26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tanroads yatumia Sh bilioni 4.1 kujenga barabara

SEIF TAKAZA-SINGIDA 

WAKALA wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Singida, umepanga kutumia zaidi ya Sh bilioni 4.1  kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu ya lami, barabara kuu ya changarawe na matengenezo ya vipindi maalum, ambayo  yalianza kufanyika kati ya mwezi  Julai hadi Novemba mwaka huu.

Kaimu Meneja wa Tanroads Mkoa wa Singida, Matari Masige, alisema hayo jana wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara  kwenye kikao cha 42 Bodi Barabara Mkoa wa Singida, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano ofisi ya  Mkuu wa Mkoa mjini hapa.

Alisema kati ya fedha hizo, zaidi ya Sh 3.1 bilioni, zimetumika kwa ajili ya kugharamia  matengenezo ya kilometa 4.1 za barabara kuu ya lami.

“Barabara hiyo ni inaanzia Kijiji cha Kintinku Manyoni mpakani na Mkoa wa Dodoma hadi Kijiji cha Malendi mpakani na Mkoa wa Tabora. Matengenezo haya yamelenga kuziba mashimo na kuweka tabaka la lami, ili kuimarisha barabara.

 “Lengo mahususi ni kuimarisha barabara. Hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 29.3 kikazi na asilimia 18.8 kifedha ya kazi zote,” alisema.

Aidha, alisema kwa matengenezo ya barabara kuu za changarawe ambayo kazi inatarajiwa kutumia zaidi ya Sh 267.1 milioni, utekelezaji wake umefikia asilimia 84 ya kazi zote.

“Hata hivyo utekelezaji wake umeathirika kutokana na upungufu wa fedha kama nilivyoeleza  awali….(awali alieleza kuwa zaidi ya Sh bilioni 4.2 zilikatwa kwenye bajeti kwa ajili ya kulipia madeni ya nyuma),” Masige alisema.

Kuhusu matengenezo ya vipindi maalum ya barabara za mkoa, Masige alisema matengenezo hayo yamehusisha kuweka lami katika barabara za mkoa zenye urefu wa kilometa 1.0, gharama yake ni zaidi ya Sh 676.3 milioni.

Alisema barabara hiyo ya kiwango cha lami ni ile ya Njuki-Ilongero hadi kijiji cha Ngamu 

“Hadi Novemba 30 mwaka huu, jumla ya kilometa 0.5 zimefanyiwa matengenezo kwa kiwango cha lami, kwa gharama ya Sh 272.7 milioni,” alisema.

Katika hatua ngingine, Masige alitaja baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni upungufu mkubwa wa fedha za miradi midogo ya maendeleo.

“Fedha hizi zimekuwa haziletwi kwa wakati, hivyo kusababisha madeni ya muda mrefu. Hata hivyo tumekuwa tukiwasilisha taarifa kila mwezi kwenye mamlaka husika,” alisema.

Pia alieleza kuwa wanakabiliana na tatizo la kung’oa/wizi wa vyuma na alama za barabarani 

Tanroads Mkoa wa Singida, unahudumia barabara kuu na barabara za mkoa zenye urefu wa kilometa 1,727.6. Kati ya hizo, kilometa 484.2 ni za barabara za lami sawa na asilimia 28. Sehemu iliyobaki yenye urefu wa kilometa 1,243.4 sawa na aslimia 72 ni barabara za changarawe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles