23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania kurusha uwanjani tena kesho michuno ya kriketi

Na Winfrida Mtoi

TIMU ya taifa ya kriketi ya wavulana walio chini ya umri wa miaka 19 ya Tanzania itaendeleza juhudi za kujihakikishia kushiriki Kombe la Dunia la mchezo huo kwa kupambana na Ghana katika mechi ya michuano ya Daraja la Pili ya Afrika itakayofanyika katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kesho.

Michuano hiyo ya Daraja la Pili ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi la ICC U-19 inachezwa jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 31 mpaka Agosti 11 ikihusisha timu nane, huku mechi zikichezwa katika viwanja vya Gymkhana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Timu zote mbili zilianza michuano hiyo vizuri, ambapo Tanzania ilipata ushindi wa wiketi sita dhidi ya Nigeria katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Gymkhana.

Katika mechi hiyo, Nigeria ilipata fursa ya kuanza kupiga mpira na kupata mikimbio 127 huku wapigaji mpira wote wa timu hiyo wakitolewa.

Femi Oresenwo, aliyepata mikimbio 26, na Ali Rahmon, aliyemaliza akiwa na mikimbio 20, walikuwa ni wapigaji mpira waliokuwa na mikimbio mingi kwa timu ya Nigeria.

Kwa upande wa Tanzania, Laksh Bakrania, ambaye pia ni nahodha wa timu, na Augustine Mwamele walipata wiketi tatu kila mmoja, na Ally Hafidh alimaliza akiwa na wiketi mbili.

Tanzania, baadae, ilifanikiwa kupata mikimbio zaidi ya mpinzani wake wakati wa kupiga mpira, ambapo ilipata mikimbio 128 huku ikipoteza wapigaji mpira wanne na hivyo kushinda kwa wiketi sita.

Karim Kiseto, aliyepata mikimbio 57, na Hamza Ally, aliyekuwa na mikimbio 20, waling’ara wakati wa kupiga mpira kwa timu hiyo.

Ghana ilianza michuano kwa kuishinda Msumbiji kwa wiketi nne katika mechi iliyochezwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mechi hiyo ilishuhudia timu ya Msumbiji ikipata mikimbio 80 wakati wa kupiga mpira na Ghana ikifanikiwa kuvuka idadi hiyo kwa kupata mikimbio 81 huku ikipoteza wapigaji mpira sita na hivyo kushinda kwa wiketi nne.

Ofisa Habari wa Chama cha Mchezo wa Kriketi Tanzania (TCA) Atif Salim alisema mapema wiki hii kuwa washiriki wa michuano hiyo wamewekwa katika makundi mawili.

Kundi A linaundwa na Botswana, Malawi, Sierra Leone, na Rwanda wakati kundi B lina timu za Ghana, Msumbiji, Nigeria, na wenyeji Tanzania.

Michuano hiyo, kwa mujibu wa ofisa huyo, ni hatua muhimu kwa timu zinazowania kushikiriki katika michuano ya kriketi ya Dunia ya ICC inayohusisha vijana walio na umri chini ya miaka 19 inayotarajiwa kufanyika katika nchi za Namibia na Zimbabwe mwaka 2026.

Salim aliongeza kuwa michuano hii ya Daraja la Pili ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi la ICC U-19 itashuhudia timu zitakazomaliza nafasi za kwanza na pili kwa kila kundi zikifuzu kushiriki katika hatua ya nusu fainali.

Baada ya hapo, timu zitakazofanikiwa kwenda fainali zitafuzu moja kwa moja kushiriki katika michuano ya Daraja la Kwanza ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi la ICC U-19.

Ofisa huyo alisema kuwa timu itakayoshinda mchezo wa kuwania nafasi ya tatu vile vile itafuzu kushiriki katika michuano ya Daraja la Kwanza ya Afrika.

Mwenyekiti wa TCA, Balakrishna Sreekumar, alisema wakati wa sherehe za ufunguzi wa michuano: “Nina furaha kubwa wakati tukijiandaa kuwa wenyeji wa michuano ya Daraja la Pili ya Afrika ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi la ICC U-19 itakayofanyika jjini kuanzia Julai 31 mpaka Agosti 11 mwaka huu.”

“Ninalishukuru mno Baraza la Dunia la Mchezo wa Kriketi (ICC) kwa kuiona Tanzania inafaa kuandaa michuano hii na ninawahakikishia wadau wote kuwa tutajitahidi kuifanya ICC na wapenzi wote wa kriketi duniani wajivune.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles