Tanzania mbioni kunufaika mafuta,gesi

0
650
Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa 

Mwandishi Wetu

TANZANIA ipo mbioni kunufaika katika sekta ya mafuta na gesi, hasa  ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanzania.

Hatua hiyo, imefikiwa baada ya kampuni za Zarubezhneft na United Metallurgical za nchini Urusi kuonyesha  nia  ya kuwekeza nchini katika sekta hiyo.

Ujumbe wa kampuni hizo ulifanya mazungumzo na Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa  wakati wa  kongamano baina ya Afrika na Urusi lililofanyika  jijini Sochi, Urusi kwa siku mbili mwishoni mwa wiki.

 “Tanzania tuna sera na sheria nzuri na rafiki kwa uwekezaji na tunakaribisha sana wawekezaji nchini kwetu” alisema Majaliwa.

Alielezea  jinsi Serikali ilivyofanya mapinduzi kuchochea ukuaji wa uchumi na kusisitiza kuhusu sera ya viwanda ambayo ndio itakayoifikia Tanzania katika lengo la 2020 kuwa nchi yenye uchumi wa kati.

Katika mazungumzo hayo kampuni hizo zilipata fursa ya kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC),Dk. James Mataragio.

 Mataragio alieleza kampuni hizo  kuhusu maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi kuwa kwa miaka 50 wamepiga hatua kwa  kugundua gesi asilia na kufanikiwa kuizalisha kwa matumizi ya kuzalisha umeme, nishati viwandani, majumbani na kwenye magari.

Alisema fursa za uwekezaji katika miradi ya mkondo wa chini kama usambazaji  gesi majumbani kwa Mkoa ya Dar es Salaam, mradi wa kupeleka gesi asilia kwenye eneo la uwekezaji Bagamoyo na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mafuta ya kimkamkati.

“TPDC tunajiendesha kibiashara,tunahitaji wabia wa kimkamkati ili kukuwa zaidi na kubadilishana utaalamu na uzoefu na kampuni za Urusi zinakaribishwa kwa kuzingatia Urusi imepiga hatua kubwa katika sekta ya mafuta na gesi,”alisema Mataragio.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni  ya Zarubezhneft, Anastasia Korolkova alisema wako tayari  kuwekeza Tanzania kwa sababu Zarubezhneft inashirikiana na kampuni za TOTAL na Equinor ambazo zote zimewekeza Tanzania .

Alisema na wao wanadhani   ni wakati muafaka kwa kampuni  yao kuwekeza nchini ambapo kampuni yao ni inamilikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Urusi na ina pato la takribani dola za Marekani bilioni  moja  kwa mwaka.

Pia kampuni ya United Metallurgical ambayo ni wabobezi katika ujenzi wa mabomba ya gesi walionesha nia ya kushiriki katika mradi wa EACOP ambao Tanzania ni mshirika mkubwa pamoja na miradi ya usambazaji gesi nchini Tanzania na katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Kongamano la Urusi na Afrika linafanyika kwa mara ya kwanza jijini Sochi likiwa na lengo la kufungua uwanja wa ushirikiano baina ya Urusi na nchi za Afrika,awali Urusi ikiwa katika Umoja wa nchi za Kisoviet (USSR) ilishirikiana   na Tanzania hususan katika elimu na ulinzi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here