27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania haina kipimo cha Ebola

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid

Aziza Masoud na Geofrey Jacka, Dar es Salaam

SERIKALI imesema haina vipimo vya kutambua ugonjwa wa Ebola.

Kutokana na hali hiyo imesema ikiwa atatokea mgonjwa mwenye virusi vya ugonjwa huo watalazimika kupeleka damu ya mgonjwa jijini Nairobi nchini Kenya ambako kuna maabara inayoweza kutambua virusi hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema kutokana na hatari ya ugonjwa huo Serikali imetenga Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema hatua ya kutenga fedha hizo inakwenda sambamba na uundwaji wa kikosi kazi ambacho kimeshirikisha wadau wa maendeleo kutoka Shirika ya la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF).

Jingine ni Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na viongozi wa Serikali wa ngazi za mikoa na wilaya.

“Tumetenga bajeti ya Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu. Mipango ya awali ni kuweka mkakati na namna ugonjwa huo utakavyoweza kutambulika mapema, mipango ya awali ni kutumia maabara ya Kemri iliyopo jijini Nairobi kwa sasa wakati uboreshwaji wa maabara zetu unaendelea ili kupata ithibati.

“Fedha zilizotengwa zitatumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya kujikinga, mashine za kupimia viashiria vya ugonjwa huo pamoja na gharama za kutoa mafunzo kwa watendaji na watumishi wa afya wa ngazi zote pamoja na kukarabati maabara zitakazosaidia kupima na kutambua virusi,” alisema Dk. Seif.

“Wizara imeanza kutoa taarifa za tahadhari ya ugonjwa huu kupitia kwa makatibu tawala na waganga wakuu wote wa mikoa na wilaya, taarifa hiyo pia inajumuisha namna mgonjwa anavyoweza kutambuliwa, namna ya kuchukua sampuli na kuwahudumia wagonjwa.

“Pia tumewaagiza waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuitisha mikutano ya dharura ya timu zao za maafa ili kupanga mikakati ya kimkoa na wilaya,” alisema.

Vituo vya Ebola vyatengwa

Waziri huyo alisema Serikali imetenga vituo vya kukabiliana na ugonjwa huo na wameandaa eneo katika Wilaya ya Temeke pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alisema kwa upande wa Muhimbili itakuwa ni chumba maalumu kwa ajili ya wagonjwa ambao wapo hospitali hiyo.

“Kwa Mkoa wa Dar es Salaam kituo cha wagonjwa kimetengwa eneo la Temeke, sehemu hii tutaendelea kuiboresha kwa kuzingatia vigezo maalumu baada ya Kamati ya Taifa ya Maafa ambayo ilitembelea eneo hilo na kubaini upungufu,” alisema.

Alisema Serikali pia itaboresha ufuatiliaji na utambuzi wa ugonjwa katika maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani ili kuweza kubaini wasafiri watakaoonyesha dalili za ugonjwa au viashiria hatari.

Alisema katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA), wizara imeweka fomu maalumu za kuhoji wasafiri ili kutambua abiria wanaoingia na kutoka nchini na kutambua nchi walizotoka.

Alisema vilevile wizara imeagiza ‘Thermoscanners’ zitawekwa katika viwanja vya ndege zitasaidia kurahisisha utambuzi wa wasafiri watakaokuwa wanarudi na dalili za mwanzo za Ebola ambayo ni homa.

Licha ya baadhi ya nchi kuzuia uingiaji wa ndege kutoka nchi za Magharibi mwa Bara la Afrika, Serikali imesema suala hilo kwa Tanzania ni mapema kulifanya mpaka watakapojua athari na hasara zitakazopatikana baada ya kuchukua hatua hiyo.

“Kuzuia kuingia kwa ndege kuna taratibu lakini kwa sasa tunaona hakuna ulazima wa kuzuia ndege kuingia nchini,” alisema Dk. Seif.

Alieleza vifaa vya kujikinga vipo vya kutosha kwa ajili ya matumizi kwa watoa huduma na kwa wagonjwa na vimeanza kusambazwa kutoka katika Bohari za Dawa (MSD) za kanda kwenda hospitali zote za wilaya, mikoa na rufaa.

“Jumla ya vifaa vya kujikinga 12,750 vimenunuliwa na kuanza kusambazwa na tunatarajia kupata vifaa vingine kutoka Zimbabwe kwa msaada wa WHO, idadi ya vifaa itaongezeka kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza,” alisema.

WHO yahadharisha

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Rufaro Chatora, alisema ugonjwa wa Ebola kwa sasa ni janga la dunia nzima na kila nchi inapaswa kujikinga na kuchukua tahadhari.

“Ebola ni janga kubwa kushinda janga lolote duniani, sio kama watu wanavyodhani japokuwa Tanzania bado haujafika lakini wanapaswa kujihadhari kwa kudhibiti mwingiliano wa watu kutoka nje ya nchi,” alisema Dk. Chatora.

Aliongeza kuwa nchi za Afrika Magharibi zimekuwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa huo kutokana na kutokua na tahadhari na wengine kushindwa kutoa taarifa za ugonjwa katika vituo vya afya.

“Kuna watu walikuwa wakipata mgonjwa wanamficha ndani na wengine wanawapeleka vijijini sehemu ambazo watu hawana uelewa na utaalamu wa kuwahudumia wagonjwa hao, hivyo basi hufariki na kuwazika wenyewe kinyume cha taratibu za ugonjwa huo na kuwasababishia maambukizi zaidi,” alisema Chatora.

Padri afariki kwa Ebola

Wakati hayo yakiendelea Tanzania, taarifa kutoka nchini Hispania zinaeleza kuwa Padri Miguel Pajares (75), aliyeambukizwa virusi vya Ebola amefariki dunia.

Padri huyo aliyekuwa akifanya kazi Magharibi mwa Afrika, alifariki kutokana na homa akiwa hospitalini mjini Madrid.

Ugonjwa huo umeua zaidi ya watu 1,000 hasa kwa nchi za Liberia, Guinea, Sierra Leone na Nigeria tangu ulipolipuka mwezi Februari mwaka huu.

Padri huyo alirejeshwa nchini Hispania kutoka Liberia wiki iliyopita akiwa na mtawa mmoja ambaye naye alinusurika kuambukizwa homa hiyo.

Mwili wake unatarajia kuchomwa moto leo ili kuepuka hatari zaidi kwa afya ya umma, taarifa kutoka Hospitali ya Carlos III ilisema.

Parajes alikuwa akifanya kazi katika Hospitali ya San Juan de Dios, iliyo chini ya taasisi ya misaada ya Kanisa la Katoliki na alikuwa akisaidia kutibu watu ugonjwa wa Ebola nchini Liberia hadi alipoambukizwa homa hiyo na kuhamishiwa Hispania.

Baada ya kufanya mkutano kwa njia ya video na wataalamu wa afya duniani, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa ni halali kimaadili kutumia dawa na chanjo za Ebola zisizothibitishwa.

Ilieleza dawa hizo zinapaswa kutumika katika maeneo yenye milipuko wa ugonjwa huo iwapo masharti yatazingatiwa, ikiwamo idhini ya mgonjwa mwenyewe.

Virusi vya Ebola

Ugonjwa wa Ebola husababishwa na virusi ambavyo kitaalamu vipo katika kundi la familia ya ‘Filovirus’ na vipo katika makundi matano.

Kundi la kwanza la virusi hivyo ni Bundibugyo, Cote D’lvoire, Reston, Sudan na Zaire, virusi vya Bundibugyo Sudan na Zaire ndivyo huleta milipuko mikubwa kwa binadamu na kupelekea idadi kubwa ya vifo.

Kwa mlipuko wa sasa katika nchi za Afrika Magharibi kirusi aina ya Zaire ndicho kimethibitishwa kusababisha mlipuko huo.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. jamani hii sasa inasikitisha sana kwani uhai wa watanzania unaonekana sasa kutokuwa na dhamani tena! haiwezekani nchi kama hii kukosa kipimo cha ugonjwa hatari kama huu, sasa hao CCM wanaodai wanaangalia maslahi ya wananchi hili kweli linauhakika kama hilo ni kweli kwanini wasingelijali afya za watanzania kununua kipimo hicho badala ya kupeleka vipimo kenya wanang’ng’ania kila mtu kwenda kwenye mchakato wa bunge ambao iwe isiwe hautakuwa na mwisho, wajumbe wote nawaombeni sana jitahidini msiifanye hii nchi haina mwenyewe lazima tuangalie suala la “ownership” katika nchi hii naona suala hilo halipo kabisa kila mtu anataka kuchukua chake mapema ni aibu sana, sasa mmekuja na propoganda oo kuna ndie raisi wa mwisho kuingoza Tanzania maskini kwani rasilimali zilizopo mngekuwa mnazitumia vizuri ingekuwaje? acheni sanaa angalieni maslahi na wananchi wenu tafadhali machine ya kupimia Ebola ni uhimu sana ikawepo.

  2. jamani wabunge wasitishe hizo posho ili maabara ya kupimia ugonjwa wa ebola ijengwe haraka sana mnataka mpaka afe mtu jamani wakati viashiria mnaviona

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles