Na Ramadhan Hassan, Mtanzania Digital
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetaja mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha barabara kuu na za mikoa zinapitika majira yote ya mwaka kutokana na matengenezo yanayofanyika kwa wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 17, 2025, Mkurugenzi wa Miundombinu na Mipango wa TANROADS, Ephatar Mlavi, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetekeleza miradi mingi yenye viwango vya juu, jambo ambalo limeimarisha miundombinu ya usafiri nchini.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kukamilika kwa awamu ya pili ya mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yenye urefu wa kilometa 20.3, inayojumuisha barabara za Mbagala – Mzunguko wa Bandari (Bendera Tatu), Bendera Tatu – Kariakoo, Sokoine – Zanaki, na Kawawa – Morogoro (Magomeni). Pia, utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo kutoka katikati ya jiji hadi Gongo la Mboto (km 23.3) umefikia asilimia 74.
Aidha, TANROADS inaendelea na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Dodoma (Outer Ring Road) yenye urefu wa kilometa 112, inayolenga kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji. Hadi Februari 2025, sehemu ya kwanza ya barabara hiyo (km 52.3) imekamilika kwa asilimia 91, huku sehemu ya pili (km 62) ikiwa imefikia asilimia 85.
Pia, TANROADS inatekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ikiwemo upanuzi wa barabara zinazoingia na kutoka Dodoma, kama vile barabara ya Chamwino (km 32), Mkonze (km 4.5), na Zamahero (km 8.5), kupitia mradi wa Dodoma Integrated and Sustainable Transport (DIST).

Katika Jiji la Mbeya, barabara kuu ya TANZAM (Uyole – Ifisi – Songwe Airport) yenye urefu wa kilometa 36 inaendelea kupanuliwa kutoka njia mbili hadi nne ili kupunguza msongamano, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 22. Vilevile, upanuzi wa barabara ya Mwanza – Usagara – JPM Bridge (km 37) unaendelea ili kuboresha mtandao wa usafiri mkoani humo.
Mlavi aliongeza kuwa TANROADS imeweka mkakati wa miaka mitano wa kukuza ushiriki wa wakandarasi wazawa katika miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja, kwa kutenga zabuni maalum kwao kila mwaka wa fedha. Sambamba na hilo, wakandarasi wa ndani wanaendelea kushiriki kwenye zabuni za ununuzi wa vifaa na ushauri elekezi, huku kiwango cha zabuni zinazotangazwa kitaifa kikiwa kimeongezwa hadi Sh bilioni 50 ili kuwapa fursa zaidi wazawa.