TANZANIA inatarajia kupata madaktari bingwa wa matibabu ya saratani ya watoto baada ya kupata udhamini wa masomo kutoka Taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation.
Taasisi hiyo imetoa nafasi za masomo kwa madaktari watatu, ikiwa ni sehemu ya mpango wake kuwajengea uwezo madaktari wa Tanzania ili waweze kuwa wabobezi katika matibabu ya saratani kwa watoto.
Madaktari hao wamepewa fursa za kusomea Shahada mpya ya Uzamili katika matibabu ya saratani kwa watoto wadogo inayotolewa na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili na watakuwa madaktari wa kwanza nchini kuwa na sifa za kitaaluma katika tiba hiyo.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Hatim Karimjee, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba taasisi hiyo inataka kuweka mazingira endelevu katika ubora wa huduma za afya kwa kuwajengea uwezo madaktari kuweza kuwatibu watoto wadogo wenye ugonjwa wa saratani.
“Ili kutimiza lengo hili ni lazima wapatikane madaktari wenye sifa nchi nzima,” alisema Karimjee, wakati akizungumza kwenye hafla ya kuwapongeza madaktari waliomaliza kozi hiyo mwaka 2015 na wanaoanza kozi ya 2016 chini ya udhamini wa Karimjee Jivanjee Foundation.
“Mwaka 2014, Tanzania haikuwa hata na daktari mmoja mwenye sifa za kutibu saratani kwa watoto, lakini baada ya Daktari Trish Scanlan pamoja na Taasisi ya Tumaini la Maisha kuanzisha kozi hiyo ya uzamili kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Tiba Muhimbili, taasisi ya Karimjee iliona kwamba ni muda muafaka kutoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania katika eneo hili na ndiyo maana tuliamua kusaidia programu hii,” alisema.
Mwaka 2014 taasisi hiyo ilitoa nafasi za masomo kwa madaktari wawili kusomea kozi hiyo mpya pamoja na mafunzo ya miezi mitatu nchini Ireland ili kupata uzoefu wa kimataifa ambapo kozi nzima iligharimu Sh milioni 70.
Madaktari walionufaika na programu hiyo ni Dk Rehema Laiti na Dk. Shakilu Jumanne ambao wamemaliza masomo na mafunzo yao na sasa wameajiriwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwenye kitengo cha saratani kwa watoto.