29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania haijawekeza kwenye lishe bora ya watoto

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif RashidBILL Gates tajiri mkubwa duniani ambaye ameanzisha Foundation (taasisi ya kutoa misaada) inayosaidia shughuli za maendeleo kama vile huduma za afya, kupambana na Ukimwi, kuimarisha kilimo, kuendeleza elimu na utafiti wa nishati endelevu.
Anaeleza kuwa alipoanza kutembelea vijiji vya Afrika ikiwemo Tanzania alikuwa anakisia umri wa watoto aliokutana nao. Mara kwa mara watoto aliodhani wana umri wa miaka saba au nane umri wao halisi ulikuwa miaka 12 au 13. Watoto wengi wamedumaa kwa ukosefu wa lishe bora.
Watoto wengi wa Tanzania wamedumaa kwa sababu ya tatizo la utapiamlo. Hawakupata lishe bora kwa muda mrefu toka wakiwa katika mimba ya mama na miaka miwili ya mwanzo ya uhai wao. Matokeo yake kimo cha watoto wengi ni cha chini ukilinganisha na umri wao. Watoto wengi hawapati chakula cha kutosha. Baadhi wanakula na kushiba lakini chakula chao hakina lishe bora inayokidhi mahitaji yote ya mwili.
Ukosefu wa lishe bora unapunguza urefu wa watoto, lakini pia unaathiri ukuaji wa ubongo, kinga ya mwili na ukuaji wa maungo. Lishe bora katika siku 1,000 za uhai wa mtoto; toka mtoto akiwa katika mimba ya mama yake mpaka kufikia miaka miwili ni muhimu katika kujenga ubongo wa mtoto, kinga ya mwili na maungo yake. Mtoto akikosa lishe bora katika kipindi hiki hawezi kujifunza na kufanya vizuri shuleni, anaugua mara kwa mara kwa kukosa kinga ya mwili na maungo yake hayana nguvu za kutosha ukilinganisha na mtoto aliyepata lishe bora.
Watoto waliodumaa wanapokuwa watu wazima na sehemu ya nguvu kazi ya taifa wanakuwa na tija ndogo katika shughuli wanazozifanya. Utapiamlo unapunguza nguvu na uwezo wa taifa na kuendeleza umaskini wa watu wake.
Tanzania tuna tatizo kubwa na la muda mrefu la udumavu wa watoto. Mwaka 1991 karibu nusu (asilimia 49.7) ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano walikuwa wadumavu; wafupi sana ukilinganisha na umri wao. Nusu ya watoto hawakuweza kujenga ubongo wao, maungo yao na kinga ya mwili wao kwa kadiri ya Mwenyezi Mungu alivyowajalia kwa sababu ya kukosa chakula na lishe bora ya kutosha.
Mwaka 2010 miaka 20 baadaye asilimia 42.5 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano bado wadumavu. Zaidi ya watoto milioni tatu wenye umri chini ya miaka mitano ni wadumavu kwa kukosa lishe bora. Ukuaji wa uchumi wa wastani wa asilimia saba kila mwaka haujasaidia sana kupunguza tatizo la ukosefu wa lishe bora.
Vietnam ilikuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa lishe bora kwa watoto kuliko hata Tanzania. Mwaka 1993 katika kila watoto 100 wa Vietnam 63 walikuwa wadumavu kwa sababu ya kukosa lishe bora.
Ilipofika mwaka 2010 asilimia ya watoto wadumavu ilipungua na kufikia asilimia 23. Hata Uganda imefanya vizuri kidogo ukilinganisha na Tanzania. Asilimia ya watoto wadumavu imepungua kutoka asilimia 45 mwaka 1995 na kufikia asilimia 34 mwaka 2011.
Mikoa inayoongoza kwa udumavu wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni Dodoma (asilimia 57.1), Lindi (asilimia 53.3), Iringa (asilimia 52), Rukwa (asilimia 51.4), Mbeya (asilimia 51.3), Tanga (asilimia 50), Kigoma (asilimia 48.2) na Ruvuma (asilimia 47.4).
Mikoa ambayo ni maarufu kwa uzalishaji wa chakula hasa mahindi, The Big Four – Iringa, Rukwa, Mbeya na Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye udumavu wa watoto ulio juu kuliko wastani wa taifa. Tatizo la udumavu siyo njaa bali kupata lishe bora.
Mikoa yenye udumavu mdogo ni Dar es Salaam (asilimia 19.7), Mjini Magharibi (asilimia 20.2), Kilimanjaro (asilimia 27.6), Kusini Unguja (asilimia 29.8), Kusini Pemba (asilimia 30.7) na Mara (asilimia 31).
Tatizo la udumavu halisababishwi na njaa au kutoshiba. Watoto wanaweza kupata chakula na kushiba lakini wakawa hawana lishe bora. Hawali vyakula vyenye protein na virutubisho vya kutosha. Ili kuepuka udumavu, mama mjamzito anapaswa kula lishe bora ili azae mtoto mwenye afya bora. Amnyonyeshe mtoto wake kwa miezi sita ya kwanza kabla ya kuanza kumpa vyakula vingine.
Kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa muda wa miezi sita ndio taratibu nzuri zaidi ya kuhakikisha mtoto anakuza ubungo na kuimarisha kinga ya mwili wake. Baada ya miezi sita mama aendelee kumnyonyesha mtoto wake mpaka kufikia alau miaka miwili na pia ampe vyakula stahihi vyenye virutubisho.
Pamoja na vyakula vyenye wanga, mtoto anahitaji vyakula vyenye protein kama vile nyama, samaki na maharage. Pia ni muhimu kupata vitamini na virutubisho vingine vinavyopatikana kwenye matunda na mbogamboga.
Virutubisho muhimu ambavyo vikikosekana vinachangia kusababisha utapiamlo na udumavu ni pamoja na vitamin A, aidini (madini ya joto), madini ya chuma (iron) na zinc. Ukosefu wa aidini unasababisha maradhi ya tezi na pia unazuia kukua na kuimarika kwa ubongo wa mtoto.
Kina mama wajawazito wasipopata madini ya chuma ya kutosha katika vyakula vyao wanakosa damu ya kutosha na wanaweza kupoteza maisha wakati wa kujifungua na watoto wanaowazaa hawana afya njema.
Kwa kuwa familia nyingi hazipati vyakula vyenye protein na virutubisho vingine kila siku, ni vizuri vyakula vinavyotumiwa kila siku kama vile chumvi, mafuta ya kupikia na unga wa mahindi kuviimarisha na virutubisho muhimu ili watoto na wananchi kwa ujumla waweze kuvipata hata kama hawajala matunda. Kuhakikisha chumvi yote inayotumiwa na wananchi wote imewekewa aidini kunaweza kuondoa kabisa tatizo la ukosefu wa madini haya katika lishe ya wananchi. Vitamin A inaweza kuongezwa katika mafuta ya kupikia.
Utafiti wa mazao ya kilimo umefanikiwa kupata mbegu bora kama vile mahindi yenye protein nyingi kuliko mahindi asilia, viazi vitamu vyenye vitamin A na vyenye mazao makubwa zaidi. Wakulima wanaolima mazao haya na kufuata taratibu za kilimo bora wanaongeza kipato chao na kujipatia chakula chenye lishe bora.
Ukosefu wa lishe bora kwa watoto wa Tanzania ni janga la kitaifa. Ni ukatili wa hali ya juu kuwa mpaka sasa hatujaweka kipaumbele kutokomeza utapiamlo. Suala la kupata lishe bora linaanza kwenye familia. Kuelewa na kuchukua jukumu la kuhakikisha kina mama wajawazito wanapata lishe bora.
Pamoja na Serikali kuwa na mpango wa taifa wa lishe, utekelezaji wake unasuasua na unategemea misaada toka nje. Wakati watoto wanaokadiriwa kuwa na utapiamlo ni zaidi ya milioni tatu, mwaka 2013, Serikali kupitia Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania iliwapatia ‘chakula dawa’ jumla ya watu 26,868 wanaoishi na virusi vya Ukimwi na watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano wenye utapiamlo walipata matibabu ya utapiamlo kwa kutumia chakula dawa.
Mfumo mzuri wa kuhakikisha afya na lishe bora kwa watoto wote wa Tanzania, ni kuhakikisha kuwa kila familia inaelewa umuhimu wa lishe bora. Kupambana na utapiamlo kunaambatana na huduma za msingi za afya na mazingira safi ya kuishi na hasa matumizi ya vyoo na upatikanaji wa maji safi na salama.
Zahanati na vituo vya afya vitoe elimu ya lishe bora na kufuatilia matatizo ya lishe bora kwa watoto na mama wajawazito. Mama wajawazito toka familia maskini wapewe vyakula vyenye virutubisho toka zahanati na vituo vya afya. Serikali za vijiji na mitaa hasa ziwe na kamati za lishe bora zitakazojikita katika kusaidia mama wajawazito na watoto wote wanapata lishe bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles