TANZANIA NA JUKUMU ZITO LA KUHUDUMIA WAKIMBIZI

0
943

Na CHRISTINA MWANGOSI, WIZARA YA MAMBO YA NDANI

JUNI 20 ya kila mwaka hufanyika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, huku Tanzania ikitajwa kuwa moja ya nchi zilizo na jukumu zito la kuwahudumia.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku hiyo kila mwaka, huku maadhimisho hayo yakilenga kuhamasisha mataifa mbalimbali kuendelea kuwahifadhi na kuwahudumia wanaokimbia nchi zao za asili kutokana na machafuko na majanga mbalimbali, kama mikataba ya kimataifa inavyoendelea kusisitiza juu ya kuendelea kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), ambalo kwa hapa nchini hufanya kazi za kuwahudumia wakimbizi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Huduma za Wakimbizi kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yatafanyika Dar es Salaam na kauli mbiu ya mwaka huu ni ‘Tupo Pamoja Na Wakimbizi’.

Tanzania imeendelea kuwahifadhi na kuwahudumia wakimbizi ambao wamelazimika kuyahama makazi yao  kwa sababu ya vita na machafuko na kwa mujibu wa UNHCR, watu milioni  43 duniani kote wamelazimika kuyahama makazi yao kwa sababu ya vita, machafuko au majanga ya asili na kati yao, milioni 10 wanahudumiwa na shirika hilo.

Mwaka 2016/17, Tanzania kwa kushirikiana na UNHCR na wadau wengine, imeendelea kutoa hifadhi na huduma kwa wakimbizi kutoka nchi jirani, Maziwa Makuu za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kutafuta suluhisho la kudumu la tatizo la wakimbizi hao.

Hadi kufikia Juni 5, mwaka huu, idadi ya wakimbizi wanaohifadhiwa Tanzania imefikia 344,542 katika kambi za Nyarugusu, Nduta, Mtendeli zilizoko Mkoa wa Kigoma na wengine katika makazi ya Katumba, Mishamo, Ulyankulu na Chogo.

Mkurugenzi wa Idara ya Kuhudumia Wakimbizi hapa nchini, ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Harrison Mseke, anasema Serikali inaendelea kupokea wakimbizi wapya kutoka katika nchi za Burundi na DRC.

Anasema awali wakimbizi kutoka Burundi walikuwa wakipokelewa moja kwa moja kwenye makambi, bila kufanyiwa mahojiano ya kina kutokana na kuingia kwa makundi makubwa.

Anasema baada ya hali ya usalama nchini Burundi kuimarika, wengi wao wanakimbia kutokana na ukame ulioikumba sehemu kubwa ya nchi hiyo.

Anasema Februari, mwaka huu, Tanzania ilisitisha utaratibu wa kupokea na kuwasajili wakimbizi bila kuwahoji kwa kina (prima facie recognition) na kuendelea na utaratibu wa kawaida wa kila mkimbizi kuhojiwa na Kamati Maalumu ya Kitaifa ya Kujadili Maombi ya Waomba Hifadhi.

“Serikali kwa kushirikiana na UNHCR na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), inaendelea kutekeleza mradi wa kuwahamishia nchini Marekani wakimbizi kutoka DRC ambao wanaishi katika kambi ya Nyarungusu. Tangu Julai, mwaka jana hadi mwishoni mwa Mei, mwaka huu, wakimbizi 6,983 wamehamishiwa nchini humo,” anasema Mseke.

Anasema pamoja na mpango huo, jumla ya wakimbizi 227 wa DRC walihamishiwa katika nchi za Australia (23), Canada (427), Uingereza (2) na Sweden  (5).

Pamoja na changamoto mbalimbali za kuwahudumia na kuwahifadhi, mwishoni mwa Desemba, 2012, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilifanikiwa kuifunga Kambi ya Mtabila na kubaki kambi moja tu ya Nyarugusu, iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, iliyokuwa na wakimbizi zaidi ya 35,000 kutoka nchi ya Burundi.

Anasema sasa Tanzania imebakiwa na kambi ya Nyarugusu ambayo ina zaidi ya wakimbizi 65,084, wengi wao wakiwa ni kutoka DRC.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, anasema kwa kuwa hali ya usalama katika baadhi ya maeneo nchini Burundi imeimarika, Serikali ya Tanzania imependekeza kuwapo mazungumzo ili kuwawezesha wakimbizi watakaopenda kurejea kwao kwa hiari warudi.

Anasema mwaka 2016/17, UNHCR   kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeanza kuwasajili wakimbizi wanaoishi nchini.

Anasema NIDA imepanga kutekeleza zoezi hilo kabla ya kuanza usajili wa raia wa Tanzania katika Mkoa wa Kigoma, ambako kuna kambi nyingi za wakimbizi.

Meja Jenerali Rwegasira anasema  Serikali ilitoa uraia kwa wakimbizi 162,156 wenye asili ya Burundi walioingia nchini mwaka 1972 na kupangiwa kuishi katika makazi ya Katumba, Mishamo mkoani Katavi na Ulyankulu, mkoani Tabora na kwamba kwa sasa Serikali inatekeleza mradi wa utangamanisho (local integration), ambao utawahamasisha raia hao kuhamia katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, anasema ili kupunguza athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya kupata  nishati ya kupikia, fito  za kujengea  katika maeneo ya ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo, wizara yake kwa kushirikiana na UNHCR, imeanza kutekeleza mradi wa kutumia majiko ya gesi kupikia badala ya kuni katika kambi ya Nyarugusu kwa awamu ya kwanza, ambapo mitungi 3,216, imegawiwa kwa wakimbizi.

 

Hatua hii ilitokana na Tanzania katika bajeti yake ya mwaka 2016/17 kuahidi kutekeleza miradi inayolenga kupunguza athari za uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kiholela kwa ajili ya kupata nishati ya kupikia, fito za kujengea na kuhamasisha upandaji wa miti katika maeneo ya ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo.

Waziri Mwigulu anasema katika kupunguza na kukabiliana na uharibifu wa mazingira, miche ya miti 1,481,592 imekuzwa na kupandwa ndani ya kambi na maeneo yanayozunguka kambi hizo.

Anaongeza kwamba, sasa ujenzi wa nyumba 15,664 ambazo zitatumia matofali mabichi na kuezekwa kwa kutumia mabati, badala ya kutumia fito za miti ambazo zinachangia uharibifu wa mazingira unaendelea.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi na Jumuiya ya Kimataifa linaamini suluhisho la kudumu kwa tatizo la wakimbizi ni kwa wakimbizi kupata nafasi ya kurejea kwao kwa hiari, baada ya mazingira yaliyowafanya kuzikimbia nchi zao  za asili kutoweka.

Jambo hili litafanyika na kufanikiwa pale Serikali za nchi na Jumuiya ya Kimataifa zitakapochukua hatua za makusudi kuhakikisha sababu zinazowafanya raia wa nchi mbalimbali kuzikimbia nchi zao zinatafutiwa ufumbuzi. Hii ni pamoja na kuwa na Serikali zinazozingatia sheria, utawala bora na haki za binadamu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here