|Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Tanzania iko hatarini kuambukizwa ugonjwa wa ebola kutokana na ukaribu na muingiliano wa watu baina yake na Congo hasa kuhusiana na wasafiri wanaotoka na kuingia hapa nchini.
Taarifa hiyo imetolea na Wizara ya afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto baada Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), kutangaza kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola Agosti Mosi mwaka huu, ambapo jumla ya wagonjwa 26 na vifo 10 vimeripotiwa na wagonjwa wanne kati yao wamethibitishwa kimaabara kuwa na ugonjwa huo.
“Kwa sababu hizi, Watanzania hatuna budi kuchukua tahadhari ya hali ya juu ili kujikinga na kudhibiti na ugonjwa wa Ebola.
“Hivyo, wizara inapenda kutoa tahadhari ya ugonjwa huu kwa wananchi wote katika mikoa yote ya Tanzania, lakini hasa ile inayopakana na nchi jirani za DRC, Uganda na Rwanda ambapo mikoa hiyo ni pamoja na Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe,” imesema taarifa hiyo.