27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

‘Tanzania imefanikiwa uwezeshaji wanawake’

15Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MFUKO wa Hanns Seidel Foundation (HSF), ambao unajihusisha na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja za uongozi, usawa wa kijinsia na masuala ya siasa, umeitaja Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika uwezeshaji wa wanawake duniani.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Mfuko huo ambao makao yake yako nchini Ujerumani,  Profesa Ursula Mannle, katika hafla ya kufanya tathmini ya mchango wa HSF nchini kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake vijana katika nyanja za uongozi, usawa wa kijinsia na masuala ya siasa.

Profesa Ursula alisema HSF imekuwa ikitekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji kwa wanawake kisiasa, kuwaandaa na kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi mahiri katika nchi wanazotoka.

“HSF imeamua kuanzisha programu maalumu nchini kwa ajili ya kuwaangalia wanawake wanaojitokeza kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ili kuwawezesha kuwa viongozi katika nafasi mbalimbali serikalini pia kuziba pengo lililopo la uwakilishi katika nafasi za kisiasa.

“Hanns Seidel Foundation itaendelea kuwaunga mkono wanawake wa Tanzania wanaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za kisiasa nchini Tanzania kupitia programu mbalimbali za ufadhili, ili kuwawezesha kumudu gharama na kuwajengea uwezo wa kushindana katika majukwaa ya siasa,” alisema Profesa Ursula.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akizungumza wakati wa hafla hiyo alisema kuwa Tanzania imeendelea kutoa kipaumbele katika nafasi za uongozi kwa wanawake.

Alisema licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na vijana wa Tanzania zikiwemo za kijamii na kimila, pia ndoa na mimba za utotoni zinachangia vijana na wanafunzi wa kike kuacha masomo yao.

“Tanzania imeendelea kuwathamini wanawake katika uteuzi wa ngazi mbalimbali za uongozi serikalini kuanzia wakuu wa wilaya  na mikoa, wakurugenzi, mawaziri na naibu mawaziri, pia uwepo wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ambaye ni alama ya hamasa na ushindi katika uongozi kwa wanawake wengine Tanzania,” alisema Ummy.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles