Na Faraja Masinde
Takwimu za mwaka huu zilizotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kuwapo kwa mafanikio katika kukabiliana na ajali zinazosababishwa na pikipiki maarufu kama Bodaboda.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2019/20 mbali na kupungua kwa ajali hizo pia hata idadi ya vifo vinavyotokana na ajali hizo vimepungua ikiwamo pia idadi ya majeruhi.
Mfano katika mwaka 2015 idadi ya ajali za pikipiki ziliozoripotiwa kutokea nchini zilikuwa 2,626 ambapo zilisababisha majeruhi 2,370 huku zikigharimu maisha ya watu 934.
Lakini takwimu za mwaka 2019 zinonyesha kuwa ajali zilikuwa 567 zilizosababisha vifo vya Watanzania 316 na majeruhi 469, aidha kwa mwaka huu hadi sasa takwimu hizo zinaonyesha kuwa kuna ajali 240 huku vifo vilivyotokana na ajali hizo vikiwa 147 na kusababisha majeruhi 191.
Hivyo, hiyo inaonyesha fika kuwa kumekuwapo na ahueni katika kupunguza ajali za pikipiki Tanzania ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.
Mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na elimu inayotolewa na jeshi la polisi kwa madereva pamoja na uzingatiaji wa sheria kwa watumiaji wa vyombo vya moto.
Aidha, juhudi hizo zinachochea katika kufikisha lengo namba moja kati ya 17 ya Malengo Endelevu (SDG) ambalo linataka kutokomeza umaskini, kwani ni bayana kwamba ajali nyingi zimekuwa ni chanzo cha umaskini kwa watu wengi.
Pia, inasaidia kufanikisha lengo namba tatu ambalo linataka afya bora kama inavyofahamika kuwa ajali zinasabaisha ulemavu, zaidi angalia takwimu kwenye mchoro wetu.