa Chini wa Gesi Asilia’ iliyotolewa na  Aristides Kato ambaye ni Ofisa Mtafiti wa TPDC, wameonesha wazi  tatizo kubwa  limezuka nchini la ‘kutawala matarajio yaliyokithiri’.

Hali  hiyo inaonekana kutishia ustawi  wa uchumi na uelewa wa watu kuhusu  rasilimali hizo  za mafuta na gesi kama mwarobaini wa  matatizo ya uchumi wa nchi.

“Tathmini  za kitaalamu na uzoefu wa masuala ya uziduaji na mapato ya rasilimali ya mafuta na gesi, yanaonesha  pasipo shaka kuwa nchi za Afrika  mapato yake hayawezi kuwa zaidi ya asilimia 25 ya pato la Taifa na hivyo ni makosa kufikiri kuwa nchi itaenda mbele sana kwa kutegemea  gesi  na mafuta  pekee, ila kwa kuchechemua  sekta nyingine za uchumi. Hivyo, kwa ujumla wake zitabainisha na kugeuza mwelekeo wa sekta hizo  kwa kuzipa kipaumbele kwa mitaji na  hivyo kusisimua uchumi wa nchi husika na uchumi wake kudorora,” walisema wataalamu hao wawili katika nyakati tofauti.

Wataalamu hao wanasema kulifanyika makosa kutoa kauli zilizokithiri wakati mambo bado yako mbali na hali ya uchumi hairuhusu kirahisi kuwekeza kutokana na mdororo wa uchumi duniani kufuatia sababu  hasi lukuki zinazoendelea kudumaza mahitaji ya mafuta duniani, ikiwemo  kuongezeka uzalishaji mafuta Marekani  na kuanza kuuza mafuta yake katika soko la dunia na hivyo kupunguza mahitaji katika soko la dunia kwa asilimia 25.

Sababu nyingine ni kwamba, wakati huu dunia imeshuhudia matumizi  makubwa ya teknolojia  kule Marekani na Canada kufanya mabanzi ya mchanga (shale) kutengeneza  mafuta, hivyo kuleta tafrani na utata kwa wawekezaji  na kudhuru  maendeleo ya miradi ghali ya gesi kama hiyo ya Tanzania ambayo  gesi yake nyingi iko ndani baharini  tcf 47.08 kilomita 120 toka nchi kavu  kwenye kina cha mita 4000 na  ile ilyoko nchi kavu ni tcf 8.04 na hivyo uendelezaji wake ni tatizo.

“Katika utekelezaji wa mradi, maamuzi  ya uwekezaji bado hayajafanyika na wawekezaji wabia wa Staoil ya Norway, Exxon Mobil ya Marekani, Pavilion ya Singapore, Royal Dutch Shell na BG Gas ya Uingereza ; kilichopo sasa ni kiwanja tu cha eneo la Likong’o pale Lindi, ambapo panatarajiwa kujengwa Mtambo wa LNG ambao unahitaji uwekezaji wa kiasi cha dola bilioni 30 (Sh  trilioni 65) sawa na mara mbili ya bajeti ya sasa ya Tanzania.

Alifafanua kuwa mafuta ndio yanayofanyika kibiashara  duniani kote, huku gesi asilia bado ikifanyika kieneo (regional) na hivyo bei ya mafuta ndio inayoamua uwekezaji katika sekta ya nishati na hivyo kuanguka kutoka zaidi ya dola 100 miaka miwili iliyopita na kuwa chini ya dola 40 mwaka huu. Hivyo kuuathiri uwekezaji wa Lindi kwani Msumbiji nayo imegundua gesi nyingi ya kiasi cha zaidi ya tcf 200 ukifananisha na tcf 57.2 ya Tanzania na hivyo kuwa mshindani mkubwa kwenye uwekezaji.

“Wawekezaji hawawekezi  mwanzo katika gesi ila hutafuta mafuta na hivyo gesi asilia ni matokeo (by product) ya utafutaji mafuta na hivyo hutegemea bidhaa hiyo kwa uwekezaji  wake mpaka pale tutakapofikia 2050 ambapo dhana ya ‘ban the unburnable’ itakaposhamiri  na kutumiwa  kwa nguvu kufuta nishati itokanayo na mafuta(Hydrocarbons) na gesi isiyo na ukaa itatawala dunia kwa hali na mali.

Mtazamo na kauli hizo za wataalamu wa TPDC zinaungwa mkono na Mtaalamu Mshiriki wa Taasisi ya Natural Resources Governance Institute (NRGI), Silas Olan’g, ambaye ni Meneja wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (Tanzania ,Ghana, Msumbiji  na Uganda) ambapo  anasema  sasa hivi si wakati mzuri kwa uwekezaji Afrika Mashariki kutokana na hali halisi ya biashara hiyo ambayo  mahitaji yake hupanda na kushuka muda wote na hivyo kushuhudia nchi zinazotaka kufanya  uzalishaji wa biashara ya mafuta kuongezeka kutoka 7 mwaka  2005 na kufikia 20 hadi sasa na kuongeza kuwa ushindani  wa kupata mitaji umeimarika na kuvutia wawekezaji katika bara la Afrika, ni jambo gumu linalohitaji ushawishi mkubwa na hivyo kufanya watawala kuwa na wakati mgumu kufanya maamuzi sahihi kwa kuvutwa na kushawishiwa na matumizi ya mbinu mbalimbali kuweza kuchechemua (lobby) na kuondokana na hali ya mkwamo mbele ya wananchi wao.

“Wawekezaji  wengi hawana haraka na hivyo huzibana nchi masikini kama Tanzania kuzilazimisha kufanya maamuzi ambayo yatafanya rasilimali hizo zichukuliwe karibu na bure kwa kuweka hali ya sintofahamu na ile ya ninataka- sitaki ili wafaidi zaidi, hivyo kutaka ujuzi wa kufikiri na kujadili bila kuonesha hisia halisi ili kulinda masilahi ya nchi,” alichagiza Meneja huyo wa NRGI.

Olan’g anasema kwa miaka mingi, biashara ya mafuta imetawaliwa na maamuzi ya Umoja wa Wazalishaji wa Mafuta Duniani (OPEC)  na kwa misingi ya kisiasa  na ukuaji uchumi wa China ukivuta uchumi huo, lakini sasa mapinduzi ya kiteknolojia ndio mhimili unaoendesha mwenendo wa  biashara ya mafuta na gesi na dunia iko kwenye mabadiliko ambayo hakuna mwelewa kamili na hivyo kufanya maamuzi mengi kumesitishwa  ili kupata picha kamili ya mambo.

Wakati mwingine ni mkakati unaotumiwa na nchi tajiri kupata masharti mazuri ya kufanya kazi na kuzibana nchi changa na masikini  ili zikubaliane na choyo cha wakubwa kwa kuchelewesha  maamuzi.

Kwa kufanya hivyo, Olan’g anasema kunaongeza ushindani ili kupata mitaji na  hivyo kujenga mzingo  juu ya thamani  halisi ya mahitaji ya nchi zinazoendelea ambazo wananchi wake wana kiu ya maendeleo ya haraka, kwani dunia sasa ni kijiji na hivyo kuzilaumu Serikali zao kwa kuchelewesha kufanya maamuzi na kupenda rushwa, madai ambayo mara nyingi si kweli, bali ni hali tu.

“Viongozi  wana wakati mgumu sana na kutakiwa kufanya maamuzi magumu kwenye  uwekezaji huo, kwani  kila mdau ana madai yake na anataka yafanyike kwa masharti yake bila kujali mahitaji stahiki ya nchi ambayo ndio yenye rasilimali na hivyo kuendeleza laana ya rasilimali kwa migogoro isiyokwisha,” alibainisha Olan’g.

Alihitimisha kwa kusema kuwa mwenendo uliopo sasa ni  kushughulikia miradi yenye gharama nafuu na ambayo inahusisha kuwepo kipengele cha uimarishaji wa masuala ya mapato ya fedha (fiscal stabilization clause) kwa bei ya chini na iliyo ya juu (Windfall profits)  kutozwa kodi si chini ya asilimia 10, wakati ingekuwa yote iwe mali ya nchi  kwani Kampuni haikufanyia kazi mapato hayo na mshiko wa Serikali (Government take) ambayo wakati mwingine hufikia kuwa ni asilimia zaidi ya 80 ya mapato. Anaendelea kusema kuwa hali ya mabadiliko ya mara kwa mara, bei na uzalishaji na kwa kuwa gesi ni rasilimali inayokwisha, ni vizuri kuweka mbele masilahi ya vivazi vijavyo kwa kuanzisha Mfuko Maalumu wa Kuendeleza Utajiri (Sovereign Wealth Fund ) na kuudhibiti vilivyo ingawa kwa suala la Tanzania mfuko huo una kasoro kadhaa.

Kwani umewekewa kiwango mahsusi cha asilimia 3 ya GDP chini ya hapo bila kufikia kiwango hicho rasmi  cha Pato la Taifa, hakuna fedha zitakazopelekwa TPDC na  SWF na hivyo kufanya nia nzuri ishindikane kutimia badala ya kutegemea  asilimia ya mauzo ghafi ambayo  ingeihakikishia TPDC kipato kama Kampuni ya Taifa ya Mafuta (NOC) na vilevile kuwekeza kwenye SWF na kufifisha mwenendo na mategemeo ya wengi katika sekta hiyo.

Olan’g anatoa ushauri kwa Serikali kuwa pamoja na Norway kuwa mfano mzuri kwa SWF, hali ya Tanzania ni tofauti lakini kinga ya uhakika kwa vizazi vijavyo kuhusu rasilimali itokanayo na mafuta na gesi ni mawanda ya uchumi (diversification) na si fedha za mauzo ghafi kwani gesi inaweza kuleta si zaidi ya  asilimia 12 ya pato la taifa au dola bilioni 3 kwa mwaka kwenye masharti mazuri.

Je umasikini Tanzania utaondoka kwa kiwango hicho? Ni swali mkakati kwa wahusika wote nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles