24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

TANROADS yasaini mikataba ya bilioni 67 ujenzi wa barabara Utete-Nyamwange

Na Gustafu Haule, Pwani

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) imesaini mikataba miwili yenye thamani zaidi ya Sh bilioni 67 na Wakandarasi wawili tofauti kwa ajili ya kutekeleza mradi wa barabara ya Utete -Nyamwage na daraja la Mbambe iliyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Mikataba hiyo imesainiwa leo Machi 20, 2023 wilayani Rufiji katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Azimio vilivyopo Utete chini ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Logatus Mativila na Wakandarasi hao huku ikishuhudiwa na Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya.

Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi  hiyo mhandisi Mativila, amesema kuwa mikataba iliyosainiwa leo inalenga kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Utete- Nyamwage kwa kiwango cha lami yenye kilomita 33.7 kwa gharama zaidi ya Sh bilioni 43.

Mativila amesema kuwa barabara ya Utete-Nyamwage inajengwa na mkandarasi china Railway Seventh Group limited huku daraja la Mbambe linajengwa na Mkandarasi Nyanza Road Works kwa gharama zaidi ya bilioni 24 na kwamba miradi yote itakamilika baada ya miezi 24.

Aidha, Mativila ameongeza kuwa ujenzi wa daraja la Mbambe utajengwa kwa urefu wa mita 81 pamoja na barabara unganishi za lami zenye kilomita 3.0.

Amesema daraja hilo kwa sasa linatumika ikiwa limejengwa kwa mbao na lina njia moja ya kupita na lina miaka 30 na kila mwaka hubadilishwa mbao na uwezo wake ni kupitisha gari lenye uzito wa tani tano pekee.

Mativila, aliishukuru Serikali kupitia Rais wa awamu ya Sita, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa ambayo imekuwa ikileta adha kwa wananchi wa Wilayani humo.

Mbunge Mchengerwa amesema kuwa anayepaswa kupewa sifa ni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwakuwa ndiye aliyefikia maamuzi ya kutoa fedha hizo.

Mchengerwa, amesema kuwa yeye ni mbunge wa tisa lakini katika kipindi chote hicho barabara hiyo haikuweza kujengwa jambo ambalo liliwakatisha tamaa wananchi wa Jimbo la Rufiji lakini maamuzi ya Rais Samia yamewapa faraja wananchi hao.

“Wananchi wa Jimbo la Rufiji walikuwa wanapata adha kubwa katika kusafiri kwani wapo wajawazito waliojifungulia njiani ,watu walikuwa wakisafiri masaa sita mpaka nane kufuata huduma za kijamii mjini Ikwiriri lakini Rais Dk. Samia ndani ya miaka miwili ameleta faraja kwa wakazi hawa,” amesema Mchengerwa

Mchengerwa amewaomba wananchi hao kumuunga mkono Rais Dk. Samia na viongozi wengine akiwemo yeye binafsi ili waweze kushirikiana kutatua changamoto zilizopo katika jimbo hilo.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya, akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa kwa wananchi kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Kasekenya amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya rais amekuwa wa kwanza Afrika kusimamia miundombinu ya barabara na daraja na kwamba lengo lake ni kuwaondolea adha wananchi kwa kuunganisha mtandao wa barabara nchini kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa wananchi.

Upande wake Kunenge amemshukuru Rais Dk. Samia kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuondoa kero na kuwatumikia wananchi na kwamba utekelezaji wa miradi hiyo ni ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, ameahidi kusimamia vizuri miradi hiyo ili iweze kukamilika vizuri huku akiwaomba wakandarasi wa ujenzi wa miradi hiyo kuheshimu mikataba na kumaliza kazi kwa wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles